Monday, June 16, 2008

YATAMBUE MAGONJWA YA MSONGO WA MAWAZO

KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika siku nyingine ya leo. Tumekuwa tukiangalia maana ya msongo na vyanzo vyake. Leo tutaendelea kuangalia vyanzo zaidi kuhusu msongo unaowapata watoto na dalili zake.
Vyanzo vingine ni magonjwa, wafanyakazi wengi katika eneo la kazi, mawasiliano hafifu kati ya timu, kutotoa taarifa juu ya utendaji, thamani na mchango, mabadiliko ya kiteknolojia, ukosefu wa uwazi wa majukumu na wajibu, kutoridhishwa na mafanikio ya kifedha, kuchoshwa na kazi zisizo na mvuto, tukio lisilofurahisha, mazingira ya kazi yasiyovutia na ukosefu wa ujuzi.
Inakubidi kuangalia hali yako ya msongo uliyonayo ili uweze kuikabili, na uwasaidie wengine kupunguza hali hiyo.
Kwa upande wa watoto, kama walinzi na waangalizi, watu wazima wamekuwa na tabia ya kuwaangalia watoto kwa ukaribu ili wawe na furaha na bila kuwa na mawazo. Vile vile tunaona kuwa watoto hawana majukumu makubwa ambayo yatawafanya wawe na msongo kama ilivyo kwa wazazi wao. Kwa hiyo hawana kitu cha kuwafanya wawe na wasiwasi.
Hata hivyo watoto wanakuwa na hofu na kuwa na mawazo kwa kiwango fulani. Mawazo yanakuwapo kutokana na mahitaji tuliyonayo pamoja na majukumu ambayo inabidi kuyafikia.
Hebu tuangalie vyanzo mbalimbali vya mawazo kwa watoto. Mara nyingi shinikizo linakuja kutokana na misongo ya nje kama familia, marafiki au shule, lakini inaweza kuwapata kutoka ndani. Shinikizo linalokuwepo kwetu linaweza kuwa na faida kwa sababu mara kwa mara linakuwa na tofauti kati ya kile tunachofikiri tunapaswa kukifanya na kile kitu halisi tunachokifanya katika maisha yetu.
Msongo wa mawazo unaweza kumwathiri mtu yeyote hata mtoto anayehisi kulemewa. Mtoto wa miaka miwili, kwa mfano, anaweza kuwa na wasiwasi kwa sababu mtu yeyote anahitaji kujisikia vizuri - mzazi asipokuwa karibu naye na kumridhisha. Kwa watoto ambao hawajaanza shule hali ya kutengwa na wazazi ni sababu kubwa ya wasiwasi.
Pale watoto wanapokuwa na mawazo mengi kuhusu masomo yao au matatizo mengine ya kijamii huwasababishia kuwa na msongo wa mawazo. Kwa kuongezea, wazazi wakati mwingine pasipo kujua wanaongeza mawazo katika maisha ya watoto wao. Kwa mfano, matarajio makubwa ya wazazi mara nyingi ni matazamio makubwa kwa watoto wao, na yanapokuja kinyume husababisha msongo wa mawazo kwa watoto wao. Wazazi wengi huwashinikiza, kwa njia mbalimbali, watoto wao kufanya vizuri au kuwaandikisha watoto wao katika vitu vingi vinavyoweza kusababisha mawazo yasiyokuwa ya lazima bila ya wao (wazazi) kushirikiana nao. Hii wakati mwingine kuwakatisha tamaa watoto hao na hivyo kuwa na msongo wa mawazo.
Wataalam wengi wanahisi kuwa asilimia kubwa ya watoto wanajishughulisha zaidi, hivyo wanakosa muda wa kucheza kutokana na vipaji vyao au kupumzika baada ya masomo. Watoto hulalamikia juu ya shughuli nyingi wanazojishughulisha nazo au wakati mwingine wanakataa kufanya shughuli walizopangiwa na wazazi wao wanaokuwa wana mambo mengi na kujikuta katika hali ya msongo.
Ni jambo jema mzazi kuzungumza na mtoto wake kuhusu (motto) anavyojisikia baada ya shughuli za kimasomo. Kama mtoto atalalamika, zungumza naye juu ya kumpunguzia baadhi ya shughuli. Zungumza na mtoto wako njia utakazoweza kumsaidia mtoto wako kupangilia muda wake na majukumu yake, hali itakayomfanya asiwe na wasiwasi.
Kama mtoto wako atakuwa anasikia ukiongelea matatizo ya kazini kwako, wasiwasi juu ya ndugu yako aliye mgonjwa, au matatizo ya kiuchumi unayokabiliana nayo, inamfanya naye awe na wasiwasi. Wazazi wanatakiwa kuwa makini wanapojadili mambo kama hayo wakati watoto wao wako karibu nao kwa sababu huyachukua maongezi hayo kutoka kwa wazazi wao na kuanza kuwa katika hali ya wasiwasi.
Tukio la Septemba 11, 2001 na mabadiliko katika dunia yetu tangu siku hiyo yamechangia kuongeza wasiwasi kwa watoto wengi na kwa wale wote walioathirika na tukio hilo. Watoto wanaoangalia marudio ya michezo ya matukio mbalimbali ya kutisha katika runinga au kusikia habari za kuanguka kwa ndege, vita, na ugaidi unaleta wasiwasi kuhusu usalama wao na kwa watu wanaowapenda.
Zungumza na mtoto wako kuhusu kile anachokiona au kusikia na kufuatilia kile anachokiangalia katika runinga, hivyo utaweza kumsaidia mtoto wako kuelewa kinachoendelea na kumwondoa hofu.
