Friday, August 28, 2009

SAHAU MAUMIVU ULIYONAYO UPATE FURAHA

WIKI iliyopita tuliangalia jinsi ya kudhibiti hisia zetu ili tuendelee kuwa na furaha, imeonekana kuwa watu wengi wameshindwa kudhibiti hisia walizokuwa nazo na kujikuta wako katika hali ya kukata tamaa, pamoja na kuvunjika moyo.

Katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi inavyokupasa uyaachie mambo yanayokusumbua, ili uishi kwa furaha. Tutaangalia jinsi ya kuachana na mambo mbalimbali tunayokutana nayo katika maisha ili kuweza kupata amani na utulivu katika mioyo yetu.

Kumbuka kuwa kama una tabia ya kuachana na ya maumivu na huzuni unayokabiliana nayo, utakuwa na maisha mazuri, lakini kinyume cha hapo, utaendelea kuwa mtu asiyekuwa na furaha siku zote.

Na pia ufahamu kuwa, kila mmoja wetu hukabiliana na changamoto mbalimbali katika sehemu fulani ya maisha yake, kama vile, hali ya huzuni au kukataliwa lakini njia nzuri ya kuishi vizuri ni kuwa jasiri katika kuikabili hali hiyo.

Japo wapo watu wengine hudhani, kwa kuwa wao ni washika dini sana, hali ya huzuni, kuhangaika, kukata tamaa haitawapata, la hasha! Kila mmoja anapatwa na hali hiyo, ila ni uamuzi wako kuchagua ni jinsi gani unapenda uwe, kuwa na furaha ama kutokuwa nayo.

Pia ukiangalia watu wengi ambao hawana furaha, hukabiliwa na magonjwa mbalimbali. Huweza kuwatambua kwa kuwaangalia muonekano wao kiafya, vile vile hupatwa na maradhi kama shinikizo la moyo, moyo kudunda kwa nguvu, kupooza na hata wakati mwingine kuugua kansa ambayo huzalishwa na hali ya msongo wa mawazo.

Kwa upande mwingine wa maisha haya tunayoyaishi, ujue kuwa nayo yana kanuni zake, kama unataka watu wakutendee mambo mema, nawe pia watendee yaliyo mema, kwa kila jambo unalotenda.

Kwa kila tendo jema, kuna mwitiko ulio mzuri, kinyume cha hapo hutabaki kuumia na kukosa furaha maishani. Wema wako unaowatendea wengine, ndivyo hivyo nawe utapokea katika maisha yako kutoka kwao.

Tiba ya kuishi maisha ya furaha ni hii ‘kuwa mzuri, kuwa mwema, usiwe mbinafsi. Watendee wengine vile unavyopenda wakutendee wewe’.

Kama kweli umedhamiria kupata furaha ya kutosha maishani, tumia kanuni hiyo ya maisha na kuifanyia kazi.

Kama unataka kuwa rafiki wa watu, nao wawe rafiki zako. Kuwa rafiki kwao na kama umezungukwa na watu wasio wazuri kwako, wabadili wawe watu wazuri kwa kuonyesha wema wako kwao, haijalishi jinsi watakavyokuchukulia.

Je, unadhani utawabadilishaje ili wawe watu wazuri? Ni kwa kushirikiana nao katika mambo yaliyo mema na kuwajali. Inawezekana wanaweza wasikukubali kirahisi, lakini jitahidi kuwa mwema kwao, bila kujali wanachokisema wala kukinong’ona.

Hebu tuangalie mfano wa mama mmoja, aliyekuwa ameolewa lakini hakuwa na furaha na mumewe, kwa kuwa kila alichokifanya mumewe huyo alikikosoa.

Mwanamke huyo aliamua kutafuta msaada kwa kiongozi wake wa dini na kumweleza kuhusu mumewe kwamba kila aliporudi nyumbani alikuwa na hasira na kukosoa kila jambo aliloliona limefanyika.

