Thursday, April 4, 2013

Hizi ndizo njia za kufanikiwa kibiashara


ILI ufanikiwe katika biashara yako inakubidi uwe na jitihada za ziada.
Kadiri mtu anavyoongeza jitihada katika usimamizi wa biashara yake, ndivyo anavyopata mafanikio.
Inapaswa kutumia jitihada za kiakili na kimwili.
Watu wengi huanza biashara baada ya kuchoka kutokana na kufanya kazi aliyoajiriwa kwa muda mrefu au kupata ‘presha’ kutoka kwa bosi wake ofisini.
Hivyo fikra kubwa aliyonayo ni kwamba katika biashara yake anakwenda kupumzika kwa kuwa ana wasaidizi, kazi yake itakuwa ni kusaini hundi tu.
Mwisho anakuja kushtukia hakuna biashara inayoendelea kwa kuwa hakuonesha jitihada tokea mwanzo.
Kumbuka kuwa kufanya biashara si jambo rahisi, linahitaji nidhamu ya hali ya juu katika utendaji kazi.
Uanzishwaji na ukuaji wa biashara unahitaji muda mwingi zaidi ya wengi wanavyodhani.
Hapo inabidi ufanye kazi muda mwingi, na kubakia na fedha kidogo za matumizi ya nyumbani, hadi pale biashara yako itakapoimarika.
Biashara inahitaji nidhamu ya hali ya juu, hata kama hakuna mtu anayekufuatilia au kukuonya pale unapokosea.
Inakupasa kuwa kwenye biashara yako kama ulivyojipangia ratiba yako ya kila siku.
Watu watakuwa wanakutafuta, pale wanapokuhitaji inabidi wajue unapatikana muda gani, unapokosekana unawavunja moyo wateja wako na kukosa fursa ambazo zingekupatia faida.
Pia inakubidi kutumia muda wa ziada na rasilimali zaidi endapo mauzo yako hayaendi vizuri.
Fanya soko au biashara yako ionekane kwa wateja wako.
Pia ni vizuri katika biashara unayoifanya, isihusishwe na familia yako. Hapa inamaanisha hata kama unafanya biashara, endapo mwanafamilia atahitaji kitu itambidi akinunue sio kuchukua bure.
Kuruhusu biashara yako iwe holela kwa familia, kutafanya ifilisike baada ya muda mfupi.
Ni vema kuweka muongozo mzuri kwa familia yako ili jambo hili liendelee.
Ushauri mwingine ni kwamba, ili biashara yako isonge mbele inakubidi uwe mvumilivu.
Ni kawaida biashara yoyote haiwezi kukua kwa siku moja. Inachukua muda kueleweka kwenye soko, kukubalika na wateja na kuweka mtandao safi.
Inabidi uwe imara katika malengo uliyojiwekea katika kipindi kigumu utakachokipitia.
Biashara nzuri ni kama miti mizuri inayochukua muda kukua. Lakini pale inapokuwa inastahimili kimbunga cha aina yoyote.
Na kama unaijenga biashara yako katika eneo lenye misukosuko ya kibiashara inakubidi uandae msingi imara unaohitaji uvumilivu.

