Friday, June 27, 2008

EPUKA KUJINYONGA FIKIRIA SULUHU NYINGINE

KUKATA tamaa na kukosa tumaini kunaweza kukuongoza katika kufikiria hali ya kutaka kujinyonga. Lakini kumbuka kuwa una njia mbadala/suluhu nyingine zinazoweza kukusaidia kuepuka mara moja mgogoro huo na zikakusaidia kuibua mpango wa usalama wa muda mrefu.
Kuna wakati inapofikia hatua na kuona kuwa hakuna umuhimu wa kuishi, au matatizo yako yanaonekana kuwa mengi, kutokana na hali hiyo, hivyo unafikia hatua na kuona njia pekee ni kujinyonga.
Unaweza usiamini, lakini unaweza kuwa na njia nyingine itakayokufanya uendelee kuishi na kujisikia vizuri juu ya maisha yako, endapo utakuwa umefikia hatua ya kutaka kujinyonga.
Mara nyingine unaweza kufikiri kuwa umeshajaribu njia zote za kuondokana na hali hiyo ya kutaka kujinyonga, bila mafanikio, na kuona kuwa familia na rafiki zako wanakutenga.
Ni sawa kujisikia vibaya, lakini jaribu kutenganisha hisia zako na vitendo vyako kwa wakati huo. Tambua kuwa hali hiyo ya huzuni uliyonayo au mawazo uliyonayo au hali ya kukata tamaa ya muda mrefu uliyo nayo inaweza ikakugeuza vibaya mwelekeo wako kuondoa uwezo wako wa kufanya maamuzi.
Hisia za kujinyonga ni matokeo ya ugonjwa usiotibika. Kwa hiyo jaribu kuonyesha kuwa kuna uwezekano mwingine, hata kama hujauona kwa sasa.
Inaweza ikawa si rahisi kuondoka katika hali hiyo iliyokupata hata ikakusababisha usijisikie vizuri usiku kucha. Kutokana na hisia hizo ulizonazo za kukata tamaa, unaweza ukapata njia ya kutafuta ufumbuzi mpya kama matibabu na sababu za wewe kuishi.
Jitahidi kila siku uwe na mbinu za kuzuia hali hiyo kwa kuzungumza na daktari, familia au rafiki zako waweze kukusaidia kuondokana na hali hiyo.
Mbinu hizo zitakuwezesha kufanya vitu ambavyo hujisikii kuvifanya, kama kuzungumza na marafiki wakati umekuwa chumbani kwako siku nzima huku umeteremsha mapazia. Au unaweza kwenda hospitali kwa daktari wa akili kwa ajili ya kukufanyia tathmini. Lakini zingatia mbinu hizo, pale unapokuwa umevunjika moyo na kukosa matumaini.
Moja ya mbinu hizo ni kutunza orodha ya majina na namba zinazoweza kupatikana kwa urahisi, zikiwamo za madaktari, familia na ndugu zako ili endapo utakuwa na hali hiyo uweze kuwasiliana nao.
Kama malengo yako ya kujinyonga yanaendana na kunywa vidonge, hii inamaanisha kuwa badala ya kunywa vidonge viwili ulivyoelekezwa wewe unakunywa zaidi ya maelekezo ya daktari. Ni vizuri kutoa maelekezo yako ya dawa ulizonazo kwa yeyote anayeweza kutunza dawa zako na anayeweza kukupa dawa hizo kwa wakati, kuondokana na hali hiyo ya kujizidishia ambayo itakusababisha madhara.
Pia waweza kuondoa nyumbani kwako vitu vyote vya hatari kama visu, risasi, wembe au silaha nyingine zozote mtu anazoweza kuzitumia katika uharibifu wa maisha yako.
Hivyo ni vizuri ukawa na ratiba yako ya kila siku itakayokufanya uwe na shughuli na kukusahaulisha yaliyopita kama kutembea mwendo mfupi, kusikiliza muziki, kuangalia sinema inayovutia, na kutembelea maeneo ya makumbusho.
Baada ya kufanya yote hayo kama hutapata walau furaha kidogo, jaribu kitu kingine tofauti kitakachoondoa maumivu yanayokukabili. Jaribu kuwa pamoja na watu wengine, hata kama hujisikii kuwa nao, ili kuondoa hali ya kujitenga.
Epuka mihadarati na pombe. Zaidi ya kupata hisia za ganzi mwilini, pombe na mihadarati inakuongezea maumivu, unajiingiza zaidi kwenye kujidhuru mwenyewe au kuwa na wakati mwingine kuchanganyikiwa.
Andika kuhusu mawazo na hisia zako. Kumbuka pia kuandika vitu katika maisha yako ambavyo unavithamini na kuvikubali. Haijalishi ni kwa udogo gani unavyoviona.
Unapokuwa katika hali hiyo ya mawazo ya kujinyonga, kabla hujaamua kufanya hivyo, zungumza na mtu yeyote kama vile, kupiga simu kwa rafiki yako au huduma ya simu za dharura.
Kama hutaki kufanya hivyo kutokana na sababu yoyote ile, njia nyingine ni kuwasiliana na daktari wako, kiongozi wa dini au yeyote uliyenaye katika imani yako.