Lakini mama huyo, alipoomba ushauri, aliambiwa kuwa, inawezekana yeye ndiye chanzo cha yote kabla ya kumsema mumewe, ni vema akajiangalie yeye kwanza, jambo alilokubaliana nalo na kulifanyia kazi, baada ya muda, mumewe alibadilika. Furaha ikatawala nyumbani kwao.

Mwanamke huyo alisema, aliamua kubadilika kwa kumjali mumewe na kuwa karibu naye, bila kujali vile alivyokuwa akimtenda na kwamba kila mumewe huyo aliporudi nyumbani, na kuanza kukosoa kama alivyozoea, kwa kuwa mwanamke alikubali kubadilika, alijitahidi kumhudumia kwa upendo, kumpatia chakula, juisi na kumpa maneno matamu, bila kujali jinsi alivyokuwa akifoka kwa hasira.

Alisema aliendelea kuwa karibu na mumewe kila siku na mwishoni mumewe huyo alibadilika tabia yake ile aliyokuwa nayo. Kama unataka kuyabadili mazingira magumu unayokutana nayo, ni vema ukaanza kubadilika wewe kwanza.

Fikiri juu ya hili. Je, ni jambo gani linalotufanya kuwatendea watu mambo mema? Ni kwa kuwa, nasi tunapenda kutendewa mambo mema pia? Kamwe tusiruhusu hali ya chuki na hasira katika maisha tunayoyaishi. Mbaya zaidi hali ya hasira zilizofichika ndani vinginevyo utapata maumivu na majeraha yaliyofichika ambayo yanahitaji kuponywa.

Majeraha hayo yaliyofichika hukusababishia hasira, ugomvi ama hali yoyote ambayo hupendi utendewe na mtu mwingine. Baadhi ya dalili zinazomfanya mtu aonekana kama ana majeraha yaliyofichika ni maneno yake, mwonekano na vitendo vyake.

Sasa basi njia ya kukabiliana na maumivu ya ndani uliyonayo ni kuyasahau na kutokumbuka mambo uliyowahi kutendewa. Watu wengi wanakosa furaha ya kweli, kwa kuwa wamekuwa wakikumbuka jinsi walivyotendewa na baba au mama yake, alipokuwa mdogo, mke au mme wake alivyomtendea siku za nyuma, kwa kuwa wanashindwa kusamehe, miaka inapita huku maumivu hayo yakiwa yanaendelea.

Usilaani. Kamwe usiruhusu maumivu yakakufanye mtu mwenye uchungu, jaribu kusahau, kumbuka kuwa, huwezi kusahau maumivu yaliyokupata kama utakuwa unayakumbuka kumbuka.

Tukutane Alhamisi ijayo.

HALI YA KURIDHIKA INAONGEZA FURAHA

KATIKA mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya, ambapo leo tutaangalia jinsi ya kudhibiti hisia zetu ili tuendelee kuwa na furaha.

Watu ambao hawawezi kudhibiti hisia zao wanajikuta wako katika hali ya kukata tamaa na kuvunjika moyo.

Lakini ukweli ni kwamba, inakupasa usikate tamaa mpaka kumwazia Mungu wako mambo mabaya, kutokana na wewe mwenyewe kushindwa kudhibiti hisia zako.

Hivyo ni vema kuwa imara katika hisia zako, bila kujali kama unapitia hali ya milima na mabonde, ili kutimiza malengo yako uliyojiwekea, kinyume cha hapo, utaendelea kuwa mtu usiyesonga mbele kutokana na hali ambayo umeiruhusu, ilhali ungeweza kuidhibiti.

Mfano mzuri ni kwa mtu aliyeelimika, kwa kuwa yuko tayari kufundishika, ambaye ni muelewa, hataabiki kwa kuonyesha kuwa anajua kila kitu, hata kama anajua.

Huwa na utayari wa kujifunza kila mara, ni msikivu. Na kama njia yake haiko sawa sawa, anakuwa tayari kubadilika, mtu wa namna hii, ni rahisi
kuwa na mafanikio ya haraka.

