Sunday, December 27, 2009

JIAMINI UTAFANIKIWA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za Maisha Yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi ambavyo kila mmoja anapaswa kujijengea uwezo wa kuweza kujiamini ili kupata mafanikio.
Kila mmoja anapaswa kutamani kuwa kiongozi yeye mwenyewe, ili aweze kujenga uwezo wa kuwa na maendeleo binafsi, pasipo kutamani maendeleo ya mtu mwingine.
Kwasababu hakuna mtu atakayemlazimisha mtu mwingine kupata mafanikio.
Lakini kwa upande mwingine, suala la mafanikio ni jambo linalotokana na muda uliopo, kujitoa na kufanyia kazi mambo mbalimbali mtu anayoyapanga.
Hivyo ujue wazi hakuna mtu atakayekulazimisha wewe kupata mafanikio, bali inakupasa kufanya bidii binafsi ili ufikie matarajio ya juu uliyojipangia.
Haya yakizingatiwa, kila mmoja atakuwa na ari ya kujisimamia, kufanya kazi kwa bidii katika mipango mbalimbali ya maendeleo ya ukuaji wa uchumi.
Sasa basi ili uweze kukua na kupata maendeleo, inakupasa kila jambo unalolipanga uweze kulitekeleza.
Ni vema kuanza kufanya jitihada binafsi za kupata maendeleo, pamoja na kufanya tathmini ya hapo ulipo na ulipotoka, taratibu utajikuta unapiga hatua siku baada ya siku.
Kwa kuwa, tayari unayo maabara iliyosheheni kila hitaji la mwanadamu, unayotakiwa kuichunguza na kuifanyia kazi, ni vema kujibidiisha ili uweze kukitumia kila kifaa kilichopo ndani yake, kwa ajili ya maendeleo.
Hakuna kikwazo chochote katika maabara hiyo, kinachoweza kukukwamisha, kama utajitambua kama wewe ni mhusika mkuu katika maabara hiyo ni wazi utapenda kujua kazi ya kila kifaa.
Kwa kuwa, ndani ya maabara hiyo, hakuna kitu cha kununua, kodi ya kulipa, wala ada ya aina yoyote ila unaweza kuitumia vile unavyopenda bila malipo yoyote.
Kama wewe ni msimamizi katika maabara yako mwenyewe, utapenda kufanya vile wanasayansi wengine wanavyofanya.
Unaweza kushangaa kwa nini watu wengi wana uelewa mdogo wa kufikia mafanikio, wakati wanazungukwa na wenye mafanikio makubwa.
Hii ni kwa sababu watu wengi hawafuatilii mambo yanayofanywa na wengine ili kufikia malengo makubwa.
Hivyo basi, Mtunzi David Sachwartz, nia yake ni kukusaidia kwa kuchunguza na kuangalia undani wa mambo yanayofanywa na wengine ambao wameweza kufanikiwa.
Kuna uchaguzi wa aina mbili wa kukusaidia ili uweze kufanikiwa; mojawapo ukiwa ni kupenda kujifunza kwa kuchunguza kila kitu unachokiona na kuamini kuwa kinaweza kukupatia maendeleo.
Pia unaweza kuchagua mifano ya watu wawili ambao unaweza kuwatumia kwa ajili ya kujifunzia katika kupata mafanikio yako.
Unatakiwa kuwachagua watu ambao mmoja wao, amefanikiwa na mwingine ambaye hajafikia mafanikio, ambao unawajua vema.
Anza kufuatilia kila jambo wanalolifanya, utapata somo litalokufumbua macho.
Kila unachojifunza kwa watu hao, kinakuwezesha kupiga hatua zaidi, lengo lako likiwa ni kuangalia kanuni za kufikia mafanikio. Pia kwa kutumia mifano ya watu hao, ndivyo utakavyopata mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za maisha kufikia mafanikio.
Ni jambo la kufurahisha unapokuwa na ujasiri, na kufanikiwa kila unachopanga, kujiangalia unavyokuwa siku baada ya siku na mwezi baada ya mwezi.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’, mtunzi wake ni David Schwartz.
Tukutane Alhamisi ijayo.