Pia, angalia sababu za kutatanisha kama ugonjwa, kifo kwa umpendaye au talaka, inaweza kusababisha msongo wa mawazo kwa mtoto wako. Wakati sababu hizi zinachanganyika na kusababisha shinikizo katika sura ya watoto, mawazo yanakua. Ingawa kunakuwapo na maridhiano kwa wazazi katika kupeana talaka, inakuwa ni jambo zito kwa watoto kwa sababu ulinzi wao muhimu unabadilika. Kutengana au kuachana kwa wazazi kamwe hakutawaweka watoto katika hali ya kuchagua upande wautakao au kuwaeleza ubaya wa mzazi mmojawapo, ambaye amesababisha kuwepo kwa hali hiyo.
Magonjwa ya msongo wa mawazo Si rahisi mara zote kugundua mtoto wako amepatwa na msongo. Ila utagundua kwa muda mfupi tabia yake imebadilika, mwonekano wake unabadilika, vitendo vyake au kutokwa na jasho jingi anapokuwa amelala. Hizi ni dalili za kuwa na mawazo. Baadhi ya watoto wanakumbana na mabadiliko ya kimaumbile ikiwa ni pamoja na kuumwa na tumbo na kichwa. Wengine wanataabika katika kumaliza kazi za shule wanazokuwa nazo. Wengine wanakuwa wapweke au wanakaa wenyewe kwa muda mrefu.
Watoto wamekuwa wakionyesha dalili za kuwa na mawazo kwa kuwa na tabia mpya kama kunyonya kidole, kuzungushazungusha nywele, au kugusagusa pua. Watoto wakubwa kidogo wanaanza kudanganya, kuona ufahari au kutokutii. Mtoto mwenye msongo huwa analala kwa kushtukashtuka, anakuwa mgumu kuachana na mtu anayeonyesha hisia zake katika matatizo madogo madogo na kubadilika kimasomo.
Kupunguza mawazo ya mtoto wako
Unaweza kumsaidiaje mtoto wako kuondokana na msongo? Kwa kuwa na muda mzuri wa kupumzika na kumpa lishe bora, itamsaidia kumwongezea mtoto wako uwezo. Kuwa na muda wa kuzungumza na mtoto wako kila siku. Kama atahitaji kuongea na wewe au kuwa na wewe katika chumba kimoja, kuwa na muda wa kumsikiliza. Hata pale mtoto wako atakapokuwa mkubwa muda huo wa faragha naye ni wa muhimu.
Ni vigumu kwa baadhi ya watu wanaporudi nyumbani baada ya kazi, kukaa chini na kucheza n watoto wao au kuongea nao kuhusu siku hiyo, zaidi sana kama wamepatwa na jambo lililowasababishia mawazo katika siku hiyo. Lakini unapoonyesha hali ya kujali katika maisha ya mtoto wako, unaonyesha jinsi alivyo wa muhimu kwako.
lcyngowi@yahoo.com0713 331455/0733 331455

ELEWA MSONGO WA MAWAZO

Si vibaya nikianza kumshukuru Mungu kwa kunifikisha siku na wakati kama huu. Naamini hata wewe msomaji wangu una kila sababu ya kumshukuru Muumba wetu, kwa kukumbushia tu, leo tunaendelea na mada yetu ambayo ilianza wiki iliyopita inayozungumzia msongo wa mawazo ambao humpata mtu kutokana na mambo mbali mbali anayokumbana nayo katika maisha. Tutaangalia maana, dalili, vitu vinavyosababisha, matokeo na jinsi ya kutatua hali hiyo, endelea.
WOTE tunakabiliana na changamoto na vikwazo mbalimbali, hata wakati mwingine tatizo linakuwa kubwa kukabiliana nalo. Inafikia mahali tunajihisi kuzidiwa, au kuwa chini ya mtutu wa bunduki, au kutokuwa na uhakika wa jinsi tutakavyotimiza mahitaji ambayo yako juu yetu, hapo huwa tunakuwa na msongo.
Iwapo utakuwa katika kiwango kidogo, msongo unaweza kuwa kitu kizuri. Msongo unaweza kukupa msukumo wa kile unachokihitaji, unaweza kukupa motisha wa kufanya vizuri zaidi na kuwa mtu mwenye malengo siku zote.
Msongo unaweza kukufanya uwe makini kwa mfano kama unasoma, unaweza kukufanya uwe makini na masomo wakati wa likizo badala ya kukaa ukiangalia Tv. Lakini mambo yanapokuwa magumu na mahitaji ya maisha yakazidi uwezo wako wa kuyatimiza, hapo ndipo msongo huwa tishio kwako kimwili na kihisia pia.
Wiki iliyopita tuliona baadhi ya sababu zinazosababisha msongo wa mawazo, leo tutaangalia sababu nyingine zaidi zinazochangia tatizo hilo.
Mojawapo ya sababu hizo ni pamoja na maisha yasiyo na uhakika 'maisha kamari.' Wataalamu wengi wanaamini kuwa kutokuwa na maisha ya uhakika ni moja ya sababu za msongo.
Wengi tumekuwa watumwa wa maisha ya kisasa tukitaka kuishi katika daraja ambalo si letu. "Wote tunataka kuwa maarufu, matajiri, washindi wa bahati nasibu," anasem mwanasaikolojia Patrick Whiteside, mtunzi wa kitabu kijulikanacho kama 'little Book of Bliss'.
Aina hii ya utamaduni unatuweka katika shinikizo. Watu wanajishurutisha ili waweze kuwa na mafanikio na pesa, wanataka kuwa na nyumba kubwa, televisheni kubwa na magari ya thamani kubwa, lakini wanasahau umuhimu wa kuwa wenzi wazuri katika familia zao," anasema.