Pia mtu wa aina hii, endapo hajui jambo fulani, hukubali kuwa hajui na huwa tayari kukiri hivyo. Mtu wa aina hii, yuko tayari kusikiliza wengine, iwe ni mzee, kijana, mwenye busara ama mwenye uzoefu zaidi yake, humsikiliza.

Hakuna ubishi, kutoelimika ni jambo la hatari, hivyo ni busara kila mmoja akapenda kuelimika bila kujali umri alionao, kwa kuwa atapata busara zaidi na mafanikio ikiwa ni pamoja na kujisimamia katika maamuzi yake, kabla ya kufanya jambo linaloweza kumharibia kabisa.

Kamwe usikubali kujishusha thamani yako na kujiona wewe si kitu, kwamba huwezi kufanya jambo fulani, kwani huo si ubinadamu. Bali inakupasa kupiga moyo konde na kusonga mbele, hata kama kuna hali ngumu inayokukatiza, jaribu kukabiliana nayo.

Kujikubali ulivyo ni pamoja na kuwa tayari kukubali kuwa watu wengine pia wanaweza kukusaidia pamoja na kukupa uwezo wa kujiamini kuweza kukiri upungufu ulionao.

Kuwa wazi, kuwa mnyenyekevu, jisahihishe na penda kuelimika. Kwa kufanya hivyo, utaweza kuishi kwa furaha na amani.

Wengi wetu tumejikuta hatuna furaha katika maisha yetu, kwa kuwa tunajitaabisha na mambo mengi na kujikuta kila wakati wewe ni mtu wa shughuli na mipango mingi isiyokwisha.

Kwa maelezo mengine, tunashindwa kuwa na furaha kila siku, kutokana na hisia zetu kuzielekeza kwenye shughuli na matukio ya siku inayofuata.

Tumekuwa na shughuli nyingi katika mipango ya maisha, hali inayotufanya kushindwa kuwa na furaha kwa muda uliopo.

Ebu tuangalie mfano wa mtu mmoja ambaye mwanzoni alifikiri kuwa, endapo angekuwa na nyumba yake angekuwa na utajiri ambao ungempatia furaha, lakini hilo lilipotimia alihitaji kitu kingine zaidi.

Alijikuta akihitaji nyumba nyingine kubwa zaidi. Wakati ukafika, akapata nyumba nyingine, lakini alijikuta kila wakati akifurahia nyumba yake ya awali, hivyo ilimlazimu kwenda kwenye nyumba yake ya awali, mara kwa mara.

Ilifikia mahali akasema kila alivyozidi kujiridhisha kwa kupata kile alichokihitaji, ndivyo alivyokuwa hafurahii vitu alivyokuwa navyo na kutamani kupata vingine zaidi. Hapa tunaona ni vizuri kuwa na kiasi katika maisha tunayoyaishi.

Hapa tunajifunza nini? Mwanadamu yeyote kama hana tabia ya kuridhika, anakuwa anajiongezea hali ya kukata tamaa na hata kuishi kwa hofu, kwa kutokufikia malengo makubwa aliyojipangia.

Ni sawa na kuamka usiku wa manane na kwenda kwenye jokofu kulifungua lakini hujui ni nini hasa unachokihitaji.

Kwa kuwa hujui unachokihitaji, unajikuta ukigusa hiki, unajaribu na kingine lakini katika vitu vyote hivyo hakuna unachokisikia ni kitamu.

Mwisho unafunga jokofu lako na kurudi kulala, huku bado ukiwa na njaa, hujatosheka.

Tunaona wengi wetu tunafanana tabia zetu kwa kuwa na hisia zisizotimizika.

Ili tuwe na mafanikio, inabidi kufanya uchaguzi katika kila tunachokiwaza. Inatakiwa kuondokana na mawazo yatakayoturudisha nyuma, kuwa na mawazo mazuri, ndoto nzuri na kufanya kazi kwa bidii.

Tukutane Alhamisi ijayo.