HUU NDIO UGONJWA WA KUSHINDWA KUFIKIA MALENGO

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila alhamisi.
Leo tutaangalia jinsi ya kukabiliana na ugonjwa wa kushindwa kufikia malengo.
Kila mmoja tayari ana vifaa vya kutosha katika maabara yake ambayo anaweza kuitumia kwa ajili ya kazi na kujifunza.
Maabara ambayo ina kila kitu kinachokuzunguka katika dunia hii. Ambamo hutapata vikwazo, kwa kuwa kila utakachojifunza utajiona kama wewe ni mtaalamu.
Ukiweza kuitumia vizuri maabara hiyo, itakuwezesha kumaliza matatizo yako ya kifamilia kama vile, kulipia kodi ya nyumba, kulipia ada za shule na mambo mengine yanayofanana na hayo. Hivyo unaweza kuitumia maabara hiyo kwa uhuru zaidi jinsi unavyopenda.
Kwa upande mwingine, unaweza kuwaza jinsi ya kuwa na malengo makubwa katika maisha, kwa kupenda kujifunza kwa wengine waliofanikiwa.
Lakini angalizo lililopo, unatakiwa kujifunza kutoka kwa wengine kwa uangalifu. Pale unapopata jambo linalokufaa lifanyie kazi.
Unapoendelea kujifunza kutoka kwa wengine, utaona kuwa, watu wasiokuwa na mafanikio wanataabika katika akili zao kwa ugonjwa wa kufikiri.
Kila mtu asiyefikia malengo ya mafanikio amekuwa na ugonjwa huo kwa kiwango kikubwa.
Na mara zote mtu mwenye malengo makubwa hupenda kujiuliza ni kwanini hapo alipofikia hajafanikiwa, kwa nini hana kitu fulani au kwanini hawezi kufanya jambo fulani, ili aweze kupiga hatua zaidi ya hapo alipo.
Kama ugonjwa mwingine wowote unavyompata mtu, ugonjwa wa kufikiri unakuwa mbaya sana endapo hautatibiwa vizuri.
Muathirika wa ugonjwa huu, anakuwa akiwaza mambo mengi, kama vile ‘najaribu kufanya jambo hili na lile lakini sipati mafanikio’ na kuendelea kuwaza: “ Je, ni afya mbaya niliyonayo” au ni ukosefu wa elimu? Umri mkubwa? Umri mdogo? Bahati mbaya? Ama kutokuwa na bahati ya maisha? Mke? Ama jinsi nilivyolelewa na familia yangu?”
Hivyo mtu huyo aliyeathirika na ugonjwa huo, asipojigundua ataendelea na hali hiyo katika maisha yake.
Ili kukabiliana na hali hiyo, ni vizuri kujizoeza kuwa na mawazo chanya yenye mafanikio, ambayo ndiyo tiba ya ugonjwa wa kushindwa.
watu wenye ugonjwa wa kushindwa huwa na visingizio mbalimbali kama vile ‘afya yangu siyo nzuri’. Hiyo hufanya kila siku anapopata changamoto ya maisha badala ya kutoka hapo alipo, kuwa na jambo lolote la utetezi fulani.
Anakuwa na afya mbaya katika aina tofauti tofauti, ambacho ndicho kisingizio chake anaposhindwa kufanya jambo linalompatia maendeleo.
Wapo watu wengine wamekuwa wakisingizia wana matatizo ya moyo, na wamekwenda kwa daktari zaidi ya mara nne, na kila wanapokwenda ugonjwa hauonekani.
Kuendelea kueleza kuwa, una ugonjwa wa moyo, mwisho wa siku tatizo hilo litakupata kweli. Kinachotakiwa ni kuishinda hali hiyo na kusonga mbele katika kupata maendeleo yako katika maisha, bila kujali unasumbuliwa na kitu gani.
Sasa basi yapo mambo manne ambayo yanaweza kukupa afya njema na kuondokana na hiyo hali inayokufanya ukate tamaa, ama kufikiria kuwa huwezi kila jambo lililopo mbele yako.
Kwanza usikubali kuizungumzia afya yako. Kadiri unavyozungumzia kuhusu ugonjwa unaokusumbua, hata kama ni wa kawaida, ndivyo utakavyozidi kukusumbua.
Kuzungumzia kuhusu afya yako kama ni mbaya ni kama unaweka mbolea kwenye mbegu zilizopandwa.
Kuzungumzia afya yako ni tabia mbaya. Inachosha wengine. Watu waliofanikiwa wana tabia ya kutokuzungumiza afya zao zinapokuwa mbaya.
Pili usiwe na hofu juu ya afya yako. Fanya kile unachokusudia ili kufikia malengo mazuri.
Tatu, jione kuwa afya yako ni njema haina kasoro. Na pia endelea kujikumbusha kuwa, maisha yapo kwa ajili ya kuyafurahia. Usipoteze. Wala usiishi kwa kufikiri juu ya kulazwa hospitali.
Vile vile usipende kuchunguza kwa nini mipango unayoipanga haifanikiwi, bali ichekeche akili yako kuelekea njia ya mafanikio.
Tukutane wiki ijayo.