Zungumza na yeyote kuhusu hisia zako, kwani anaweza kukusaidia kukupa nafuu katika mzigo ulionao wa kuvunjika moyo na upweke, hata kama ni msaada wa muda. Itakusaidia kuhamisha mtazamo na kuona kuwa upo uwezekano mwingine zaidi ya kujinyonga.
Pia, zingatia kuweka ratiba maalumu ya shughuli ambayo utajaribu kuifuata wakati unajisikia vibaya. Ufunguo wa tatizo hilo ni kujiingiza kwenye shughuli mbalimbali kama kikwazo cha kuruhusu mawazo mabaya. Pia, uhakikishe kuwa shughuli hizo zinakupatia furaha na kukupa faraja, siyo kukuongezea msongo.
Jaribu kufanya haya ili uweze kujihisi kuwa unapenda kuendelea kuishi. Fanya zaoezi la kupumua pumzi kutoka ndani, piga muziki wa ala, oga kwa maji ya moto, kula chakula kizuri ukipendacho, andika jarida, fanya matembezi, wasiliana na familia, marafiki au wasiri wako unaowaamini.

Monday, June 16, 2008

MBINU ZA MAFANIKIO KWA WAFANYABIASHARA

KATIKA haya mabadiliko ya milenia mpya, wajasiriamali wameweza kujitofautisha na wafanyabiashara wakubwa ili kuwaridhisha wateja wao. Kuwa na ujuzi, ustadi na uwezo wa kupigania kupata bidhaa bora ni njia mahususi ya kufanikisha biashara.
Hivyo basi, mjasiriamali au mfanyabiashara mkubwa anatakiwa kuwa na mipango mizuri na ya kitafiti kufanikisha hili, kwani huo ni ufunguo wa mafanikio.
Mara nyingi mfanyabiasgara lazima awe mbunifu. Hivyo unatakiwa kuwa mfikiriaji mzuri wa kuuza bidhaa unazozivumbua. Ni muhimu kuongeza thamani katika bidhaa ulizo nazo na huduma zako.
Unapokuwa mjasiriamali unatakiwa kuwa na uvumbuzi wa mawazo yanayofanana na biashara yako kwa kuongeza thamani au huduma. Kwa matokeo hayo wateja watagundua ubora wakati watakapoona uhalisia wa bidhaa ulizo nazo.
Unapotaka kuwa mfanyabiashara wa kiwango cha kuthaminiwa inakubidi uwe mtawala mzuri na meneja aliyebobea.
Uwe hodari katika kujifunza na kupata faida ya teknolojia mpya ili iweze kukusaidia kukuza biashara yako katika uchumi mpya. Kukamilisha teknolojia mpya katika biashara yako ni lazima, hivyo utaendelea kukuza na kuifanya iende na wakati.
Uwe mwendelezaji anayelenga kuimarisha mtandao. Kujihusisha na wafanyabiashara wengine ni muhimu sana kwa kuwa itakusaidia katika ukuaji wa biashara yako.
Pia kuwa mwangalifu kuimarisha mawasiliano uliyo nayo kwa wateja wako na kujenga mawasiliano mengine mapya ili uweze kuwa na mazingira ya kiushindani.
Baadhi ya mbinu za kufanya mabadiliko mazuri katika biashara yako ni pamoja na uwazi, mpango wa kibiashara ulio wazi au unaoeleweka na utaalamu. Uwazi unahitajika katika biashara yako, hivyo ni muhimu kutozuia habari zozote muhimu na kuwa mkweli kwa wateja wako.
Kuwa na mpango wa biashara inayoeleweka kunakufanya uweze kuimarisha ubora wa bidhaa na huduma, ili kufikia mahitaji ya wateja wako na kuwaridhisha. Mpango wako wa biashara mara zote uwe unauangalia na kuuimarisha uweze kuelewa mabadiliko na mahitaji ya wateja wako.
Unatakiwa kuimarisha na kutathmini utaalamu ulio nao ili kuweza kufanya kilicho bora zaidi. Usisahau kwamba unahitaji kutoa muda ili kuzingatia eneo lako la utaalamu ulionao.
Kumbuka matangazo na masoko kwa biashara ndogo yanaongeza bidii na mipango ya kukuwezesha kufanikiwa zaidi. Wamiliki wengi wa biashara ndogo ndogo wanavunjwa moyo kwa haraka kwa sababu hawaelewi upepo wa biashara kwa wateja wao wanaowategemea baada ya kufanya kampeni ya matangazo yao ya awali.
Matangazo ni sanaa inayokuwezesha kutazama na kutengeneza mpango wa muda mrefu utakaokuongoza katika mafanikio.
Kuna mambo matatu wamiliki wa biashara ndogo ndogo wanayoweza kufanya katika kuongeza nafasi ya mafanikio katika kampeni ya kutangaza.
Kwanza, unatakiwa kujiaminisha katika mpango wako wa muda mrefu. Kama hukufanya hivyo bilashaka unahitaji mpango mwingine.
Jambo jingine ni kuwa unapokuwa na mipango ya kufungua biashara ni matangazo. Kujitangaza ni njia moja nzuri sana, lakini nayo inahitaji kuwe na hiyo mipango ya kujitangaza. Angalau unatakiwa kuwa na mpango wa kutangaza biashara zako kwa miezi sita, lakini ukweli ni kwamba inatakiwa ujitangaze kwa mwaka mzima. Hii itakusaidia kuimarisha mkataba wa muda mrefu na watangazaji, kwani kwa kufanya hivyo utakuwa unapunguza gharama za uangazaji.