Mjasiriamali yeyote anaweza kufanikiwa


WATU wengi wameshindwa kuendelea mbele katika shughuli zao za kijasiriamali kutokana na changamoto wanazokabiliana nazo kibiashara.
Lakini ukweli ni kwamba mjasiriamali yeyote anaweza kufanikiwa katika biashara yake kama atafuata sheria na kanuni za kibiashara, ikiwemo kupata mafunzo ya ujasiriamali.
Kama unafanya biashara ambayo wateja wanapata huduma wanazohitaji kwa urahisi, ama michezo au sehemu ya kusoma barua pepe zao na kufanya shughuli nyingine zinazohusu mtandao, unakuwa kwenye nafasi ya mafanikio.
Lakini kama unapata eneo ambalo silo, utajikuta unafunga haraka biashara hiyo tofauti na matarajio uliyokuwa unayategemea.
Biashara nyingi zinafungwa ama kuwa na mafanikio, kutokana na msingi wa eneo iliyopo.
Kama eneo hilo ni zuri pia linavutia, watu wengi watafika kwa kuwa wanapenda vitu vizuri, huduma nzuri kwa wateja ama ubora wake.
Lakini kama eneo hilo si zuri, inahitajika nguvu ya ziada kwa ajili ya kuwashawishi wateja kufika, ambapo itakubidi bidhaa ziwe za gharama ndogo na kufanya jitihaza zaidi za ushawishi ili watu waweze kufika.
Nini kifanyike? Inabidi uchague eneo zuri kuliangana na aina ya biashara yako. Hakuna eneo zuri au baya, hata kama unafanya shughuli zako nyumbani mbali na wateja wako, patakuwa ni pazuri kwa baadhi ya biashara.
Itengeneze biashara yako kutokana na asili yake na kwa walengwa wako.
Katika hilo ni vema ukazingatia miundombinu, ulinzi na wasambazaji wako.
Wakati mwingine inapendeza kama utaanzisha biashara yako kwenye eneo ambalo biashara kama hiyo ipo. Kwa kuwa tayari eneo hilo litakuwa limeshazoeleka kwa bidhaa ya aina hiyo au huduma hiyo.
Pamoja na ushindani utakaokabiliana nao, utakuwa umepata mafanikio kwa kuwa eneo hilo tayari litakuwa la kibiashara.
Eneo zuri ni gharama, pia ni vigumu kulipata. Lakini pale unapolipata, unapunguza gharama za soko. Sio busara kufanya biashara katika eneo unalolipa gharama ndogo, ambapo matokeo yake unapata wateja ambao kazi yao ni kufanya utalii sio kununua.
Sababu nyingine ambayo inasababisha biashara nyingi kushindwa, zinakuwa hazianzishwi na wajasiriamali bali wataalamu mbalimbali ambao wanafikiri kuwa ni wajasiriamali.
Kinachofikiriwa hapa ni kwamba, kama mtu anajua kutengeneza bidhaa kitaalamu, anadhani kuwa anaweza kufungua na kuiendesha biashara bila kuwa na utaalamu wa kibiashara, lakini hili halina ukweli wowote, matokeo yake biashara inakwama.
Biashara nyingi zinakwama kwa kuwa wajasiriamali wengi hawana ujuzi.
Mjasiriamali yeyote anapaswa kuwa na ujuzi wa kibiashara, uelewa wa bidhaa zake anazozizalisha zinapopatikana pamoja na watu sahihi atakaoweza kuwatumia katika shughuli yake hiyo.
Kwa mfano, uendeshaji wa biashara ya shule ni zaidi ya kuwa mwalimu mzuri wa kufundisha. Kujua jinsi ya kutengeneza nywele haimaanishi kuwa unaweza kuendesha biashara ya saluni. Ama kuwa daktari mzuri haimaanishi kuwa unaweza kumiliki hospitali.
Kuanzisha shule hakumaanishi kunahitaji walimu wa ufundishaji tu, na saluni ni zaidi ya kutengeneza nywele, na hospitali sio tu kwa ajili ya kutibu wagonjwa.
Mauzo na masoko, mahesabu na kuwajali wateja ni zaidi ya shughuli zinazochangia mafanikio ya biashara.
Zaidi ya yote, unaweza kujua jinsi ya kutengeneza nywele lakini unakuwa dhaifu katika eneo la masoko au msimamizi mzuri wa fedha. Matokeo yake huwezi kupata wateja wa kutosha au kusimamia shughuli za kifedha, hivyo biashara kuyumba.
Kama wewe una fani yako halafu unataka kuanzisha biashara inayoendana na fani uliyonayo, usidhani kuwa unajua kila kitu. Pata muda wa kusoma jinsi ya kuendesha biashara, masoko, huduma kwa wateja na shughuli nyingine za kibiashara.
Njia nyingine ni kutafuta mbia ambaye ana uzoefu katika maeneo mbalimbali kama masoko, uhasibu na utawala.
Kama unataka kupata mbia kuwa makini kuepuka sababu nyingine zinazosababisha biashara kushindwa.
Kwa kufanya hivyo, biashara yako itakuwa yenye mafanikio.