IKUBALI HALI ULIYONAYO UPATE FURAHA

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi.

Leo tutaangalia jinsi unavyoweza kupata furaha kwa kuikubali hali ya upungufu uliyonayo.

Si rahisi kwa mtu yeyote kukubali hali ya uhitaji aliyonayo, lakini kufanya hivyo ni jambo la muhimu.

Ni ukweli usiopingika kuwa, katika maeneo yote ya maisha tunayoyaishi, kanuni zake zinafanana.

Na kwamba, unakuwa na furaha pale tu unapokubali hali ile ya upungufu uliyonayo, kwa kuwa hapo ndipo kwenye hitaji lako.

Kama ni kweli kuwa kila mmoja wetu hajakamilika katika eneo fulani katika maisha, kwa nini basi unakuwa hauko tayari kuikubali hali hiyo?

Wengi wetu tumekuwa hatuko tayari kukubali hali ya upungufu tuliyonayo, kwa kuhofia kuwa jamii inayotuzunguka itatucheka, kututenga ama kudhalilika.

Lakini kinachotakiwa hapa, ni kutoogopa jambo lolote lile, liwe kutengwa, kukataliwa ama kudharauliwa.

Sasa ni jinsi gani hali hii ya kuwa na furaha inaweza kukubadili wewe na mimi? Ni pale tu utakapoonyesha unahitaji msaada ama una upungufu.

Kwa mfano unaweza kuhitaji msaada kwa mtu yeyote kwa kumuuliza maswali yafuatayo: "Nimepata tatizo, je, waweza kunisaidia?, "Sielewi jambo fulani unaweza kunielewesha?, "Sijakubaliana na wewe, je, tunaweza kuonana mahali na kujadili zaidi?", "Nimepata hasara, je, waweza kuniongoza cha kufanya?"

Maswali ya namna hiyo ndiyo mwanzo wa kukuweka huru katika maisha yako. Hivyo furaha inakuwepo kwa mtu yeyote yule anayejua kuwa, eneo fulani ana upungufu hivyo anaukubali na kuhitaji msaada kwa wengine.

Kama wewe hauko tayari kulikubali jambo linalokusumbua, usishangae usipoona kuwa, wengine hawakujali.

Hivyo suluhu ni kujiweka mbele, jaribu kuwa mtu fulani ambaye hukuwahi kuwa hivyo, pamoja na kujiweka maridadi wakati wote.

Na ukweli ni kwamba, katika hali ya kuumia uliyonayo, kuna mtu ambaye yuko tayari kukusaidia juu ya upungufu wako, endapo tu ataelewa tatizo lako na kuliachilia. Lakini kama utajionyesha kuwa huna matatizo, hakuna njia ambayo mtu yeyote ataweza kukusaidia.

Wakati wote kuna mtu ambaye yupo tayari kukusaidia. Na kwamba mtu yeyote husaidiwa pale atakapokubali kuwa ana uhitaji katika sehemu fulani.

Kuna mfano wa mtu mmoja ambaye alikuwa ni mtumwa wa ulevi kwa muda mrefu, aliteseka katika hali hiyo kwa kuwa hakuwa tayari kuikubali. Na pale alipoelezwa kuhusiana na athari zinazoweza kumpata, hakuwa tayari kupokea msaada.

Siku moja baada ya kulewa kupindukia na kugonga gari lake alilokuwa akiliendesha, kwa maneno yake mwenyewe alijikuta akisema kuwa: ''Nimeteseka kwa ulevi kwa muda mrefu, kwa kuwa nilikuwa nasema kuwa, ninaweza kuudhibiti unywaji wangu, nilikataa ukweli kuwa nilikuwa mlevi niliyepitiliza, ningepokea uponyaji endapo ningeonyesha ninahitaji msaada. Na sasa baada ya hali hii kunikuta ninahitaji msaada na kubadili maisha yangu."

Tokea siku hiyo, maisha ya mtu huyo yalibadilika kwa kuwa alijitambua na kuhitaji msaada.