Hii inakusaidia kufikia ukomo uliojiwekea wa uchapaji na kutoa ujumbe mbalimbali unaotaka uwafikie wateja wako katika vipindi mbalimbali vya mwaka.
Na jambo la tatu ni ongezeko la thamani - kama biashara ndogo unashindana na ushirika wa wateja wako. Unatakiwa kuwa tofauti. Zungumza kutokana na kile wateja wako wanachokihitaji na jinsi ya kuwapatia, lakini pia unaweza kuwa sehemu ya wateja.
Inaweza kukuvunja moyo wakati unashindana na biashara ndogo na kubwa endapo hutapata matokeo mazuri ya biashara kutokana na ulivyojitangaza. Ili kuleta utofauti unayo nafasi kubwa ya kupata wateja wote ambao hawakufanyi ukatulia.
Pata faida kwa kutoa huduma za bure – huduma za kawaida ambazo wafanyabiashara wadogo wanashindwa kufaidika nazo ni kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Kama una bidhaa mpya au huduma au kitu chochote kipya katika kiwanda chako ambacho unafikiri kuwa wateja wako wanatakiwa kujua, andika taarifa kwa vyombo vya habari. Pia unaweza kutoa taarifa hiyo kwenye magazeti binafsi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blohdpoy.com0713 3314550733 331455

VYANZO VYA MIGONGANO NA JINSI YA KUVIKABILI

JINSI jamii inavyokuwa na mfumo wa aina fulani kuna uwezekano wa kujenga mizizi inayosababisha mikwaruzano mbalimbali.
Ni vema kuelewa kuwa jamii yoyote ina mfumo wake, hivyo kuwa na baadhi ya watu wanaojikuta hawatendewi haki kama wengine, hali inayochangia kuwapo kwa migongano, mikwaruzo au kutokuelewana.
Hali hiyo hutokea hasa pale kiongozi wa mtaa, wilaya, nchi, eneo, kazi au katika shughuli yoyote inayowashirikisha watu wengi anaposhindwa kuwawakilisha wote kwa usawa.
Kumbuka kuwa kila mwanadamu ana mahitaji muhimu, kwani kila mmoja hupenda kuwa salama na kutambulika. Ikiwa mahitaji yake hayafikii malengo, husababisha maamuzi mabovu kutolewa, amani kutoweka na kutokuelewana.
Tunaweza kuona vyanzo mbalimbali vinavyosababisha migongano katika jamii tunamoishi. Zinaweza kuwa za kisiasa au kijamii. Tunaona kuwa mara nyingi kutokuelewana hutokea pale watu wanapokosa kuelewana katika jambo linalofanana. Endapo kunakosekana usawa katika mojawapo ya mambo, kwa mfano, utofauti wa kipato unaosababisha mifarakano kutokana na rasilimali za nchi kama vile ardhi na maji.
Pia tunaona hali ya kutokuelewana huibuka pale watu wanapokuwa hawana furaha kutokana na watawala wanaowaongoza.
Mara nyingi tumeshuhudia kuwa migongano ya mara kwa mara hutokea wakati kikundi fulani kinapotaka kuwa huru kutokana na utawala uliopo madarakani, madai yao inaposhindwa kuwasilishwa serikalini, serikali inapowadharau na kutowaheshimu au kukutana na mahitaji yao ya muhimu.
Migongano mingine inatokea kuhusu masuala ya dini na siasa. Wakati mwingine husababishwa na kikundi cha dini au siasa kilichohujumiwa. Hata hivyo, migongano yoyote inaibuka wakati watu wanapoumizwa.
Ingawa mara nyingi migongano hiyo huonekana ni kinyume, inaweza kufikiwa muafaka kama utatuzi utapatikana. Pia katika maeneo ya kazi mara nyingi kumekuwa na mifarakano ya mahitaji. Wafanyakazi wanapozidiana katika rasilimali na kutambuliwa kazini, migongano hutokea.
Kwa mfano, utakuta kuwa mkuu wa idara amekuwa akiwapendelea baadhi ya wafanyakazi kwa kuwapa motisha zaidi, hali inayowavunja moyo wafanyakazi wengine na kusababisha migongano.
Pia ufahari au jinsi ya kuishi na watu maeneo ya kazi huleta kutokuelewana kama tu hutajishusha na kuishi maisha ya kawaida katika jamii inayotuzunguka.
Kumbuka kila mtu ana tabia zake binafsi, kunakuwa na tofauti katika kuwafikia watu na matatizo yao. Kama kiongozi jihusishe nao kuelewa mitindo yao ya maisha na jifunze jinsi ya kuepuka migongano inayoweza kusababishwa na hali hiyo.
Kwa mfano, itakapotokea mfanyakazi mmoja anapofanya kazi katika mazingira bora na mazuri wakati mfanyakazi mwingine anafanya kazi katika mazingira yasiyoridhisha, wafanyakazi hao wawili ni rahisi kukorofishana na kutokuelewana, kwa vile mmoja wao ataona kuwa hatendewi haki kwa hilo.
Matatizo mengine huchangiwa pale mtu asipoweza kufikia lengo alilokusudia kutokana na kutowezeshwa na mwajiri wake - kwa upande wa vitendea kazi, hali inayochangia kuchelewa kutekeleza majukumu yake.