Fanya biashara kuendana na wakati uliopo


WIKI iliyopita tuliona ni kwanini biashara inayoanza inashindwa kuingia kwenye ushindani kibiashara, na nini kifanyike ili kukwamua biashara hiyo.
Leo tutaangalia sababu nyingine inayokwamisha ama kuyumbisha biashara inayoanza.
Ni vema mfanyabiashara yeyote akajua muda wa bidhaa yake aliyonayo imetengenezwa lini na inakwisha lini matumizi yake ili kujua kucheza na soko lake.
Endapo umeanzisha biashara na hujafuatilia jambo hilo, inapofikia muda ambao bidhaa hizo zinakwisha muda wake, kwa vyovyote vile utapata hasara kwa kutojiandaa jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.
vile vile inakupasa kuwapa wateja wako kile wanachokihitaji. hapa ninamaanisha kuwa, inapaswa uuze bidhaa iliyopo kwa wakati na inayokubalika. Si busara kuuza bidhaa yoyote ile bila kuangalia mfumo uliopo wa utandawazi.
Kama ni mfanyabiashara wa magari inabidi uuze magari ambayo yanaendana na wakati uliopo, kwa kufanya hivyo utateka soko lako kwa haraka.
Tofauti na hivyo, bidhaa utakazokuwa nazo zitapitwa na wakati kwa kukosa wateja, mwisho wa siku zinaondolewa sokoni, hivyo kusababisha biashara.
Katika miaka ya sasa, teknolojia imeleta mapinduzi ya haraka katika biashara. Hivyo kampuni mbalimbali zimekuwa zikiboresha bidhaa zake kila mara ili tu kuwaridhisha wateja wake.
Hali imefanya bidhaa nyingi kuonekana zipo nyuma ya muda wake kwa kuwa haziendani na wakati uliopo.
Ili kuliteka soko lako, inakubidi uwape wateja wako kile wanachokihitaji ambacho kipo kwa kipindi hicho. Kamwe usiache kuagiza biashara ile inayokubalika kwa kuwa, wateja nao hawataacha kuinunua.
Unachotakiwa kukifanya hapa ni kila mara kuiboresha bidhaa hiyo kutokana na wakati uliopo, ili kuipa thamani bidhaa hiyo.
Chukua mfano wa kampuni ya magari ya Toyota na Ford, ni miongoni mwa kampuni zinazofanya vizuri katika kuboresha bidhaa yake hiyo duniani.
Kampuni hizo hazisubiri mpaka watu wakayachoka magari yao, bali hubuni aina mpya ya magari na kuiweka sokoni. Kwa njia hii, magari ya kampuni hiyo yamekuwa yakipendwa na watu.
Inatakiwa uwe na sababu za kutosha za kuwafanya wateja wanunue bidhaa zako kuwashinda washindani wako.
Kumbuka kuwa wewe ni mtumishi, wateja wako ni mabosi. Biashara yako ipo kwa ajili ya kuwahudumia wateja na si wateja kuihudumia. Kama mtumishi unapaswa kufanya kama vile mabosi ambao ni wateja wako wanavyotaka ili kufanikiwa katika biashara hiyo.
Kosa jingine ambalo linayumbisha biashara ni mpangilio mbaya ama kutokuwa na mpangilio kabisa. Hali hii huifanya biashara ndani ya muda mchache kutokusonga mbele.
Mara nyingi mtu anapotaka kuanzisha biashara anakuwa anajiamini kwa asilimia mia kuwa atafanikiwa bila kufanya utafiti wa kutosha kwa kuangalia vitu vidogo vidogo vinavyoweza kukwamisha biashara hiyo.
Wafanyabiashara wengi badala ya kuiangalia biashara ile kwa karibu na uzalishaji wake unavyokwenda, anang’ang’ania kuangalia mambo ya kiutawala zaidi, kama vile majukumu ya viongozi, masuala ya kisheria na huduma nyingine baada ya mauzo.
Kwa biashara ya kawaida, kutumia muda mwingi kwa ajili ya kutuma nyaraka mbalimbali au kuzijaza, kuboresha ‘website’, kuzungumza na simu, kusikiliza malalamiko ya wateja, kujibu malalamiko hayo na shughuli nyingine, kama hujajiwekea mpango mzuri kwa shughuli zote hizo, utakosa wateja au hutazalisha kwa kuwa muda mwingi utaupoteza katika shughuli za kiutalawa kuliko kuangalia uzalishaji na uuzwaji wa bidhaa.
Jambo unalopaswa kulifanya kabla ya kuanza biashara yako ni kufanya utafiti wa mahitaji yote yanayohitajika. Kuwa na mbinu za kiutawala ili kwamba usipoteze muda mwingi katika eneo hilo na kupoteza wateja.
Hapa inapaswa kuajiri watu wengine ambao watahusika na masuala ya kiutawala na shughuli nyingine. Unaweza kuwapa mafunzo ili waweze kukuwakilisha pamoja na biashara yako.
Pia njia nzuri ya kuepuka kufanya vibaya katika biashara yako ni kuandika mpango mkakati wako. Kwa kufanya hivyo utafikia malengo uliyojiwekea.
Kwa kuweka mpango mzuri utajua ni majukumu gani yanakuhusu na yapi unaweza kuyaachia kwa wengine. usijifunge kwa shughuli unazoweza kuwapa wengine wakazifanya. Fanya vile tu unavyoweza kufanya.
Kama unafanya kazi zako mwenyewe ama una wafanyakazi wachache, weka taratibu nzuri za kiutawala utafanikiwa.