Kwa upande mwingine, furaha ya kweli inapatikana pale ambapo unaacha hali ya kulaumu. Ama kumlaumu Mungu au kujilaumu mwenyewe.

Watu wengi wanapopata matatizo hujikuta wakimlaumu Mungu ama kujilaumu wenyewe, badala ya kutafuta njia ya kumtoa hapo alipo ili aweze kuwa huru.

Sasa basi endapo umefikia hatua ya kukata tamaa ya maisha, umekutana na kipindi kigumu, kamwe usimlaumu Mungu kwa kuwa kufanya hivyo hutapata jibu la tatizo ulilonalo.

Makosa mbalimbali ambayo mwanadamu huyafanya pindi awapo katika hali ngumu ni yale ya kuhukumu, yatokanayo na utashi, sababu, ubinafsi, ukaidi, upumbavu na mengineyo yafananayo na hayo. Yote hayo ni chanzo cha binadamu kinachomfanya awe maskini na kuteseka.

Ama wakati mwingine unakuta mtu analaumu kwa ugonjwa alionao, ilhali wakati mwingine yawezekana yeye mwenyewe ameshindwa kujilinda mpaka akapata magonjwa.

Kwani kwa upande mwingine tunaweza kusema kuwa, magonjwa mengi sisi wenyewe ndiyo tunayasababisha kwa kutokula vizuri, kutokulala vizuri, kutokufanya mazoezi vizuri, kutopumua vizuri, haya yote ni kutokana na mazingira yanayomzunguka binadamu. Hivyo tunaona mambo mengine ni sisi wenyewe tunajisababishia na Mungu si wa kulaumiwa.

Mengi ya magonjwa hayo, huwapata wanadamu kutokana na uelewa mdogo ama elimu waliyonayo juu ya athari zinazoweza kutokea endapo ulishindwa kufanya jambo fulani.

Vile vile si vizuri kujilaumu wewe mwenyewe kutokana na hali inayokukabili, kwani kwa kufanya hivyo hutaweza kutatua tatizo linalokusumbua wala kuibadili hali hiyo.

Unaweza kupata hali ya kufiwa na mtoto, mzazi ama mume wako mpenzi, hali itakayokufanya ujitenge na wenzako, uache kujichanganya na kufanya mambo mengine ya kukusaidia, kutokana na hali iliyokukuta endapo hautakuwa makini na kuendelea na shughuli zako za kila siku, utajikuta hali yako kimaisha na kiuchumi inazidi kudidimia.

Katika hali kama hiyo, ndugu ama rafiki zako hawataweza kuyainua maisha yako siku zote, watakusaidia kwa sehemu tu, lakini itabidi nawe unyanyuke na kutoka katika hali ile ya kutokuwa na furaha na kujichanganya ili uweze kusukuma gurudumu hili la maendeleo.

Tukutane Alhamisi ijayo

TATUA TATIZO LINALOKUSUMBUA ILI UWE NA FURAHA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za Maisha Yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na furaha katika maisha yetu ya kila siku.

Hebu tuangalie mfano huu. Mwanamke mmoja alikuwa anahojiwa na mwandishi wa habari kwenye runinga na ghafla aliulizwa swali kama ‘anadhani ni watu gani siku hizi wana furaha’.

Kwa taharuki bila utulivu, mwanamke yule alikurupuka na kujibu lile swali kuwa kila mtu ana matatizo mengi, akimaanisha kuwa hakuna mtu yeyote aliye na furaha.

Hii inaonyesha dhahiri kuwa mwanamke yule kwa muda ule hakutarajiwa kuulizwa swali kama lile. Na aliulizwa bila kupewa nafasi ya kuwa na maandalizi. Na kwa muda huo, alikuwa ni mtu aliyejawa na mawazo.