Mara nyingi, mtu anajikuta hana uchaguzi ila kuendelea na hali ya mawazo. Lakini ni muhimu ukathubutu kujaribu na kurudi nyuma huku ukifikiria juu ya uchaguzi ulioufanya awali. Kufikiria juu ya mabadiliko unayoweza kuyafanya kulingana na aina ya maisha unayoishi.
Kama hali ya mawazo inaendelea, inaweza kuleta matatizo makubwa katika kutekeleza majukumu ya kitaalamu kulingana na fani yako au maisha, au hata kuathiri afya yako.
Sababu nyingine ni matatizo ya kiuchumi. Kama mtu hana fedha za kukidhi mahitaji ya muhimu atajikuta katika hali mbaya ya kuwaza ambayo inaweza kumsababishia msongo.
Mtu huyo atajikuta katika lindi la mawazo , akijaribu kufikiri jinsi atakavyopata fedha kwa ajili ya kufanya biashara, au kusomesha mtoto au hata itakayomwezesha kuishi maisha mazuri.
Mwingine unaweza kukuta akiwaza juu ya nyumba na anataka kuishi katika nyumba ya hadhi fulani lakini hana uwezo wa kufanya hivyo, au pengine kuharakishwa kutoka katika nyumba katika kipindi ambacho alikuwa hajawa tayari kufanya hivyo, hayo pia yanaweza kuwa matatizo ambayo yanaweza kuleta msongo.
Sababu za msongo zina wigo mkubwa, wakati mwingine unaweza kukuta mtu anapata shinikizo kutoka kwa bosi wake, au hata ndugu anaoishi nao kama vile shemeji au wifi, au wakati mwingine kuachishwa kazi au kustaafu akiwa hajajiandaa.
Kwa wale wanaostaafu hupatwa na msongo pale ambapo hujikuta wakitakiwa kuachia nyadhifa zao wakati hawajajiandaa kwa ajili ya maisha mapya nje ya kazi. Wengine hujikuta hawajaweza kujenga nyumba au kuwa na biashara yoyote ya kuwaingizia fedha kwa ajili ya kuendeleza maisha yao yaliyobaki.
Msongo hutuathiri sote. Hivyo basi iwapo unaweza kutambua dalili basi unaweza kuudhibiti.
Mbali na sababu tulizoziona hapo juu, zipo sababu nyingine ambazo ni za kawaida kabisa, ambazo husababisha msongo kama kitisho, hofu na shaka.
Hofu inasababisha mtu kupatwa na msongo. Hii inajumuisha hofu ya kimaumbile, hofu ya kijamii, hofu ya kifedha na mengineyo. Katika hali ya kawaida, hali inakuwa mbaya wakati mtu anapohisi hakuna namna ya kupunguza vitisho, hiyo huathiri hisia na hivyo huwa vigumu kuzidhibiti.
Kiujumla tishio lolote katika mahitaji linaweza likasababisha msongo.
Hali yoyote ya utisho inasababisha hofu, ambayo huleta msongo. Hofu inaongoza kufikiria matokeo, ambayo ni chanzo halisi cha mawazo.
Wakati ambapo tuna shaka, hatuna uimara katika kutabiri, na wakati tunahisi hofu au tishio hali hiyo husababisha shaka.
Tabia ya utambuzi
Kunapokuwa na pengo kati ya kile tunachofanya na kile tunachofikiri, hapo tunashuhudia tabia ya utambuzi ambayo inahisiwa kama shinikizo, kwa hiyo kama ninafikiri kuwa mimi ni mtu halafu nikafanya kitu ambacho kitamuumiza mtu mwingine, hapo nitakuwa ninajiweka katika hali itakayonisababishia shinikizo.
Pengo hilo linaweza kutokea pale ambapo hatuwezi kufikia malengo yetu. Tunaamini kuwa waaminifu na tumejitoa kikamilifu lakini inapotokea jambo la kutukwamisha tusifikie malengo yetu hayo tunakumbana na mazingira yanayotufanya tuonekane kuwa si waaminifu au wenye uwezo wa kile tulichopanga kukifanya.
Mfano ni pale ambapo tunakumbana na tishio la kijamii, kwamba tusipofanya kitu Fulani, jamii haitatuelewa au tutataabika.
Chanzo kitokanacho na maisha
Kuna vyanzo mbalimbali vya msongo wa mawazo katika maisha ikiwa ni pamoja na kifo cha mume, mke, ndugu katika familia au rafiki wa karibu. Afya pia inaweza kuwa chanzo, hasa pale ambapo unahisi hali si nzuri katika mwili wako, ama kwa ugonjwa na ujauzito kwa mwanamke.
Uhalifu pia ni mojawapo ya mambo yanayoweza kusababisha msongo. Uhalifu kama vile kudhalilisha wengine kijinsia, kuvunja na kuiba, kudokoa au wizi wa mifukoni.
Kutumia dawa za kulevya
Katika ulimwengu wa sasa, watu wengi na hasa vijana, wamejikuta wakikumbwa na msongo kutokana na kujiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya, hali ambayo inawafanya kutojithamini au kukata tamaa ya maisha.
Dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia humfanya mtu ashindwe kujikinga na hatimaye kujikuta akijeruhiwa.
Mambo mengine ni mabadiliko ya ghafla katika familia kama vile mume na mke kutengana, kupata mtoto bila ya kutarajia hasa kwa wanawake walio katika ndoa.
Matatizo ya kimahusiano
Kila mtu hupenda kuwa na mahusiano ili kuoyesha ni jinsi gani anapendwa au kupenda.