Wakati mwingine mwajiri anaweza kukulaumu mara kwa mara kutokana na uzembe wa kampuni hiyo kwa kutoona umuhimu wa kuwa na vitendea kazi vya kutosha, au wakati mwingine idara mojawapo hupewa vitendea kazi na nyingine kukosa. Hiyo huleta hali ya mvutano na kutokuelewana katika maeneo ya kazi.
Shinikizo kutoka kwa viongozi wa kazi huchangia migongano. Kwa kuwa inaweza kutokea watu wawili au zaidi katika kitengo kimoja wanapokuwa na majukumu tofauti yanayotakiwa na bosi wao kwa wakati mmoja.
Kwa mfano, kiongozi wa kazi anapotaka taarifa kamili ikamilike saa tisa alasiri - muda anaotakiwa mfanyakazi mwingine kukamilisha taarifa yake - ambapo wote kwa pamoja wanahitaji kutumia mashine moja kwa kuwa mashine nyingine ni mbovu, kipi ni suluhu? Matokeo yake mgongano unatokea.
Migongano mingine husababishwa na hali ya upendeleo kwa baadhi ya wafanyakazi. Utakuta bosi bila uficho wowote anaonyesha hali ya kuwathamini baadhi ya wafanyakazi na kuwadharau wengine.
Ubaguzi katika maeneo ya kazi unasababisha minong’ono, tuhuma, na hatimaye migongano. Hivyo ili kuondoa hali hiyo, kiongozi mkuu wa kampuni anatakiwa kuwa thabiti katika kuhakikisha kampuni yake haiwi na mgawanyiko wowote na kuwafanya wafanyakazi wake wafanye kazi zao kama timu moja imara.
Mingine husababishwa na sera mpya ambazo hazikutarajiwa.
Popote sera za kampuni zinapobadilika, kutokuelewana kunatokea, wafanyakazi wanahitaji kufahamishwa sheria na sera za kampuni, pale mabadiliko mapya yanapotokea hawatakiwi kubahatisha. Vinginevyo vitu visivyotarajiwa vitatokea kama kupeana taarifa potofu.
Njia mbalimbali zinazoweza kumsaidia mkurugenzi wa kampuni, mkuu wa idara au yeyote mwenye dhamana ya kuwaongoza wenzake, jinsi ya kutatua migogoro katika maeneo ya kazi.
Ni vizuri ukatambua kuwa baadhi ya migogoro hatima yake hujenga mahusiano bora zaidi tofauti na ilivyokuwa mwanzo endapo itatatuliwa kwa umakini.
Ukumbuke kuwa migongano katika sehemu za kazi ni sehemu ya maisha na haiepukiki, lakini ni jinsi gani tunaishughulikia inapotokea kama bosi bila kuathiri biashara na shughuli za uzalishaji katika kampuni yako. Kama viongozi kunakuwepo na majukumu imara ya kusuluhisha migogoro kwa haraka.
Viongozi wa kisasa hawaatakiwi kuwa ‘wanyapara’, bali wawe viongozi wanaodhihirisha fani zao, heshima na usawa katika mazingira yoyote na zaidi wanaposhughulikia migongano.
Kwanza yampasa kiongozi atathmini chanzo cha tatizo. Mafanikio ya kutatua tatizo la kutokuelewana kwa kikundi au jamii yanatokana na kuelewa chanzo halisi cha mgongano huo. Ni muhimu sana kuangalia mgogoro kutokana na mtazamo wa kila mmoja unaomhusu.
Kutokuelewa chanzo cha tatizo kutafanya utatuaji wa tatizo hilo kuchukua muda mrefu kutambua aliyehusika na sababu za kuhusika kwake, na sababu zinazofanya tatizo hilo kuwa gumu. Kutegemeana na hali ya tatizo lilivyo, unaweza kuzungumza ‘chemba’ na kila mmoja aliyehusika katika mgongano huo au unaweza kuzungumza nao wote kama kikundi. Kusikiliza ni silaha mojawapo muhimu itakayoweza kukusaidia na kulielewa tatizo.
Pia katika utatuaji wa tatizo unatakiwa kuwa makini na kujua kwa undani chanzo. Kuwa mkweli katika kulishughulikia tatizo. Sikiliza kwa umakini kukuwezesha kutoa mawazo yasiyopendelea upande wowote na kukuwezesha kutatua tatizo. Mruhusu kila mmoja kuwa mhusika katika hatua hizo na hakikisha uko wazi, mkweli na kutenda kwa usawa kama unavyozungumza na mtu binafsi. Usihukumu.
Ainisha njia bora zaidi ya kutatua matatizoMara unapokuwa na vielelezo vya uhakika mbele yako ni kazi yako kuongoza kikundi katika kufikia suluhu au kuainisha njia bora ya utatuzi. Mafanikio ya utatuzi wa matatizo mbalimbali mara zote inahusisha pande zote katika kutathmini tatizo na kipindi cha kutafuta utatuzi.
Muulize mtu binafsi kama anaweza kutoa mawazo ya jinsi ya kutatua tatizo. Unaweza kushangaa ni jinsi watu mara nyingi wanavyokuwa kamini kufikia mwafaka wa tatizo na kuwa na maamuzi yao binafsi.