Lakini ukweli ni kwamba furaha huwa ipo tu, bila kujali kama mtu ana matatizo ama hana. Inawezekana kabisa kila mmoja akawa na matatizo, lakini si kwamba kila moja hana furaha, kwani wapo watu wenye furaha lakini wana maisha duni, lakini wapo wengine hawana furaha ingawa ni matajiri wakubwa.

Tunaona kuwa kuna watu ambao wamejaaliwa kuwa na vitu vyenye thamani ya mabilioni ya fedha, lakini wamekuwa na matatizo ya kifedha. Utajiri wao upo kwenye mali walizowekeza.

Hupokea mshahara, lakini kiasi kikubwa kinakwenda kwenye madeni aliyonayo. Pia katika maisha haya tunayoyaishi kila mtu anakuwa na eneo fulani ambalo limekuwa likimkosesha furaha katika maisha yake. La msingi ni kuikabili hali hiyo na kutafuta ni jinsi gani utapata furaha na amani katika maisha.

Hata wewe inawezekana una hali hiyo katika shughuli zako uzifanyazo. Kama hilo unalikubali, hata kama una fedha nyingi bado kuna eneo utakuwa umekwama hivyo utakuwa huna furaha. Kila mmoja anapoanza maisha anakuwa na ndoto ya mafanikio. Inakubidi ujue ndoto ya shughuli unayotarajia kuifanya na jinsi ya kushikamana nayo.

Endapo ndoto za malengo yako zitatimia, ni lazima utakuwa na mafanikio makubwa. Na hapo ndipo furaha yako itakapotimilika. Pia wengine wana sononeko katika ufahamu wao. Hapa utaona kuwa kila mtu amebahatika kupewa eneo lake alitawale. Kwa maana kwamba, wapo wenye akili za darasani, wenye ushauri wa busara, wenye akili ya biashara na mambo mengine.

Utaona hapa kila mmoja, Mungu amemjalia kwa sehemu yake. Kwa hiyo kila mmoja ana eneo ambalo hakubahatika kuwa nalo. Hebu tuangalie mfano huu. Wanafunzi wawapo darasani, wapo wanaoelewa kwa haraka zaidi somo fulani kuliko wengine. Wengine ni wepesi katika hisabati, wengine histori na wengine Geography. Inategemeana na vile alivyojaliwa.

Hivyo kama mwanafunzi mzuri unapoona somo fulani linakupiga chenga huku wenzako wakiwa wanalielewa kwa urahisi, unaumia na kukosa furaha. Kinachotakiwa ni kutafuta njia ya kutatua hali hiyo ili uwe na furaha katika eneo hilo.

Kwa mfano, kuna kijana aliyekuwa haelewi somo la historia wakati mwalimu wake alipokuwa akifundisha darasani. Hivyo kila mara mwalimu huyo alipoingia darasani alikuwa akikosa furaha.

Wakati huo, wenzake walikuwa wakilifurahia somo hilo kwa kuwa walikuwa wakilielewa vizuri pale mwalimu wao alipowafundisha.

Mwalimu wake aligundua hali hiyo kwamba kijana yule hana furaha kama wanafunzi wengine anapokuwa darasani. Na siku moja alimuuliza, ana tatizo gani ili aweze kumsaidia lakini kijana yule alimweleza kuwa hana tatizo.

Kwanza tunaona kuwa kijana yule alifanya kosa kwa kuwa hakuwa tayari kujieleza ili apate msaada kwa mwalimu wake. Hivyo ni ukweli usiopingika kuwa pale unapokuwa na tatizo na ukawa tayari kujieleza, unakuwa na amani na furaha moyoni, kwa kuwa unapata msaada zaidi. Kinyume cha hapo, unakosa furaha kila mara kipindi hicho kinapokaribia.

Kwa hiyo, tunaona kuwa mafanikio ya mwanafunzi yanapatikana pale anapokubali kuwa hawezi somo fulani, ili apatiwe msaada zaidi. Kwa upande mwingine, mtoto nyumbani anaweza kuwa na hali ya mfadhaiko na kushindwa kuwa na mawasiliano mazuri na wazazi wake, kutokana na jinsi ile wanavyomlea, kwamba wamekuwa wakali sana na hawamfundishi kwa upendo pale anapokosea.