AKILI YAKO NI KIWANDA CHA MAFANIKO

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tunazungumzia ili ufanikiwe unatakiwa ufanye nini.
Ni ukweli usiopingika kuwa, ili ufanikiwe katika maisha yako, inakubidi ufanye jitihada ya dhati. Kwa kujiuliza ni wapi uliposhindwa, ili uweze kuongeza bidii.
Vile vile, ni vema kuangalia udhaifu wako ulipo, ili uweze kurekebisha pale unapokosea katika kufikia mafanikio unayoyataka.
Watu wengi hupenda kuwa na mafanikio makubwa, lakini hawaonyeshi jitihada za dhati za kuwatoa pale walipo na kuwasogeza mbele.
Mara zote hukata tamaa kwa kuwaza mambo ambayo huwarudisha nyuma, hawako tayari kukubaliana na ukweli kuwa wanaweza kufanya jambo lolote ili kufikia malengo makubwa, cha msingi kinachotakiwa ni jitihada.
Hivyo basi, ni vizuri kuiambia nafsi yako, kuwa wewe unaweza kufanya jambo fulani kubwa litalokutoa hapo ulipo na kukufikisha sehemu nyingine yenye mafanikio zaidi.
Watu wengi hawaamini kuwa, Mungu amewabariki kwa kuwapa utajiri mwingi katika maisha yao, kwa kuwa, hawajui akili, nguvu, vipaji mbalimbali walivyonavyo ni utajiri tosha Mungu aliowapa katika maisha yao.
Ni vema kujiamini kuwa unaweza kufanya jambo kubwa katika maisha. Jitihada katika jambo lolote linakuleta mafanikio, kwa kukutoa katika hatua moja na kukupeleka katika hatua nyingine.
Vinginevyo utabakia kila siku ukiiambia nafsi yako, kwa nini wengine wanafanikiwa na wewe unabaki katika hali ile ile.
Jione kuwa wewe ni mtu wa thamani na ni mtu wa daraja la kwanza. Pia jenga hali ya kujiamini katika kila jambo unalotaka kulifanya.
Jiamini wewe mwenyewe na mambo mazuri yatatokea kwako, usiwe na hali ya hofu katika mambo uyafanyayo.
Akili yako ni kiwanda cha fikra. Ni kiwanda kilicho na shughuli nyingi. Hivyo itumie kwa busara upate mafanikio mengi.
Utakapoitumia akili yako vizuri utajikuta kila siku unapiga hatua zaidi. Kamwe usiiruhusu akili yako kuwaza kushindwa.
Unapodhamiria kufanya jambo fulani amini kuwa utafanikiwa. Wasiwasi utakufanya ushindwe katika kila unalotaka kulifanya.
Inuka, mlango wa mafanikio uko wazi na ujiweke kwenye kumbukumbu sasa kwamba unajiunga na kundi ambalo linakubali mabadiliko katika maisha.
Na hatua ya kwanza katika maisha yako, ambayo huwezi kuiepuka, amini kuwa unaweza kufanikiwa.
Je, ni jinsi gani, unaweza kuwa katika hali ya kujiamini kwamba unaweza kufanya jambo lolote na ukafanikiwa?
Ni pale tu utapofikiri kuhusu mafanikio yako na siyo kushindwa, uwapo kazini kwako ama nyumbani.
Hata pale utakapoona unapokabiliwa na hali ngumu, jiambie kuwa utashinda. Na kama upo ushindani kati yako na mtu mwingine, fikiri kuwa, una uwezo wa kushinda na si kushindwa.
Na nafasi ya kushinda inapoonekana, fikiri kuwa unaweza na si kwamba huwezi. Akili yako mara zote ifikiri kuwa unaweza kufanya jambo la mafanikio katika maisha.
Hali ya kuwaza mafanikio inakufanya katika akili yako uweke mikakati ya kukufanya upige hatua zaidi. Kinyume na hapo, utakaporuhusu akili yako kuwaza hali ya kushindwa, kamwe hautapiga hatua yoyote, kila mara utabakia pale pale.
Jambo jingine jikumbushe kwamba wewe ni bora kuliko unavyodhani. Watu wenye mafanikio si kwamba wana nguvu zaidi ya wengine.
Wala mafanikio si suala la kuona mtu fulani ana bahati, bali ni hali inayoweza kujengwa na mtu mwenyewe kwa kuongeza bidii.
Panda kuwaza mambo makubwa, ukubwa wa mafanikio yako unategemea jinsi unavyowaza. Kama unawaza malengo madogo, utarajie kupata mafanikio madogo.
Unapofikiri malengo makubwa, unakuwa na mafanikio makubwa pia.
Kumbuka hili, mawazo na malengo makubwa, mara zote yanarahisisha mambo yako na kukufanya usipate vikwazo vingi, tofauti na unavyowaza malengo madogo.
Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa kitabu cha ‘The Magic of Thinking Big’ kilichotungwa na David Schwartz.
Tukutane alhamisi ijayo.