Mbinu, kanuni za kufanya biashara


WATU wengi wanapoanza biashara wanakuwa hawafanyi utafiti wa kutosha, matokeo yake biashara wanazozianzisha zinakufa.
Hivyo basi, biashara unayoifanya ni vema ukazingatia vitu mbalimbali kabla ya kuifungua, ikiwamo eneo la biashara, samani pamoja na muonekano wake kwa wateja wako.
Baadhi ya watu wanaoanza biashara zao wanakuwa na makosa yanayojirudia mara kwa mara kwa kupangisha ofisi za gharama kubwa, kununua samani za bei kubwa pamoja na vifaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kutoa vipeperushi vya thamani kwa lengo la kuujulisha umma kuhusu biashara hiyo, bila kuangalia bajeti aliyojiwekea kwa biashara hiyo.
Lakini ni vema kujua mbinu na kanuni za kufanya biashara ili uweze kusonga mbele badala ya kurudi nyuma, ama kuifunga baada ya muda mfupi.
Mara nyingi wateja wanapenda kufanya biashara na watu wenye utaalamu wa biashara husika. Maana yake ni kwamba, mteja huyo anamuona mfanyabiashara huyo kuwa yuko makini na anaijali biashara yake.
Lakini kama tabia ya biashara yako ipo kinyume cha hali hii, yaani mfanyabiashara mwenyewe si mtaalamu wa biashara yake, wateja humkimbia.
Mfanyabiashara unaweza ukaiweka biashara yako katika mtazamo ule unavyotaka iwe, mfano jinsi unavyovaa, sehemu iliyopo na vifaa unavyovitumia, ni tafsiri tosha ya biashara yako iko vipi.
Pia unaweza kutumia fani yako ikakubalika kwa wateja uliowakusudia. Kwa mfano, kama unaanzisha mgahawa mdogo wa kuwahudumia wateja wa kawaida kama wafanyakazi wa ujenzi, hutakiwi katika biashara yako uwafanye wajisikie hawako huru.
Ingawa katika mgahawa wako una uwezo wa kuwawekea uma na visu, usifanye hivyo kama wako huru zaidi kutumia vijiko ama mikono yao.
Mfano mwingine, kuna saluni moja ya kifahari ilishindwa kusonga mbele kwa kuwa wamiliki hawakuzingatia mahitaji ya wateja walio nao. Katika saluni hiyo waliiweka katika daraja la juu na kujenga tafsiri kuwa wanaoingia humo ni wale tu wenye pesa zao, badala ya kulenga wateja wa eneo hilo husika, ambao walikuwa ni watu wa kawaida.
Hivyo hawakuwapata wateja wale waliowakusudia, pia wale wa kawaida ambao hawakuwalenga, kwa kuwa waliwadharau tokea awali. Hapa jambo lililokuwa linatakiwa ni kuwaweka katika mizani moja wateja wote wa daraja la kawaida na daraja la juu.
Kufanikiwa kwa biashara kunatokana na mwonekano wake. Kama mfanyabiashara unatakiwa kujenga mwonekano mzuri wa biashara unaoutaka, kwa kuonesha kuwa hilo ni eneo la fani yako.
Jambo jingine linalosababisha biashara zisiendelee ni pale mhusika anaposhindwa kupata soko la uhakika. Unaweza kuzalisha bidhaa za viwango vya juu pamoja na kutafuta masoko kwa wingi, lakini ukawa hauna soko la uhakika.
Utafiti unaonesha kuwa, wafanyabiashara wengi wanaanza biashara kwa kufanya utafiti wa juu juu bila kujiridhisha uhitaji wa biashara anayotaka kuianzisha kama atapata wateja au la.
Matokeo yake anatumia mtaji mkubwa, muda na nguvu wakati huo biashara hiyo inakuwa ndogo.
Nini kifanyike? Kabla ya kuanza biashara inatakiwa ufanyike utafiti wa kutosha wa kujua kama soko litakuwapo, ukubwa wa soko hilo na uimara wake.
Huhitaji kufanya utafiti wenye gharama kubwa. Unatakiwa kuzungumza na wateja wako kwa kuwauliza ni kwa kiasi gani wananunua bidhaa hizo na mara ngapi.
Zungumza na wasambazaji na washindani wako. Jua biashara nyingine zinakwenda vipi na jinsi gani wanaboresha masoko yao.
Kushindwa kwa bidhaa inawezekana inatokana na kushindwa kwa biashara. Sababu ya kushindwa kwa bidhaa inawezekana ni kutokana na maelezo ya mfanyabiashara husika, bidhaa yenyewe au soko. Hali hiyo ukikutana nayo labda uwe na bidhaa nyingine inayokuingizia kipato, ni vema kubadili biashara kuliko kuacha kabisa kufanya biashara.
Viashiria vifuatavyo huchangia kushindwa kwa biashara. Viashiria hivyo ni kuanzisha biashara katika muda mbaya ama kwenye kipindi kibaya cha hali ya hewa ya biashara husika, kulenga kundi ambalo sio sahihi, kutumia mikakati dhaifu, bei mbaya, kushindwa kuitangaza, kuiinua ama kuweka utayari wa bidhaa husika kwa wateja ili waweze kujua thamani na faida za bidhaa husika, pamoja na matarajio yasiyofikia malengo.
Kabla ya kuzindua bidhaa, ni vema kufanya utafiti ili kujua watu wanataka nini. Asilimia kubwa ya wafanyabiashara hawajui soko lao linahitaji nini, hivyo wanazalisha kile wanachodhani soko linahitaji, kuliko kujua soko linataka nini.
Lakini wakati mwingine, ni vigumu kujua soko liko vipi hata baada ya kufanya utafiti. Mfano mzuri ni pale unapochapisha, wachapishaji hufanya utafiti lakini bado vitabu vinakataliwa na wasomaji bila sababu za msingi.
Kuzuia kupata hasara zaidi, unashauriwa kuchapisha kiasi kidogo cha vitabu na kujua mwitikio wa soko lako.