Kama hawatakuwa na uwezo wa kufanya hivyo, unaweza kutumia njia bora ya kutatua tatizo. Malengo yako ni kuhakikisha unapatikana mwafaka wa usawa na utatuzi wa tatizo lililokuwepo ambalo litaleta utatuzi thabiti katika kampuni yako au kwa mtu binafsi.
Suluhisho
Wakati mwingine linapotokea tatizo, chukua muda na kujiuliza maswali yafuatayo:Nini kinachosababisha migongano katika kampuni yako? Kwa nini wewe au mwingine anahitaji vitendea kazi? Je, mtindo wa mfanyakazi fulani ni tofauti na mtindo wako uliouzowea?
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733331455Mwisho

TABIA 10 ZA KUEPUKA KUHUSU PESA

“YEYOTE anayepata kipato na kujihudumia mwenyewe anapaswa kuwa na bima ya ulemavu,” aliwahi kusema mwanasaiokolojia mmoja wa nchini Marekani aitwaye Simon.
Baraza la Usalama la Taifa nchini Marekani liliarifu kuwa zaidi ya watu milioni 20 walikumbwa na majeraha yaliyowasababishia ulemevu kwa mwaka 2002 pekee.
Hili laweza lisiwe jambo la kawaida hapa kwetu lakini kitu tunachoweza kujifunza ni kwamba tunapaswa kuwa na utaratibu wa kujikatia bima.
Hebu fikiri jambo ambalo linakufanya uwe nje ya kazi kwa siku kadhaa au miezi kadhaa litakugharimu kiasi gani na ni iwapo utapata pesa hizo na itakuwaje utakaporejea katika shughuli zako za kawaida?
Ni wazi kuwa utajikuta umebakia nyuma kwa kiasi fulani lakini kama utakuwa na bima ya ulemavu basi shirika la bima linge gharamia matibabu na ungelipwa malipo ya ulemavu.
Msomaji wa safu hii huu ni ulimwengu wa sayansi na maendeleo na unaweza kujiunga na bima bila ya usumbufu wowote na pasipo kuchukua muda mrefu.
Ni rahisi kufanya hivyo iwapo mwajiri wako hayuko tayari kufanya hivyo waweza kuangalia mfukoni kuwa ni kiasi gani ulichonacho na ukawasiliana na kampuni au mashirika ya bima na kujiunga. Kumbuka kuwa unapojiunga na bima ni vyema ukapata sera za aina ya bima unayotaka kujiunga nayo na zisome vyema na ikiwezekana pata maelekezo kwa mtaalamu kabla ya kuamua kujiunga rasmi na aina hiyo ya bima.
Kutotambua ongezeko dogo la matumizi
Matumizi madogo ya pesa, kama ilivyo kwa uvujaji mdogo katika chombo, yanaweza kumaliza pesa ulizonazo katika pochi yako.
Njia ya kuepuka hilo ni kutambua wastani wa matumizi yako kwa siku, wiki au mwezi na iwapo kuna ongezeko basi tambua ni kiasi gani, na iwapo litaweza kuathiri matumizi yako au la.
Baada ya hapo sasa unaweza kuamua kufanya matumizi hayo au kuaachana nayo au kubadilisha na matumizi mengine. Yapo matumizi kama vocha za muda wa maongezi ya simu, safari zisizo za lazima au idadi ya vinywaji ni baadhi ya vitu ambavyo huongeza matumizi japo kwa sehemu ndogo lakini huwa na mabadiliko makubwa katika hali ya fedha ya mhusika.
“Jaribu kuangalia kumbukumbu zako na angalia pesa ulizonazo na madeni unayodaiwa yanatokana na nini? Utaratibu wa aina hii utakupa hali halisi katika matumizi yako ya pesa na utang’amua athari za ongezeko dogo tu la matumizi,” alisema Berkeley Calif, wa Marekani.
Njia muhimu ya kukwepa hilo ni kujiuliza kuwa je, matumizi yaliyoongezeka yana umuhimu wowote?
Kungojea malipo ya pensheni ili kuwekeza
Hili ni moja ya makosa makubwa yanayofanywa na watu wengi. Wafanyakazi wengi wanashindwa kuwekeza wakati wakiwa kazini na hivyo kusubiri hadi walipwe malipo ya kustaafu. Hali hii inawafanya wengi kujikuta wakistaafu huku hawana kitu na hivyo kutumia malipo ya kustaafu katika kutekeleza mahitaji yao na hivyo kukuta pesa hiyo ikimalizika bila ya kufanya jambo la msingi lililokusudiwa ambalo ni kumtunza mstaafu hadi anakufa.
Wengi tunaweza kufikiri kuwa ni jambo lisilowezekana lakini kumbuka kuwa ili uwekeze ni lazima ujinyime na unaweza kufanya hivyo kwa kutenga asilimia ndogo tu kutoka katika mapato yako au kwa wale ambao si wafanyakazi wa ofisini wanaweza kuweka utaratibu wa kuchangiana na wenzake kwa mzunguko na inapofika zamu yake anaweza kuwa na utaratibu wa kuweka pesa benki hadi atakapoona imefikia kiwango cha kufungua mradi fulani anaweza kufanya hivyo.
Ni rahisi kuanza, angalia mfumo wa mapato yako na jiulize kuwa unaweza kuanza na kiasi gani na uamue kuanza kwa ujasiri.