Laiti mtoto yule angeweza kuwa wazi na kuwaambia wazazi wake hali aliyonayo inachangiwa na wao, angeweza kuwa na hali nzuri. Na ukawa mwanzo wa mahusiano mazuri kati yake na wazazi wake.

Vile vile kwa upande mwingine, ni vema wazazi wakawa wazi kwa watoto wao, pale wanapoona kuwa wamewakosea. Wawe tayari kukiri makosa hayo kwa watoto wao. Si vema mzazi akaonyesha kuwa yuko sahihi wakati wote hata kama amekosea. Ni vema kukiri kuwa jambo fulani limefanyika kimakosa.

Eneo jingine linalowanyima watu furaha ni upande wa hisia. Hapa utaona kuwa, watu wengi wamekuwa wakiugua maradhi mbalimbali, kutokana na hisia wanazokuwa nazo.

Wengine hufikia hatua ya kupungua uzito, kutokana na hali hiyo. Wengine kutokana na kupata msukosuko wa kimahusiano hufikia hatua hata ya kutaka kujiua.

Ni kweli kuwa katika maeneo yote ya maisha kanuni zinafanana. Hivyo unapokutana na tatizo ni vema kuikubali hali hiyo iliyokupata japo si jambo rahisi, ili urejeshe furaha yako uliyokuwa nayo. Na kwamba, furaha inapatikana pale tu unapokubali kuwa umepungukiwa hivyo unahitaji msaada.

Kuna swali moja la kujiuliza kwamba, kama kila mmoja kati yetu eneo fulani katika maisha ana uhitaji, kwanini basi tunakuwa wagumu kuikubali hali hiyo? Yawezekana ugumu unakuwepo kwa kuogopa kuwa, unaposema ukweli katika eneo fulani utakataliwa na jamii, rafiki ama familia.

Ama pia kukubali hali ile uliyonayo itakufanya upate aibu. La hasha, hiyo ndiyo njia sahihi ya maisha ya kujikubali na kuachana na mambo yale yanayokuumiza. Kinachotakiwa ni kujivika hali ya ujasiri bila kuogopa jambo lolote lile.

Furaha inakuja kwa mtu yule anayegundua eneo ambalo anahitaji msaada na kuwa wazi. Mafanikio yanakuja kwa mtu anayeomba kusaidia katika eneo lile aliloshindwa.

Tukutane alhamisi ijayo

FEDHA HAZIWEZI KUKUPA FURAHA

KARIBU mpenzi msomaji katika safu hii ya Maisha Yetu, inayokujia kila Alhamisi, lengo likiwa ni kujifunza mambo mbalimbali tunayoyapitia. Leo tutaangalia mambo yanayoweza kukupa furaha katika maisha.

Mara kwa mara waweza kufikiri kuwa kama ungekuwa na gari la aina fulani, nafsi yako ingeweza kufarijika. Kama ungeweza kumpata mtu mtakayeweza kuishi maisha ya ndoa katika raha na shida, ungekuwa na furaha, kama usingekuwa na hali ya msongo kutokana na ukosefu wa fedha, ungekuwa umejitosheleza.

Ni kweli unaweza kuwaza mengi zaidi ya hayo kwamba kama ungeweza kufanya jambo fulani ama kuwa na magari, nyumba, dhahabu na vitu vingine vya thamani, ungeweza kuwa na furaha, lakini hicho pia siyo kipimo halisi cha kuhitimisha furaha yako.

Sasa ni wapi ambako unaweza kuipata furaha, kama si kwenye utajiri, mazoezi, kukubalika ama kwenye mahusiano. Tunaona kuwa, ipo siri kwamba tabia yako ni muhimu kuliko hali halisi. Kinachotakiwa kufanya ni kuondoa mawazo hasi na kuwa na mawazo chanya.