Acha mawazo hasi


KATIKA makala zangu za Maisha Yetu niliwahi kuandika kwamba njia pekee ya kufanikiwa ni kutoruhusu mawazo yanayoleta kizuizi, kama vile kuwaza umaskini, kuwa na hofu au wasiwasi kila mara kwa kile unachokifanya.
Endapo wewe ni mtu wa aina hiyo inakupasa ubadilike ili usonge mbele kimafanikio.
Mara tu unapomaliza kuyachuja mawazo yako, unachagua yale unayotaka kuyafanyia kazi. Utagundua kuwa nayo yanahitaji kuongezewa ubora wake. Jifunze kutokufunga milango yako ya kuwa mbunifu.
Ni jambo lisilowezekana kati yetu kuwa kinyume cha ujuzi tulionao.
Mfano mtu hawezi kupita mbele ya gari liendalo kasi kwa kuwa anajua kuwa ataumia, hawezi kuogelea baharini kama anajua atazama, hawezi kuwa mstari wa mbele katika jambo la hatari kama anajua kuwa atadhurika.
Mafanikio hayahitaji kuwa na kiasi kikubwa cha ujuzi juu ya jambo fulani, lakini unatakiwa kung’ang’ania ili uweze kupata mafanikio hayo kwa ujuzi wowote ulionao.
Mkulima mmoja aliyejulikana kwa jina la Walter na ambaye siku za usoni angependa kuwa mchezaji bora wa mpira wa miguu, alimuuliza rafiki yake kuwa amewezaje kupata sh milioni 10 katika kazi yake anayoifanya kutokana na ujuzi alionao na kuweza kushinda kila dhana ya kushindwa ambayo ilikuwa inaibuka katika utendaji wake?
Rafiki huyo alimjibu kuwa wakati anaanza, alijua anataka kufanya nini na anachotarajia kukipata.
Alikuwa na njozi iliyomwezesha kujenga picha katika mawazo yake kulingana na malengo aliyotaka kuyafikia katika maisha yake.
Hivyo hiyo ndiyo siri kubwa ya mafanikio katika maisha yake.
Walter anasema kuna wakati alisikia umati wa watu ukishangilia katika mawazo yake.
Kuna wakati alijenga picha ya sherehe ya kupewa tuzo iliyojaa waandishi wa habari za michezo, wageni na wanamitindo mbalimbali.
Ndoto hiyo sasa ameanza kuifanyia kazi, hivyo anaamini atafanikiwa kama rafiki yake huyo alivyofanikiwa.
Inaonesha watu wengi wamekuwa hawako tayari kutulia na kufanyia kazi ndoto zile wanazokuwa nazo, kwa kuzipa nafasi ndogo katika utekelezaji wake.
Kuna mamilioni ya watu wanaoamini wanaangamia kwa umaskini na kushindwa kwa sababu baadhi ya malengo waliyonayo wamekuwa hawawezi kuyafanyia kazi.
Bila kujua watu wengi hujitengenezea mazingira mabaya kutokana na mawazo hasi yanayochukuliwa na mawazo na kutafsiriwa kwenda katika vitendo.
Kwa sasa hivi utaweza kutambua kwamba mawazo ni vitu ambavyo kama vikifanyiwa kazi vizuri na kutekelezwa vinaweza kuwekwa katika mfumo wa uhalisia.
Kama utakuwa na njozi za kupata zaidi na ukazijengea picha hiyo bila kujali utakumbana na vikwazo gani, hiyo itakuwa ni vipaumbele katika maisha yako.
Kama utaruhusu picha ya namna hii kuwa ya kudumu katika ulimwengu wako wa mawazo; utafikiri mawazo ya mafanikio na kuzungukwa na watu wenye mafanikio watakaotia moyo njozi zako.
Utatenga sehemu ya kipato chako kwa ajili ya kujilipa wewe mwenyewe, moja ya hatua muhimu katika kupata utajiri.
Utajihusisha katika mpango unaoleta mafanikio binafsi na kukufanya uchague lengo la maisha yako.
Pia utatafuta ujuzi na utaalamu kwa wale wote ambao wamefanikiwa. Mwishoni utafanikiwa licha ya kukumbana na vikwazo katika kutekeleza njozi zako.