Inapotokea kuwa hitaji la mtu katika mahusiano halikufikiwa, basi mtu hujikuta katika msongo ambao huathiri zaidi hisia, hili linaweza kuwa pia katika upande wa mahusiano mabaya na mpenzi wako, mwenzi wako, rafiki au ndugu katika familia, hata mfanyakazi mwenzako au bosi katika maeneo ya kazi.
Mabadiliko ya kimaumbile; kama kukosa usingizi na kuongezewa muda zaidi kazini, mtu kuwa mnene au mwembaba au hata kurefuka au kuwa mfupi isivyo kawaida, ni baadhi ya mambo yanayochangia msongo.
Mabadiliko ya kimazingira kama vile kuhamishwa eneo la kazi au makazi, mfano kutoka mjini kwenda maeneo ya shambani, kuhama shule na kwenda katika shule ambayo hupendezwi nayo huweza kumfanya mtu awe katika hatari ya kukumbwa na msongo.
Jambo jingine ni kuzidiwa na majukumu kama vile kuongeza ukubwa wa familia huku kipato kikiwa kidogo au kujikuta wategemezi wako wakiongezeka kwa ghafla, mfano watoto wa ndugu yako kuhamia kwako baada ya ndugu huyo kufariki yeye na mwenzake.
Msongo katika maeneo ya kazi
Nchini Uingereza, Idara ya Afya na Usalama inaorodhesha mambo sita makubwa ambayo yanachangia msongo katika maeneo ya kazi.
Hitaji la kazi: Udhibi walio nao wafanyakazi juu ya kazi wanazofanya na jinsi wanavyopaswa kuzifanya.
Uungwaji mkono unaoupata kutoka kwa wenzako na wakubwa wako. Mahusiano baina ya mtu na mwenzake, iwapo watu wanatambua wajibu wako na majukumu uliyonayo, na pia ni kwa kiasi gani kampuni inashauriana na wafanyakazi kuhusiana na mabadiliko ya maeneo ya kazi.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 331455; 0733 331455

MAANA YA MSONGO WA MAWAZO

KARIBU wapenzi wasomaji wetu katika mada yetu mpya ya siku ya leo, ambako tunaangalia maana ya msongo, chanzo chake na jinsi gani ya kukabiliana na hali hiyo.
Wazazi wengi huelewa zaidi mambo mbalimbali kuhusu msongo wa mawazo. Bila shaka, msongo ni mada yenye mazungumzo mengi. Ninaongelea kuhusu msongo katika usawa wa kazi na maisha ya nyumbani, msongo wa msongamano wa magari barabarani, msongo wa maisha katika jamii tunayoishi, na pia msongo wa kushughulika na mtoto anayelia.
Tuangalie jinsi ya kupunguza msongo mbali na fukwe za bahari, kubadilishana mawazo na watu wa aina mbalimbali na katika maeneo mbalimbali.
Ninaamini kuwa kama mzazi, unaelewa ni jinsi gani unavyojisikia unapoondoa msongo ulionao.
Katika yote yanayoongelewa, watu wengi wamekuwa na wakati mgumu wa kuelewa ni nini hasa, maana ya msongo. Msongo ni hisia, lakini ambazo hazionyeshi mihemko ya mtu.
Badala yake, inaonekana kuwa kitu kilichozoeleka katika mihemko mbalimbali tofauti, pamoja na kuchanganyikiwa, hasira, wasiwasi, woga, huzuni, na pia kukata tamaa.
Pia lipo suala la kimaumbile katika suala la msongo. Unaweza kujisikia mzigo katika kifua chako, unaweza kuhisi katika sehemu ya tumbo lako, au katika taya yako kutoka kwenye meno yako yaliyofungamana.
Ni dhahiri, bado hatujui kwa usahihi ni wapi msongo unapotokea.Kama unafikiria kuhusu hili, kwa upande mwingine, matukio ambayo yanamsumbua mtu mmoja hayawezi kuwa kwa mwingine, ambayo yataibua maswali.
Unaweza kujiuliza swali hili, hivi ni kweli msongo wakati wote huwa ni kitu kibaya? Na kama siyo, nini tofauti kati ya msongo mzuri na mbaya?
Majibu ya maswali haya yanakuwa hayajibiwi, ingawa wanasaikolojia na madaktari wamekuwa wakifanya utafiti juu ya msongo na matokeo yake kwa karibu miaka 200.
Hata sasa, kama unavyofikiria juu ya msongo katika maisha yako, na juu ya watoto wako, utakuta baadhi ya utambuzi wa kanuni za kisayansi siyo tu unashangaza, lakini pia usiofaa.
Kwa miaka mingi, wanasayansi wamekuwa wakielewa kuwa mwili unakubaliana na mazingira ya maumivu kwa kuruhusu baadhi ya homoni zinazosababisha msongo – kama chombo cha kufyatulia risasi ambayo inatumika kwa kupigana au kukimbiza maadui. Msongo mara nyingi husababisha kupanda kwa shinikizo la damu, kupanda kwa kisukari, mapigo ya moyo kwenda mbio, kupata tabu katika kupumua, mtiririko wa damu huhama kuelekea miguuni na kwenye ubongo na kutoka tumboni na kwenye utumbo. Kukaza kwa misuli, na ile hali ya kujisikia inapungua.
Kwa dozi ndogo, msongo unasaidia katika kuwaza na ustahimilivu. Hii inamaanisha kuwa unaweza ukawa unafanya mtihani ambao unaamini kuwa ni mgumu kama wa hesabu. Hivyo unatumia muda mrefu kufikiri njia ya kufanya na kupata jibu sahihi.