Kuna mfano wa mtu mmoja aliyeona kuwa kama angekuwa na gari zuri la kifahari, furaha yake ingetimia. Kutokana na kupenda kuwa na gari, mara kwa mara alikuwa akiota kuwa na gari hilo.

Mtu huyo kila alipokuwa akijiwazia kama yupo kwenye usukani wa gari, alihisi ananusa harufu nzuri ndani ya gari. Na kwamba alihisi kama yupo barabarani analiendesha gari hilo.

Muda mfupi baadaye, alipandishwa cheo ofisini kwake na kujiona kuwa yale aliyoyatamani ameyapata. Na kwamba ataweza kujitosheleza kwa kile alichokihitaji. Baada ya kupata gari lile alilokuwa akilihitaji, alijikuta tena akitamani kila mwanamke aliyemuona, hali iliyofanya matumizi yake kuongezeka kuliko kipato kile alichokuwa akikipata.

Na kwamba wanawake aliowapenda hawakuwa na upendo wa dhati kwake, ila ni kwa kuwa walimuona anaendesha gari zuri la kifahari, kutarajia kupelekwa katika hoteli nzuri za kifahari, pamoja na kupewa zawadi nzuri za gharama.

Baada ya muda mchache alibaini kuwa, gari hilo badala ya kumpatia furaha, alipata maumivu, kwa sababu pesa yake ilitumika katika mambo ya kifahari zaidi. Taratibu alianza kufikiria gari lake na marafiki wapya aliowapata baada ya kuwa na gari, pamoja na kujiuliza kama kweli wanawake wale walikuwa wakimpenda kwa dhati ama walilipenda gari lake.

Furaha yake kuhusiana na gari lile ikaanza kutoweka, alianza kupata sononeko katika nafsi yake, pamoja na kuona gari lile kwamba ni mzigo. Hali hiyo ikamkatisha tamaa kwa yale aliyoyategemea, kwamba gari ndiyo utimilifu wa furaha katika maisha yake.

Ni vema kukumbuka kuwa vitu vinavyoonekana kwa macho haviwezi kuleta furaha ya kweli. Kwa sababu watu wanaotafuta furaha kwa kutumia fedha, ukuu walionao, utajiri ama mali walizowekeza, ni sawa na kuitafuta furaha hiyo kwa muda tu, na si ya kudumu. Kwa kuwa, siku zote fedha haziwezi kununua furaha.

Kuna mifano ya watu wengi ambao ni matajiri, lakini wamekuwa wakikabiliwa na matatizo mengi. Hawana furaha kama uliyo nayo wewe au mimi. Ni ukweli kwamba, fedha waliyonayo inawapa matatizo mengi na furaha kidogo.

Watu wengi mashuhuri wamekuwa wakiishi maisha ya kukata tamaa, matokeo yake, wengi wao huamua kujiua. Hivyo basi, furaha haipatikani kwenye utajiri, marafiki, kutumia dawa za kulevya ila ni katika kuituliza akili yako.

Tukiangalia katika maandiko matakatifu ndani ya Biblia, ambayo ndugu zetu Wakristo wanaiamini, yanasema kwamba heri wale walio maskini wa roho kwa maana ufalme wa Mungu ni wao, heri wale wenye huzuni kwa kuwa watarehemiwa. Heri wale wenye upole kwa kuwa watairithi nchi. Heri wale wenye njaa na kiu ya haki kwa kuwa watashibishwa. Heri wale wenye mioyo safi kwa kuwa watamuona Mungu. Heri wale wapatanishi kwa kuwa wataitwa wana wa Mungu.

Hivyo basi, neno heri lina maana ya furaha, hivyo bila kujali kama umeshinda ama umeshindwa, umefanikiwa ama hujafanikiwa, una furaha ama unatabika. Kwa hiyo mtu yeyote anayesoma maneno hayo na kuyarudiarudia moyoni mwake, anajikuta ni mwenye furaha wakati wote.


Tukutane Alhamisi ijayo.

Twitter Facebook