Kufikiri kunaleta mafanikio


KWA mara nyingine nakukaribisha katika safu ya Maisha Yetu, ili uweze kujifunza mambo yaliyopo, yanayotokea na yanayoendelea kutokea katika dunia hii.
Miujiza inaweza kutokea kwenye maisha yako wakati unapotumia akili katika njia ya kukubali.
Na pale unapotambua kwamba kitu pekee kitachokutenganisha kutoka kwenye mafanikio au kushindwa ni vile unavyofikiri, unavyohisi na kuamini.
Kama unavyofikiri na kuamini kila siku, unakuwa tayari umeshapanda mbegu ya mafanikio au kushindwa katika mawazo yako.
Amini kuwa kufikiri na kuhisi kunakuletea mafanikio. Unaweza kuwa na vipaji vingi vya asili vinavyosubiri kuendelezwa, jitahidi kuvivumbua.
Amini kuwa vipaji vyako ni vya thamani na unaweza kuvitimiza kwa kuvifanyia kazi. Amini kushinda mara kwa mara katika vita ya ushindi.
Ni bora kuwa na imani ndogo ya kufanya jambo kuliko kukosa kabisa. Huwezi kuwaza mara moja kuwa unataka kuhamia kwenye nyumba mpya bila kufanya maandalizi.
Lakini unaweza ukapata wazo hilo, ukalipangilia, ukachukua hatua na mwishoni ukapata matokeo mazuri.
Unaweza kuwa na mawazo mazuri yaliyojaa utajiri katika maisha yako, afya njema na furaha kubwa kwa kumwamini Mungu.
Maendeleo hutokana na changamoto mbalimbali unazokabiliana nazo. Unaweza kukua kwa kukutana na changamoto hizo na hapo ndipo utakapopata mafanikio, japo kwenye mafanikio vikwazo mbalimbali hutokea lakini inakubidi usikate tamaa.
Chukua changamoto mbalimbali kama mafanikio. Unapokutana na changamoto katika kupata mafanikio yako kabiliana nazo utashinda.
Mafanikio huja wakati unafanya jambo lenye ubunifu. Hujaumbwa kwa ajili ya hali fulani, bali umeumbwa kama wakala uliye huru wa maamuzi yako ambayo yako ndani ya uwezo wako.
Ukiwa na mawazo, malengo na changamoto za mafanikio ndipo utakapofanikiwa. Unafanya shughuli yoyote kwa ajili yako mwenyewe.
Izoeshe akili yako ikubali kila unalolipanga unalitimiza kwa kuchukua hatua zote muhimu kuanzia hapo ndipo utakapoona mafanikio yako.
Kushindwa mara moja haimaanishi kwamba utashindwa siku zote, si kwamba mmoja anapofanikiwa atakuwa na mafanikio ya kudumu mpaka pale atakapotumia mafanikio hayo kwa kupiga hatua zaidi.
Maisha ni hatua
Umezaliwa ushinde na utashinda kama utaamini ukweli huo. Ni asili ya mwanadamu kuwa na hali ya wasiwasi.
Wasiwasi juu ya familia yake, majirani, kazi na maisha yake. Kumbuka wasiwasi unasababisha hofu na ndiyo chanzo kikuu cha kushindwa.
Unapokuwa na hofu juu ya siku ya kesho, haileti maana kwani hujui siku ya kesho itakavyokuwa kwako. Usiishi kwa ajili ya kesho, bali kwa ajili ya siku iliyopo yaani leo.
Kama una wasiwasi juu ya yatakayotokea kesho, mwezi ujao au mwaka ujao, unajiweka katika hali ya kushindwa katika mafanikio yako kwa kuvuruga mawazo mazuri uliyojipangia.
Kamwe usifikiri kuhusu matatizo ya kesho, ishi siku ya leo kwa kufanya mipango mizuri uliyoipanga.
Huwezi kufanikiwa kama unakaribisha wasiwasi au hofu katika maisha yako. Kama una wasiwasi wa ratiba yako uliyoipanga kwa siku zijazo, ni kupoteza nguvu zako.
Shughulika na mambo yale ambayo ni ya muhimu. Fanya kitu kimoja kwa wakati, kazi moja kwa wakati, usichanganye mambo.
Unaporuhusu wasiwasi unakaribisha umaskini katika maisha yako. Kamwe usihofu kuhusu hali ya maisha yako ya siku zijazo.
Ujasiri na jitihada katika maisha ndiyo unaotakiwa. Kubali na kabiliana na changamoto unazokumbana nazo bila kuziogopa.
Fikiria matarajio uliyoyapanga na uyape kipaumbele katika akili yako na mboni ya jicho lako. Kuwa jasiri katika kila hatua unayopitia.
Jua kwamba lazima utafanikiwa na simama katika ukweli huo. Jua kuwa kila siku ni mpya.
Kesho bado haijafika hivyo ukiwa na hofu kwa ajili ya kuhofia matatizo ya siku ya kesho ni sawa na kupoteza nguvu katika akili yako.
Ni vema kuzungumzia mafanikio katika kila jambo unalolifanya sasa.
Kama unasubiri mafanikio yakufuate, unakosea.
Ni vema kuchangamkia mafanikio. Kila jambo linalokuletea mafanikio lipo sasa, amani katika moyo wako unaweza kuwa nayo sasa.
Unaweza kuwa na mafanikio na afya njema uliyokuwa nayo sasa. Kila mara usiwaze yaliyopita au kushawishika kuishi matamanio ya siku zijazo.