Hiyo ni hali ya kuwaza ambayo inazaa matunda mazuri kwa maana ya kukumbuka na kupata njia sahihi ya kufanya mtihani wako, japo imekugharimu muda mrefu katika kufikiri.
Unapokuwa na mawazo, katika ubongo wako, mishipa maalum ambayo imejiunganisha inashindwa kufanya kazi yake ya kutoa ufahamu au kuhisi hivyo hali ya ufahamu huenda polepole, pia vihisishi vinaweza kuwa kwa haraka zaidi.
Husababisha hali ya mwili kuwa na hofu inajionyesha wazi katika mwili wa binadamu, lakini kinyume chake ni kweli kwamba mawazo mazuri na furaha inaweza kukufanya kuonekana mwenye taswira ya furaha, kisaikolojia na kimtazamo wa nje.
Pia inapunguza mwonekano wa hofu, inapunguza mapigo ya moyo, na inaongeza mzunguko wa damu katika utumbo mdogo na tumbo (inapunguza mawazo na maumivu ya viungo).
Matokeo ya msongo wa muda wa ziada. Katika kupambana au kupigana na majukumu katika mwili wako kwa ghafla, baadhi ya misongo, ingawa ni midogo, misongo ya kila siku, kama msongo wa kuishi katika nyumba yenye kelele au kukaa kwa muda mrefu kwenye msongamano wa magari kila siku, pia inasababisha homoni hizo kuachia, kwenye kipimo kidogo sana.
Na ingawa athari zake ni kidogo, misongo inaongezeka.kwa hiyo, kama siku moja utachelewa kazini, gari lako likagoma, mtoto wako akaanza kulia, na mbwa wako akakimbia mbali, mchanganyiko wa yote husababisha kupatwa na msongo mkubwa. Hivyo huleta athari katika maisha yako.
Misongo hiyo inapokuwa siku baada ya siku, inaweza kusababisha matukio mabaya, zaidi ya kupata muda wa kupumzika na kupata ahueni. Nadharia moja kubwa iliyokubalika inasisitiza kuwa msongo wa kudumu unaweza kumdhoofisha mtu.
Kwa nini baadhi ya watu wanaonekana imara zaidi kuliko wengine katika kukabiliana hali ya msongo? Jibu ni uthabiti wa mtu ndiyo unaomwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha. Thabiti ni kiwango cha kitu kama mhimili katika daraja, kwa mfano linaruhusu kona pasipo kuvunjika. Sawasawa, na watu thabiti katika uzoefu wa kukabiliana na msongo bila kudhurika.
Watu thabiti wanategemea kuwa na mtazamo thabiti na mzuri katika maisha yao na hata yanapotokea matatizo ya muda, wanakuwa na uhusiano mzuri na watu ambao wanawasaidia kupata ufumbuzi wa matatizo yanayowaletea msongo wa mawazo.
Kwa mfano, katika masomo mengi ya makuzi ya watoto, tunaambiwa kuwa watoto waliowahi kuishi kwenye maisha magumu, maisha yao ya utu uzima wengi wao huwa na maisha mazuri na hubahatika kuwa na marafiki wazuri wanaowapa mielekeo mizuri ya maisha yao.
Wanapokuwa katika umri huo huwa wanasumbuliwa sana na msongo wa kutaka kuwafahamu wazazi wao ili na wao wapate nafasi ya kuwasaidia kimaisha kitu kinachowafanya mara nyingi kuwa katika wakati mgumu wa kuwa na mawazo pamoja na kuwa na mali.
Vyanzo vya msongo
Wote tunaweza kuchoka kama kitu kitakuwa tofauti au chenye changamoto kitatokea katika maisha yetu. Hata hivyo, ili kuwe na usawa, ni lazima tuwe na uwezo wa kuendana na mabadiliko kama yanavyotokea.
Mabadiliko ya kupita kiasi na ya haraka yanaweza kutokea mara kwa mara na kuwa chanzo kikubwa cha msongo na kisicholingana na maisha yetu. Mahitaji ya mabadiliko ya haraka ambayo ni rahisi kuwa makubwa kwa mwili na akili kuyashughulikia katika muda mfupi.
Wengi wetu wanahisi hatua za maisha zinaongezeka kwa kasi. Inaonekana kuna shinikizo la kawaida kazini na nyumbani. Sababu kuu tatu za maisha ya kisasa zinahusika.
Sababu ya kazi
Kuna mabadiliko makubwa kwa jinsi tulivyokuwa tunafanya kazi katika miongo iliyopita. Mashirika mengi yamepunguza wafanyakazi kwa hiyo hao wachache waliobakia wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii na kwa muda mrefu, wakati wengine wamekuwa na mikataba ya muda mfupi.
Nchini Uingereza nako pia wanafanya kazi kwa muda mrefu kuliko mahali pengine popote Ulaya, na teknolojia imekua, maana yake wanatumia e-mail, faksi na kupiga simu kokote wanapokuwa.
Sababu ya nyumbani
Watu wengi wamekuwa wakihama kutoka kwenye familia zao, na hawarudi tena kwa ndugu zao ambao ndiyo washauri wao wakuu katika mahitaji mbalimbali.
Sababu ya jinsia
Tatizo jingine linalochangia katika suala la jinsia, hasa katika familia, pale wanawake wanapokuwa na kazi nzuri zaidi ya waume zao, na kufanyika msaada mkubwa kwa familia.
Na wakati huo waume zao wanakuwa na kazi za kawaida ambazo kinawapatia kipato cha kawaida. Katika familia huwa tatizo kwa upande wa mwanaume ambao hupenda mara nyingi kuwa juu.
