Saturday, February 22, 2014

JINSI GANI YA KUFANYA KAZI NA ANAYEKUCHUKIA

JE unawezaje kushughulika na mtu anayekuchukia kazini? Hilo ndilo swali la msingi la kujiuliza. Na jinsi gani unaweza kuzuia usichukiwe na wafanyakazi wengine.
 
Kila mmoja ana hisia ambazo zinaweza kumwongoza afanye jambo Fulani ama asilifanye, kwa ajili ya kuzuia ghadhabu au kutokuelewana kusitokee.
 
Sasa ni kwa jinsi gani unaweza kushughulika na mtu anayekuchukia katika eneo la kazi.
 
Kuchukiwa ni hisia iliyopo kwa mtu ambayo mtu huyo anayemchukia mwingine badala ya kumpiga anamalizia hisia hizo kwa kumchukia.
 
Hii inamaanisha kuwa, kama kuna mtu anakuchukia kazini inaonyesha kuwa,  wewe ni mtu wa muhimu hivyo anatumia mbinu hiyo kukudhoofisha kisaikolojia.
 
Inakuaje akili ya huyo anayekuchukia inajiridhisha kuwa wewe ni adui wake wa kwanza? Na kwa nini anakuchukia hata kama hujafanya jambo baya kwake?
 
Wakati mwingine wewe unayechukiwa inawezekana umefanya jambo ambalo ni baya bila kujitambua. Kwa mfano imefikia mahali ukaonekana una akili kupita kawaida ambapo unaitumia akili hiyo  katika eneo la kazi watu wakuogope. Kutokana na hali hiyo ukachukiwa, hakikisha hauonyeshi hisia zako pindi unapochukiwa.
 
Hivyo, yule au watu wale wanaokuchukia eneo la kazi wataweza kuficha hisia zao hizo kwa kuwa wametambua wewe sio mtu mbaya kwao. Mtu anaweza kukuchukia katika kazi kutokana na wivu, kutokujiamini ama hofu.
 
 
Hali halisi inaonyesha kuwa, mtu ama watu wanaweza kukuchukia bila sababu kwa kuwa unawafanya wawe na hofu kila wanapokuona.
 
Ili kushughulika na watu wa aina hiyo ni lazima kwanza utafute sababu inayowafanya wakuchukie na kuonyesha kuwa hujali.
 
Ni jinsi gani utawazuia watu wasikuchukie katika eneo la kazi.
Kwa mfano umejua kuwa Fulani anakuchukia katika kazi kwa sababu anakuonea wivu, katika hali ya namna hii, unaweza kumsaidia mtu huyo nje na kazi kulainisha hali yake ya kuwa na wivu na kumpunguzia asikuchukie.
 
Ni muhimu sana kutokujifanya una akili sana mbele ya wale ambao hawatambui hilo , na wale ambao wanaweza kujenga chuki kwa ajili hiyo.
 
Pia epuka kujionyesha kuwa una mafanikio zaidi au mwenye akili, ili usijenge maadui wengine bila kujijua au kuwafanya watu wengi wakuchukie katika eneo la kazi bila kufanya jambo lolote baya.
 
Wakati mwingine unashauriwa kufanya makosa madogo madogo mbele ya watu wa aina hiyo ili tu kuwachanganya kwenye mafanikio uliyo nayo kiuhalisia.
 
Pia usijiweke wazi wakajua mipango yako uliyonayo wala kulinganisha ndoto zako kubwa ulizonazo kwa mawazo yao madogo waliyonayo.
 
Ushauri mwingine ni kutokujali mazingira ya namna hiyo, kikubwa kwako ni kusonga mbele.
 
Pia pale unaposulubiwa kwa jinsi yoyote ile onyesha kuwa hujali, we endelea kufanya kile unachotakiwa kukifanya.
 
Kanuni ya kukumbuka ni kwamba, simamia kile unachokiamini, hivyo tabia ya mtu mwingine isikusumbue, chukua muda kumfahamu vizuri mtu huyo na historia yake, pia kile kinachomfanya awe hivyo.
 
Kamwe unapokumbana na adha katika kazi, usitake kufanya ushindani na yule anayekutendea mabaya ili kujiepusha na migongano.
 
mwisho

0 Maoni:

Twitter Facebook