Kusubiri hadi dakika ya mwisho ndipo ukusanye pamoja mtajiWatu wengi huwa na kawaida ya kutaka wapate mtaji wote wa kuwekeza kwa wakati mmoja. Si ajabu kusikia mtu akisema ifikapo Mei nitafanya jambo fulani, au mshahara wa mwezi ujao nitafanyia jmbo fulani.
Kwa utaratibu huo ndugu msomaji utajikuta ukibakia kupanga kuwa nitafanya jambo fulani ifikapo mwezi au siku fulani na siku hiyo haitafika kamwe.
Nilipanga kuwa mwezi huu nitanunua viatu vya watoto wa shule lakini imetokea dharura…” alisikika mama mmoja akisema.
Mama huyu ambaye ni mfanyakazi wa kipato cha mwisho wa mwezi alishindwa kuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba kila anapopokea mshahara wake na akafikiri kuwa anaweza kutenga mshahara wake wote kununulia viatu vya watoto lakini dharura ikamkwamisha. Iwapo mama huyo angekuwa na utaratibu wa kujiwekea akiba, dharura isingeingilia mambo yake.
Kulipa kila mtu na kuweka akiba kilichobakiaKamwe usije ukasema kuwa nitaweka akiba kwa kile kitakachobaki. Iwapo utakuwa na mazoea hayo, basi ni wazi kuwa malengo yako ya kujiwekea akiba yanaweza yakashindwa.
Kuweka akiba ni moja ya matumizi muhimu hivyo hakikisha kuwa unalipa kipaumbele miongoni mwa matumizi yako muhimu.
Amua kuwa asilimia 5 au 10 ya kipato changu ni kwa ajili ya kuweka akiba na hakikisha kuwa una nidhamu wakati wa kutekeleza hilo. Usithubutu kulipa madeni yote na kusema kuwa kitakachosalia ndicho nitakachoweka akiba la badala yake waweza ukaamua kulipa sehemu ya madeni na sehemu iliyosalia unaweza kuonana na wadai wako na ukawaomba ulipe wakati mwingine lakini kuweka akiba ni jambo lisiloweza kuahirishwa kamwe iwapo unataka kufanikiwa katika malengo yako.
Iwapo utakuwa na mazoea ya kulipa madeni na kufanya matumizi mengine huku ukisubiri kinachosalia ili kuweka akiba unaweza kujikuta unastaafu kazi bila ya kubakiwa na kiasi cha kuweka akiba. Kumbuka kesho nzuri huanza leo, hivyo kuweka akiba yenye manufaa kunatakiwa kuanza leo, hivyo msomaji wa safu hii panga na uanze leo kujiwekea akiba.
Kushindwa kusimamia vitega uchumi vyako
Hili ni jambo linalowakabili watu wengi na kufanya waishi katika maisha ya kushindwa kila siku.
Ni vyema kutambua kuwa kuweka akiba ya pesa ni jambo moja na kuwekeza pesa hiyo ni jambo jingine. Kuwekeza ni namna ya kufanya pesa uliyojiwekea akiba iweze kuzalisha faida.
Njia nzuri ya kufanya hivyo ni kuwekeza katika miradi mbalimbali, sababu ya kufanya hivyo ni kuogopa kuwekeza katika mradi mmoja ambao unaweza kufa na kukufilisi kabisa. Kumbuka ule msemo wa kwamba ‘usiweke mayai yote katika kikapu kimoja kwani kikianguka yote yanaweza kupasuka’.
Wekeza katika maeneo tofauti au kiasi fulani cha fedha ulizojiwekea akiba. Hii itakusaidia kutambua iwapo mradi uliowekeza unaendelea vyema au la, kama unaendelea vyema unaweza kuongeza mtaji zaidi na iwapo mradi haufanyi vyema unaweza kuachana nao na ukafikiria kufungua mradi mwingine. Dhana ya kuwekeza katika maeneo tofauti inalenga kuhakikisha kuwa mtaji wako wote haupotei.
Kuhakikisha uwiano na kumudu vyema vitega uchumi vyako kunaweza kukusaidia kutambua ni wakati gani biashara ni nzuri na ni wakati gani si nzuri. Hili laweza kuonekana jambo dogo lakini ni muhimu sana na halikwepeki, iwe kwa wafanyabiashara wadogo au wakubwa. Wachumi wanasema kuwa uwekezaji katika maeneo tofauti tofauti huleta faida kubwa ikilinganishwa na uwekezaji wa eneo moja kwa wakati mmoja. Kwa mfano, utafiti uliofanywa na taasisi ya biashara ya taifa nchini Marekani mwaka 2005 ulionyesha kuwa watu waliowekeza katika eneo moja waliweza kupata faida ya asilimia 2.5 kwa mwaka ikilinganishwa na 6 kwa wale waliowekeza katika maeneo zaidi ya mawali kwa wakati mmoja.
Angalia mfano huu waweza kuwa wa kufurahisha laikini una mafunzo ndani yake.
Kwanini unakuwa na samani nyingi ndani ya nyumba? Kwanini uwe na kiti na kochi wakati vyote vinatoa huduma moja tu ya kukalia?
Ni rahisi kuwa vinashirikiana kutoa huduma hiyo na hivyo kumpa faida zaidi mtumiaji. Tambua malengo yako na ona jinsi ya kutekeleza malengo hayo kisha jitoe kikamilifu katika kutekeleza malengo yako.