Mbali na wanaume kupenda kuwa juu, lakini inaonyesha kuwa mwanamke anapokuwa na kipato kikubwa kumzidi mumewe, mara nyingi hujisahau na kujiona kuwa yeye ndiye mhimili wa familia.
Kwa maelezo mengine hufikia mahali na kumdharau mumewe, hali hii hutokea si kwa wanawake wote bali wale ambao hujisahau kuwa wana wajibu upi kwa waume zao.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com0713 3314550733 331455

FIKIRI UWE TAJIRI - 10

“HAKUNA mtu anayependa kuwa masikini,” maneno hayo yalisemwa na George Shaw. Naye Sophie Tucker anasema: “Nimeshakuwa tajiri, nimeshakuwa maskini, katika hali zote hizo maisha ya utajiri ni mazuri.
Kuna aina ya mafanikio mtu anayoyapata bila kutumia fedha. Pia kuna mafanikio mengine ili yapatikane inabidi uwe na fedha, inategemeana ni wapi unapoanzia ili kufikia malengo yako unayokusudia.
Fedha au utajiri ni jambo ambalo tunalipata kutokana na juhudi mbalimbali ambazo zinatufikisha kufikia malengo tuliyokusudia katika fikra zetu.Kwanza inapasa kujipanga na kujua jinsi gani utafanyia kazi fedha hizo ili kufikia malengo na matarajio yako.
Watu wengi wanasema kuwa pesa inaleta afya. Pia ukumbuke kuwa furaha ya kweli haipatikani kutokana na vitu ulivyonavyo, bali inapatikana kutokana na jinsi ulivyo, pamoja na uwezo wa kuweza kutumia malighafi uliyo nayo. Unaweza kuwa na fedha ili mradi kufurahia uhuru wa mwili na akili.
Mtu hawezi kuwa huru kama atakuwa anafanya kazi ya mfululizo kila siku na kupata kipato kidogo, endapo mtu huyo itamlazimu kulipa zaidi ya kile anachopata, mfano analipa gharama kubwa.
Katika mfululizo huu utaelewa njia ya kukufanya uwe huru kutoka kwenye vikwazo unavyokabiliana navyo na kufurahia maisha ya utajiri.
Njia ya kwanza ni muhimu kama unazika, mara moja , ile hali ya kuona kuwa pesa ni mbaya au haina umuhimu. Pesa siyo mbaya. Kama Biblia inavyosema, “kupenda pesa ni kubaya.” Ni kweli kuwa, pesa ni muhimu. Ni muhimu kama chakula na nguo kinavyohitajiwa kununuliwa, malazi, elimu na ankara unazotakiwa kulipia.
Pesa ni muhimu kwa yeyote anayeishi katika jamii ya waliostaarabika, na kufikiri kuwa si muhimu ni kujidanganya.
Kumbuka kuwa ni haki yako kuwa tajiri. Pesa ndiye dereva wetu mkubwa, inaongeza mtandao wako wa kuwa tajiri, inakuwezesha kupata utajiri ili uweze kuwasaidia wengine, na kumiliki fedha kwa faida itakusaidia wewe na familia yako kuwa na malengo ya mafanikio. Uwezekano wa kuwa na pesa unachangamsha akili yako kufikiria kufikia malengo uliyojiwekea.
Pia ni kawaida kuwa huwezi ukawa na furaha kama wewe ni maskini, na unahitaji kutokuwa maskini. Umaskini au kutokuwa tajiri ni aina ya maumivu yanayosababishwa na upumbavu wa mtu wa kuzijua kanuni katika akili yake ambazo zitamwongoza katika mafanikio.
Umaskini ni uchafu, unakufanya kutokuwa huru, pia unadhoofisha ujuzi ulio nao. Uko katika aina ya ugonjwa. Mtu maskini anajiona kama mfungwa, umaskini unawafanya wanaume na wanawake kupenda kunywa pombe, kula madawa ya kulevya na mara nyingine kujinyonga.
Umaskini unafanya kitu chenye thamani, kipaji, watoto wenye akili kugeuka na kufanya uhalifu. Unawafanya watu kufanya mambo ambayo hawajawahi kufikiria kama wangeyafanya.
Utajiri si pesa tu, bali hata amani uliyonayo ni utajiri. Amani katika akili yako ni jambo la thamani lenye mafanikio. Katika hali yoyote ile unapokuwa na amani, unakaribisha utajiri katika maisha yako. Pia inakusaidia kuishi maisha yako katika maeneo yako mwenyewe unayoyapenda. inakupatia amani katika kile unachochagua, ndiyo maana maisha yako kila siku yanakuwa ya kitajiri na yenye mafanikio.
Mtu mmoja alisema kuwa utajiri unakuja kwa mtu ambaye anaona umuhimu wa utajiri. Kama maelezo yaliyotangulia yalivyosema, huwezi kuwabeba wengine kuelekea mafanikio, lakini unaweza ukawaonyesha njia ya kila mmoja kujisaidia mwenyewe.
Je, ni kiasi gani cha pesa ambacho unataka kukimiliki? Chukua dakika chache na ujibu maswali yafuatayo.
Umepata nini kwa ajili ya kufanya biashara? Dunia imekufanyia nini kwa kile unachokifanya? Watu wangapi wanafanya kile unachokifanya? Utakapojibu maswali hayo, utajua ni kwanini baadhi ya watu wanakuwa na pesa nyingi zaidi ya wengine?
Kwa hiyo unatakiwa kuondoa mawazo yote uliyonayo juu ya umaskini, yanayokuzuia usisonge mbele kimaendeleo.
Umaskini si adui. Adui ni mtu ambaye wakati wote anaangalia si tu udhaifu alionao bali anauabudu pia.