JINSI YA KUEPUKA KUPATA HASARA


KATIKA biashara yako hali inapokwenda mrama ni vema kuweka tamko la kusitisha hasara uliyoipata, kwamba hauko tayari kukubali hasara hiyo iendelee.
Jitahidi kuweka mikakati zaidi ya kuiboresha biashara yako na kuomba ushauri wa kimaendeleo kwa wafanyabiashara waliofanikiwa.
Tumwangalie mfanyabiashara John Robert, aliyekuwa amepewa fedha na rafiki zake kiasi cha dola 200,000 za Kimarekani, ili kuwekeza katika soko la hisa.
Baada ya kupewa fedha hizo na kuzifanyia biashara, Robert alifikiri kuwa angepata faida ambayo ingemfanya awe na maendeleo zaidi katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya ilikuwa kinyume na matarajio yake.
Awali, alipoanza biashara hiyo alipata faida iliyomfanya asiwe mbunifu katika biashara yake, lakini matokeo yake ni kwamba baada ya muda mfupi alifilisika.
Mfanyabiashara huyo, baada ya kufilisika alipata hofu kutokana na fedha alizopewa kwa ajili ya kufanya biashara.
“Sikujali kupoteza pesa zangu mwenyewe,” anasema mfanyabiashara huyo ambaye kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake, kutokana na kupoteza pesa za rafiki zake.
Lakini, mara baada ya kufanikiwa kuishinda hofu iliyokuwa ikimkabili, alijikuta amepata ujasiri mpya na kwenda kuwakabili tena rafiki zake na kuwaeleza kilichomsibu.
Pamoja na maelezo hayo, rafiki wale hawakuonesha mshangao katika jambo hilo, bali walilichukulia kuwa la kawaida. Lakini kwa upande wake ilionekana halitatibika.
“Nilijua nilikuwa nafanya biashara katika mtindo wa 'pata potea' nikitarajia zaidi bahati na mawazo ya watu. Nilikuwa nikishiriki katika soko la hisa kwa kusikia,” anasema.
Kwa maelezo ya Robert, alianza kufikiria makosa yake na kufanya uamuzi kabla ya kuamua kurudi kwenye soko kwa mara nyingine. Alijaribu kutafuta chanzo cha jambo hilo, pia alifikiri na kuamua kuja na mwongozo mpya wa mafanikio.
Baada ya hali hiyo kumtokea, alitafuta ushauri kutoka kwa rafiki zake, kwa kuwauliza ni jinsi gani wameweza kufanikiwa na kuendesha biashara zao, ambazo zinakwenda vizuri.
Mmoja wa rafiki zake, aliyeendesha biashara yake vizuri, alimweleza akiweka tamko la kusitisha hasara katika hofu yake kwenye majukumu aliyojipangia. Hivyo, mtu yeyote anaweza kuondoa tabia ya hofu aliyonayo.
Popote unaposhawishika kuweka pesa zako baada ya kupoteza, ni vizuri kutulia na kujiuliza maswali yafuatayo: Ni kwa kiasi gani umekuwa na hofu kuhusu jambo fulani juu yako? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika hofu inayokukabili na kusahau? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika wasiwasi na kusahau?
Kumbuka unapoanza kuwa na hofu ya vitu vilivyopita na kufanyika, ni kama unakuwa ukijaribu kupanda mazao yako kwenye vumbi.
Maana yake ni kwamba yale yaliyopita usiyasumbukie, bali ugange yajayo. Ukiendelea kuyasumbukia utajisababishia mikunjo katika paji la uso wako na vidonda vya tumbo.
Hivyo, endapo una tatizo la kukumbuka mambo yaliyopita, iambie nafsi yako kwamba huishi kwa ajili ya mambo hayo. Badala yake unaweza kuwa na mipango mizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako.
Unaweza kujishughulisha kwa kuandaa mashindano mbalimbali kama vile muziki, ngumi au uchoraji.
Lengo ni kuwa unajishughulisha kila mara ili usiwe na nafasi ya kufikiria mambo yaliyopita ambayo yamekusababishia hasara na hofu maishani mwako.
Tukutane Alhamisi ijayo.
Makala hii ni kwa msaada wa mtandao wa inteneti na kitabu cha ‘Ondoa wasiwasi anza maisha mapya’.