Kutawaliwa na hisia katika vitega uchumi
Yapo makosa makubwa mawili hapa: watu kuwa na mapenzi mazito dhidi ya vitegea uchumi vyao na kujikuta wakati wowote wakielekeza au kujitoa kwa ajili ya vitega uchumi kuliko kawaida au, wakati vitega uchumi vinapoanza kwenda mrama au kombo hutaka kuachana na mambo mengine na kuhangaika navyo hadi vitakaporejea katika hali ya kawaida. “ Hili ni kosa kubwa japo wengi wanaweza kudhani kuwa ni jambo jema na la muhimu,” anasema mwanasaikolojia wa nchini Uingereza Simon.
Hii ni hatari kwani inaweza kukuletea athari ambazo zinaweza kukufanya ushindwe kufanya mambo mengine ya maisha. Simon anasema kuwa katika utafiti alioufanya kati ya mwaka 2000 na 2002 aligundua kuwa watu waliokuwa na mapenzi makubwa na vitega uchumi vyao walipata hasara ya asilimia 30 na 50 baada ya mambo kwenda kinyume na walivyotarajia. Sababu kubwa ilikuwa ni kwamba walikuwa na mapenzi makubwa mno na miradi yao na wakajikuta wakiacha kufanya mambo mengine na kusikitikia miradi yao kuwa haiendi vyema na hatimaye wakajikuta wakipata hasara katika maeneo mengine.
Nini cha kufanya ili kuepukena na hili? Fanya jambo rahisi kiasi hiki, tambua ni wakati gani biashara fulani inakuwa na soko zuri na ni wakati gani hali ya soko si nzuri.
Jambo jingine ni kuhakikisha kuwa unawekeza katika maeneo tofauti na hapa ni kazi au biashara na usije ukawekeza katika mapenzi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.comwww.ngowil.blogspot.com0713 3314550733 331455

MAKOSA 10 YA KUACHANA NAYO KATIKA MATUMIZI YA PESA

SI jambo la ajabu kumsikia mtu akisema fulani ana matumizi mabaya ya pesa au yule akipata pesa zinamtawala.
Hata hivyo, tunashindwa kutambua kuwa hiyo si njia ya kumsaidia mtu wa aina hiyo kwani hawezi kubadilika.
Mtu huyo tunamuona mfujaji wa pesa kutokana na ukweli kuwa hajui jinsi ya kushughulikia tatizo alilonalo.
Ni vema ukatambua kuwa, kamwe huwezi kubadilisha mwenendo wako kuhusu hali ya kifedha, isipokuwa unaweza kushughulikia baadhi ya matatizo.
Hii inahusu tabia ya kufanya au kutofanya mambo fulani. Tabia zetu nyingi kuhusu pesa huundwa bila ya sisi kujitambua au kutojali katika kipindi kirefu.
Hakuna hata mmoja wetu ambaye hukaa chini na baada ya kufikiri kwa muda mrefu, akatoka na jibu kwamba, kuwa na uwiano katika kitabu cha hundi ni jambo la kijinga. Badala yake tabia huibuka yenyewe baada ya muda mrefu.
Tabia yetu kuhusu pesa husababishwa na namna tunavyotunza pesa, tunavyotumia, tunavyothamini na tunavyofikiri kuhusu mustakabali wetu. Hivyo kile tutakachojifunza kuhusu pesa, kinaweza kufanya tuwe na mwenendo mzuri au mbaya wa pesa zetu.
Ni vema ukakumbuka kuwa, unapogundua juu ya jambo fulani ambalo limekosa mwenendo mzuri, basi utafute namna ya kuachana nalo.
Acha kurudia makosa yale yale kila mwaka na ujiulize ni kwa nini huweki akiba kutokana na kipato chako? Njia pekee ya kuepekuna na tabia hiyo ni kufuta mfululizo wa makosa hayo yenye tabia ya kujirudia na udhamirie kubadili maisha yako.
Baadhi ya watu huishi huku wakiendelea kurudia makosa katika sekta ya kiuchumi. Bila shaka hutakiwi kuwa mmoja wa watu wa aina hiyo.
Ili uepukane na mkosaji anayerudia kosa, unapaswa kuhakikisha kuwa hufanyi kosa lolote miongoni mwa makosa haya kumi ambayo wengi wetu huyafanya kuhusu pesa.
Hata hivyo unapaswa kuhakikisha kuwa unaitambua vyema hali halisi ya gharama duniani, huku ukichagua njia muafaka ya kukabiliana na kila hali.
1. Kutumia pesa bila ya bajeti
Mara nyingi watu hufikiri juu ya mipango mbalimbali ya kuwaingizia fedha, mfano wapo wanaofikiri ni jinsi gani watawekeza ili kuifanya pesa hiyo iongezeke, lakini ni wachache sana ambao hufikiri juu ya kuandaa bajeti, hasa kwa kuzingatia uwezo wao kifedha.
Mshauri mmoja wa masuala ya kifedha kutoka nchini Marekani, John Ritter, aliwahi kusema iwapo una kipato na Ankara, unahitaji pia kuwa na bajeti.
“Mara nyingi kuna kikubwa kinachotoka kuliko kipato,” anasema.