Amekuwa akitumia nguvu zake kuwashawishi wenzake kuwa hakuna chochote wanachoweza kukifanya wakafanikiwa.
Ondoa kabisa mawazo yako potofu kuwa ni lazima uwe maskini. Kumbuka umaskini na mafanikio unatokana na akili yako. Kama utaamua kufuta mawazo ya umaskini, ni lazima uielekeze akili yako kwenye bahati njema, mafanikio na kufaulu. Kumbuka kuwa siri uliyoigundua ni sawa na shamba la almasi. Hii habari inaelezea siri kubwa ya maisha kwamba una shamba kubwa la almasi. Hizi almasi zilizopo zinajulikana kama jambo lenye kuwezekana na uwezo. Kuna uzuri mwingi wa vito vya thamani ndani yake, inatakiwa subira ili uweze kuchimba.
Ujuzi katika maisha yetu ya kila siku juu ya suala la kufikia malengo yenye mafanikio, unafundisha kuwa thamani ya sheria nyingi zinazosisitizwa katika kufikia malengo yako na kuwa tajri ni elimu.
Kwa kuwa elimu itakufanya kuwa mwelewa. Pili, kuwa mdadisi. Unapokuwa mdadisi uwapo shuleni, kazini au katika jumuiya. Jifunze kutoka kwa wengine, walimu wako, familia yako na rafiki zako. Kila mmoja ana kitu tofauti kwa ajili ya mwingine.
Tatu, amua ni nini unachohitaji nje ya maisha unayoyaishi. Kabiliana na changamoto mpya zinazokutatiza. Nne, kuwa tayari kupata faida katika nafasi zote zinazotokea kwako. Si tu kwa zile nafasi zinazogonga katika mlango wako. Kuwa wa tofauti.
Tano, usichukie. Chuki haizalishi. Wala haitakujengea chochote katika maisha yako. Na katika yote hayo, kuwa mkweli wa nafsi yako.
Kuwa mtu wa thamani na uligundue hilo. Jiamini. Kila siku uwe na maono mapya ambayo ni imara.
Fikiri uwe tajiri imefikia tamati.
Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine mpya.
lcyngowi@yahoo.com 0713 331455 0733 331455

FIKIRI UWE TAJIRI - 9

ILI haiba iweze kuwa na mafaniko ni lazima idumu huku ikifanya kazi ya kutambulika ya Daniel James inataja ukweli kuwa haiba yenye mvuto si tu inaweza kufungua milango mingi bali inaweza pia kukusaidia ili uweze kuwa na kiwango cha juu cha ufanisi.
James alikulia katika nyakati za giza za huko Frorida nchini Marekani ambapo kulikuwa na ubaguzi wa rangi katika mji huo.
Miaka michache baadaye aliweza kushinda ubaguzi wakati akiwa katika jeshi baada ya kuwa Mmarekani mweusi wa pili kupandishwa cheo na kuwa Jenerali katika Jeshi la Anga la Marekani na kuwa mtu wa nne katika historia ya utumishi wa jeshi.
Utajiri na mafanikio ya James vilitokana na uwezo wa kuweza kutumia kikamilifu ushauri ambao mama yake alishirikiana naye wakati alipokuwa mtoto.
“Mama yangu alinifundisha misingi,” alikumbuka. “Upendo wa Mungu, upendo wa nchi na upendo wa mwanadamu. Na si kujaribu kuwa makini katika kukosoa kwamba umesahau kuangalia katika mazuri ambayo yako kwetu sisi wote.
“Kwa baadhi ya watu utahitajika kuchimba sana ili kuweza kupata sifa nzuri, lakini kila mtu anastahili pongezi na kuthaminiwa”.
Licha ya kukosekana haki ambako nimekumbana nako nilifahamau thamani ya kuthamini. Kama ningejazilizia sifa na kuthamini wafanyakazi wenzangu, nilijikuta kuwa nilikuwa na furaha ya kufanya hivyo.
James aliambatana na hekima hii maisha yake yote alikuwa na uwezo wa kuwafanya wale wote waliokuwa kando yake wajihisi kuwa ni maalumu kwa kuwatambua mmoja baada ya mwingine kwa kile kizuri walichofanya.
Alipuuzia ile dhana ya kwamba watu wengi unaokutana nao hujihisi kuwa ni bora zaidi yako kwa namna fulani. Aliamua kuugawa moyo wake kwa ajili ya wale waliokuwa wadogo kwake kwa kutambua umuhimu wao na mchango wao.
Aliwapa kile walichohitaji na mara nyingi ilikuwa ni kusifu kwa uwazi na uaminfu pamoja na kuthamini.
Ninaamini kuwa hutadharau mifano hii rahisi, lakini pengine zawadi yenye maana sana ambayo unaweza kuitoa kwa mtu mwingine nayo si nyingine isipokuwa kuthamini.
Kama bado unafikiri kuwa una mashaka juu ya dhana ya kwamba kusifu na kuthamini vina nguvu ya kimiujiza basi hebu jifunze katika mfano huu.
Kisa hiki kinaweza kuwa sawa na kilichopitwa na wakati lakini ujumbe wake unaonekana kuwa mbele ya wakati. Ilikuwa ni kawaida ya mtu mmoja mzee kukaa nje ya ukuta wa mji wa kale wa hapo alipokuwa akiishi akifanya kazi ya kuangalia wapita njia ambao walikuwa wakija kutoka upande mmoja na kuishia katika upande mwingine.
Kwa kawaida alipendelea kukaa katika kivuli akiwa amezungukwa na watoto akiwasimulia hadithi walizozipenda. Katika muda mwingi wa mchana wapita njia wengi wangependa kusimama hapo na kuzungumza naye.