Wednesday, April 3, 2013

UKOSEFU WA MAWAZO HUUA BIASHARA


KILA siku mamilioni ya watu wamekuwa wakikabiliana na changamoto mbalimbali katika dunia hii tunayoishi.
Mbali na misukosuko katika ndoa au mahusiano ya mwanamke na mwanamme, hali inayochangia kutokuelewana, msongo wa mawazo, ugonjwa, wengine hufikia hatua ya kujinyonga.
Kadhia nyingine kubwa ni kuhusu kushindwa au kufilisika kwa biashara aliyonayo.
Kutokufanikiwa kwa biashara hizo kunatokana na mipango katika biashara, masoko na suala la kifedha.
Pia inakuwa si rahisi kujua kwa undani ni kwanini biashara ndogo zinakufa. Haitoshi kusema kuwa ni kutokana na ushindani wa kibiashara uliopo, ama mabadiliko ya teknolojia, madeni, mauzo madogo, ama huduma mbaya kwa wateja.
Yote hayo ni ugonjwa unaosababishwa na usimamizi mbovu katika biashara husika.
Mbali na hayo, ujuzi binafsi, elimu, kujituma na ari ya kazi ndivyo vinavyohitajika katika utawala wa biashara.
Biashara nyingi hushindwa kuendelea kutokana na ukosefu wa mawazo mazuri. Zinaweza kufa kutokana na muundo mbaya wa uwekezaji katika biashara.
Mara zote kumbuka kuwa, mpango mzuri wa biashara ni muongozo wa kufikia malengo ya kibiashara unayoyatarajia, hata kama kutakuwepo na baadhi ya vikwazo katika biashara ile unayoifanya.
Kumbuka kama huna mpango mzuri katika biashara uliyonayo, ni sawa na kuwa na silaha ambayo huwezi kuitumia wakati wa mapambano.
Jambo la kuelewa ni kwamba, kama hauna ujuzi wa kuendesha biashara yako, unajiweka kwenye nafasi mbaya ya kushindwa kuiendesha sio kwa sababu biashara hiyo haina faida, bali ni kwa kuwa unashindwa kuisimamia katika misingi inayotakiwa, kwa kuona ufahari kuwa na biashara ambayo haisongi mbele.
Jambo muhimu unapochagua kufanya biashara ni vema ukachagua ile ambayo una ujuzi nayo pia unaielewa kwa undani.
Unaweza kuwatumia wale watu wenye vipaji ama wenye uaminifu katika biashara ambao wataweza kukusaidia kwa kile unachotaka kukifanya.
Wape nafasi ya kukuongoza na kukufanyia tathmini au kukueleza kuwa hawakubaliani nawe pale unapokwenda tofauti katika biashara.
Ikumbukwe kuwa biashara nyingi zinaanza vizuri, lakini mwisho wake unakuwa mbaya, kwa kuwa biashara inaendelea kukua na wale wasimamizi wake wanashindwa kuisimamia vizuri kutokana na mahitaji yaliyopo kwa wakati huo au kutokuweka wafanyakazi wazuri wanaoweza kuleta ushindani kwenye soko.
Mfano mzuri katika hili, ni pale mfanyabiashara mdogo anapoanzisha chuo na baadaye kinakuwa chuo kikuu.
Hapa utaona kuwa wale wafanyakazi aliokuwa nao katika chuo kile akiwemo yeye mwenyewe, hawawezi kuwa na ushindani katika kuendesha chuo kikuu.
Kwa kuwa chuo kikuu kinafanikiwa kwa kuweka watu wenye uzoefu na ujuzi, ambao kiwango chao cha elimu kinaridhisha.
Hata mfanyabiashara mkubwa, Bill Gate ambaye ni mwanzilishi wa Microsoft, amefikia hapo alipo kutokana na kuwa na timu imara ya watu wanaomzunguka.
Kama mwanzilishi wa biashara yako inakubidi kujua ni wakati gani wa kuchukua watendaji wenye ujuzi katika biashara unayoifanya.
Kwa upande mwingine katika siku za leo, suala la masoko linaonekana kuwa muhimu kuliko bidhaa husika. Mlaji analundikiwa bidhaa nyingi zenye matumizi yanayofanana.
Hivyo inabidi kuwe na kampeni kubwa kwenye timu ya masoko ili kuweza kuuza bidhaa hizo.
Kumbuka kipindi kile ambacho bidhaa zilikuwa zikijiuza zenyewe kimekwishapita. Hivyo wajasiriamali wengi wanashindwa kujua ukweli huu katika kipindi hiki cha ushindani.
Wafanyabiashara hao wamekuwa wakifanya jitihada kubwa na kutumia muda mwingi kutengeneza bidhaa bora na kuziweka sokoni bila kujihangaisha kuhusu kutafuta masoko.
Matokeo yake, hutumia pesa nyingi kwenye kuendeleza bidhaa na pesa kidogo kwenye kutafuta masoko ya bidhaa hizo, mwisho wa siku, mapato hupungua na wanafilisika na kuondolewa sokoni na wapinzani wao ambao wanajua mikakati ya kupata masoko kwenye biashara walizonazo.


Twitter Facebook