Je, kutumia pesa bila bajeti kunaweza kukugharimu nini? Wengi wetu wanaweza wasikubaliane na hili kwa kuamua kutokubaliana nalo, au wamekuwa wakisumbuka bila ya kuelewa kinachowasumbua.
Jambo hili si jingine, isipokuwa kukosa utulivu wa akili na mawazo kuhusu pesa pamoja na uwezo wa kuandaa bajeti ya muda mrefu.
Mwisho wa hali kama hii ni kushindwa kuwa sahihi juu ya kile ulichotumia kuwa ni asilimia 15 au 20 au zaidi katika chakula au afya.
Namna ya kuepukana na athari hiyo, hakikisha unaweka utaratibu wa kutambua kila aina ya matumizi unayoyafanya ili kung’amua ni wapi pesa zako zinakwenda.
Njia nzuri ya kumudu jambo hilo ni kuhakikisha unaorodhesha mahitaji yote ambayo hayalipwi kwa utaratibu wa ankara, mfano vinywaji, burudani mbalimbali, kuchangia sherehe miongoni na mengine mengi.
Baada ya kufanya hivyo hakikisha unatenga kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya dharura, mfano matengenezo ya gari iwapo umebarikiwa kuwa nalo, au hata pesa ambayo itakuwezesha kusafiri kwenda kuona mgonjwa au kuhudhuria msiba.
Watu wengi hudharau mahitaji ya aina hii na kuyaweka kando ya bajeti kwa sababu hayana umuhimu kwao.
Hata hivyo, mara yanapotokea, umuhimu wake huonekana na hapo ndio hutambua kuwa kumbe katika wakati wote kuna matumizi.
2. Kutembea na kadi inayoruhusu ukope
Hili ni tatizo kubwa kwa nchi za wenzetu walioendelea, na wengi hifikiri kuwa hiyo ni sehemu ya ustaarabu na maendeleo.
Kutembea na kadi inayoruhusu ukope, ni hatari kwani inakufanya kuwa na tamaa ya kupata mahitaji. Sharti la ukopaji wa aina hii ni kukatwa riba kubwa ikilinganishwa na mtu anayenunua moja kwa moja.
Hapa kwetu kuna taasisi na mashirika yanayotoa huduma na vitu kwa njia ya mkopo, lakini iwapo utachunguza vema, utagundua kuwa muda ambao unakaa na deni unakugharimu zaidi, kwani utalazimika kulipa kwa asilimia kadhaa zaidi ya yule aliyenunua kwa kulipia moja kwa moja.
“Mara nyingi watu wanaotaka kulipia huduma au kitu kidogo kidogo hawawezi kufanya chochote na badala yake wanapata hasara kubwa,” anasema John Ritter.
Kwa ujumla kadi za aina hii ni njia mojawapo ya kukufanya uwe mtumwa wa mahitaji yako au madeni.
Ushauri ambao ningependa kukupatia hapa ni kwamba, hakikisha unafanya malipo yanayotakiwa kwa wakati na usikubali kubaki na deni lisilo la lazima.
Baada ya hapo, hatua inayofuata ni kuhakikisha kuwa unadhamiria kwa hali na mali, hata ikiwezekana kwa kujinyima, ili uweze kulipa na kuachana na madeni hayo kabisa, ukianza na moja na baada ya jingine.
Tambua kuwa siku zote deni kubwa ni gumu kulimaliza, lakini hiyo isikukatishe tamaa na badala yake ione kuwa changamoto kwako. Iwapo ulifurahia matunda ya deni hilo, basi uwe tayari kubeba mzigo wake.
Kwa ujumla njia rahisi ya kuepukana na madeni, ni kuhakikisha kuwa unalipia mahitaji yako yote kwa ukamilifu, kila ifikapo mwisho wa mwezi.
Iwapo utahitajika kutumia kadi inayokuruhusu kukopa wakati una dharura, basi hakikisha kuwa unakopa kiasi cha kutosha kukidhi dhahruara hiyo tu (mfano, ugonjwa, ajali au safari).
Baada ya kufanya matumizi hayo, hakikisha kuwa hutumii kadi hiyo hadi utakapokamilisha malipo ya deni hilo.
3. Kudharau riba zitolewazo na benki
Bila ya kujali kiwango cha riba kinachotolewa katika masoko ya hisa, mabenki au kuwekeza katika taasisi zinazotoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni jambo la muhimu kuweka pesa katika taasisi zinatoa riba.
Unaweza kujenga utaratibu wa kununua hisa katika makampuni, mashirika au hata taasisi za fedha. Jambo la kuzingatia, ni kwamba, hii ni njia ya kuzalisha pesa ambazo huzitumii kwa sababu siku utakapoamua kuuza hisa hizo au kuhitaji pesa zako, hazitarejea kama zilivyokuwa, zitaongezeka.
Ipo faida ya kuwa mwanachama unayechangia katika taasisi zinazotoa mikopo, kwani hupata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo.
Mfano, mwanachama anayekopa kutoka taasisi ambayo hutoa mikopo kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, ni wazi kuwa atapata unafuu wakati wa kurejesha mkopo huo kuliko mtu anayekopa wakati si mwanachama, kwani riba ya urejeshaji wa mkopo wake itakuwa ya juu zaidi.
Kwa leo tuishie hapa, juma lijalo tutaendelea na makosa yaliyosalia.

Twitter Facebook