Siku moja wakati wa majira ya joto mgeni moja alifika hapa na kuamua kusimama kwa muda ili aweze kuzungumzia na yule mzee ambaye kwa wakati wote huo alikuwa makini akiwasimulia hadithi marafiki zake watoto.
Mgeni yule alimsogelea mzee yule na kumuuliza: “Ninafikiria kuhamia katika mji wako huu je, unaweza kuniambia ni watu wa aina gani ambao wanaishi katika mji huu?”
Haraka mzee yule alisema, “Ni aina gani ya watu huishi katika mji ambao wewe unatoka?” yule mgeni alijibu kwa kusema: “Watu katika mji wangu si wakarimu, wanadanganya na kuiba na kusema uongo. Wanazungumza vibaya kila mmoja juu ya mwingine. Ninaondoka katika mji huo kwa sababu ya watu wasiofaa ambao wanaishi huko.”
Yule mzee alimwangalia mgeni yule kisha akasema: “Ninasikitika kukufahamisha kuwa utakutana na watu wa aina hiyo hiyo katika mji huu.” Na bila ya kusema neno lolote mgeni yule aligeuka nyuma na kuondoka zake na kumuacha yule mzee akiendelea na kuwasimulia watoto hadithi.
Muda mfupi baadaye mgeni mwingine akaja hadi katika lango la kuingilia katika mji huo, naye pia akasimama na kuanza kuongea. Akasema: “Mtu wangu mwema, ninahitaji kuingia mjini huu wa kwako je, unaweza kuniambia ni aina gani ya watu ambao wanaishi humo ndani?”
Yule mzee akauliza swali kama lile la mwanzo alilomuuliza yule mgeni wa mwanzo. “Ni aina gani ya watu ambao wanaishi katika mji ambao wewe unatoka?” Mgeni yule akajibu kwa kusema kuwa “Watu katika mji wangu ni wema sana. Wana urafiki na kila mtu wana upendo na wakati wote huwa wanaangalia uwezekano wa kutenda mambo mema kwa ajili ya watu wengine. Nilisikitika sana kuondoka katika mji ule kutokana na ukarimu na utu wema wa watu wake lakini hata hivyo kazi ninayoifanya inanilazimu kuondoka katika mji ule.”
Mzee yule alimshika mkono mgeni yule na kumwambia: “Utapata watu wa jinsi hiyo hapa. Karibu katika mji wetu.” Mgeni yule akatembea na kuingia kupitia katika lango la mji.
Watoto walikaa kimya. Baadaye mmoja wao alimsogelea mzee yule na kumuuliza “kwa nini babu hukuwaambia watu wale ukweli? Ulimwambia mmoja kuwa watu wetu walikuwa ni wabaya na mwingine kuwa watu wetu ni wazuri.” Mzee aliwaomba waketi ili aweze kuwaeleza.
“Nimewaambia ukweli,” alisema. “Mnaona, bila kujali kuwa mnakwenda wapi au mnafanya nini mtakuta aina ya watu mnaowataka katika jamii nyingine. Kama unataka watu wazuri mtawapata, lakini pia kama mnatafuta watu wabaya mtawapata pia bila shaka ndio mtakaopata. Kila mmoja wetu hapa ana sifa nzuri zaidi ya mbaya alizonazo. Siku zote jaribu kutafuta kilicho chema kutoka kwa watu wengine”.
Wakati fulani mtu mmoja alisema: “Ninajua furaha ni nini kwa sababu nimeshafanya kazi njema.” Mtu huyo alisema hivyo kwa sababu alifanya kazi nzuri na akapata kuthaminiwa na kusifiwa na wenzake kutokana na kile alichofanya.
Kutambua, kusifu na kupenda ni vitu vyenye kutia hamasa sana katika maisha. Tunapokumbana na vitu hivyo huwa tunaondoka katika eneo hilo ambalo tumekutana navyo tukiwa na furaha na kujihisi wenye thamani.
Kinyume chake ni kwamba tunapokosolewa huwa tunajihisi kuwa hatujitoshelezi na tusio na mwelekeo. Kwanini tunajisikia furaha pale tunaposifiwa? Ni kwa sababu kusifiwa maana yake ni utambulisho na uthibitisho wa thamani yetu.
Sifa huonyesha hutuambia kuwa tunaheshimika, tunahitajika na kuthaminiwa na hivyo kuonyesha kuwapo kwetu. Mara kadhaa huwa tunazuia sifa.
Wakati mwingine ni kwa sababu tunataka kuonekana kama wazalendo zaidi au wabinafsi zaidi. Lakini katika wakati mwingine hata hatuahangaiki kufanya juhudi.
Tunasahau kuwa kila mmoja hufurahia kutambauliwa, neno la kumsifia. Kusifia ni uthibitisho wa thamani yetu. Kusifu ni kukaririsha ushuhuda kuwa hisia zetu za ndani zimehalalishwa. Hutuambia kuwa tunahitajika.
Hivyo basi sifia wengine lakini pia usisahau kujisifia wewe mwenyewe pale unapostahili. Sifia maisha. Ni rahisi sana na jambo lenye kufurahisha kushiriki katika maisha ya mtu mwingine kwa kusema maneno machache lakini yenye kujenga.
Kusifu kwa dhati huhitaji nguvu kidogo sana na hufanyika kwa muda mfupi. Lakini matokeo yake huonekana baada ya muda mfupi lakini yakadumu kwa muda mrefu.
Tukutane wiki ijayo.
lcyngowi@yahoo.com 0713 331455, 0733 331455

Twitter Facebook