AMINI KUWA UNAWEZA KUFANIKIWA

MSOMAJI wangu, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kuwa na malengo makubwa katika maisha.
Kufikiria mambo makubwa katika maisha, kunakuwezesha kuishi maisha mazuri, yenye furaha, utimilifu, kipato kizuri, marafiki na heshima.
Mafanikio maana yake ni kupata mahitaji unayohitaji, kustawi katika maisha, kuwa na nyumba nzuri, kupata safari, kuwa na vitu vipya, fedha zinazotosheleza mahitaji, pamoja na kuwapa watoto wako mahitaji ya muhimu.
Vile vile kwa maelezo mengine mafanikio ni kupandishwa cheo kazini kwako, kuendelea kuwa karibu na watu katika biashara zako na maisha yako kwa ujumla.
Pia kwa maelezo mengine, ni kujiheshimu, kuendelea kuwa na furaha pamoja na kutosheka katika maisha, kuwa na uwezo wa kufanya zaidi kwa wote wanaokutegemea.
Maana yake nyingine ni kushinda ama kufaulu katika maisha.
Kila mwanadamu anapenda kuwa na mafanikio katika maisha yake, hakuna hata mmoja anayefurahia hali ya kutokupiga hatua katika maisha, pia hakuna anayependa kuwa nyuma katika maisha haya tunayoishi.
Hivyo ni vizuri kupenda kujenga imani ya kujiamini kuwa unaweza kufanya jambo fulani ulilokusudia na kufanikiwa.
Kwa kuwa, mtu yeyote anapoweka nia kuwa anaweza jambo fulani, anafanikiwa. Lakini kinyume cha hapo, kamwe hatafanikiwa, atabakia katika hatua ile ile kila siku, ilhali wengine wakiwa wanasonga mbele.
Kila siku ulimwenguni, vijana wanaomaliza vyuo huanza kazi mpya. Kila mmoja anafikiria kuwa siku moja atafurahia mafanikio yatayompandisha juu kwa kumtoa hapo alipo na kumpa nafasi nyingine nzuri zaidi.
Lakini wengi wa vijana hao, hawafikirii kwamba ipo siku wanaweza kufika mbali zaidi ya hapo walipo. Matokeo yake, hawafiki mbali kwa kuwa hawana imani ya kuwatoa hapo walipo.
Matokeo yake, hubakia kuwa watu wa kawaida katika maisha yao.
Lakini kuna baadhi ya vijana wachache, wanaoamini kuwa, katika kipindi kifupi, tokea waanze kazi, watakuwa wameshasonga mbele zaidi.
Wanakuwa wanawaza kufika mbali zaidi na kuamini hivyo kunatokana na imani yao hiyo na kufikia pale walipokusudia.
Vijana hao huwa wajanja kwa kuwatazama wale waliowatangulia, upungufu wao na kufikiria jinsi ya kufanya vizuri zaidi.
Huwa wanawatazama wale waliofanikiwa kwamba wanakabilianaje na vikwazo mbalimbali na kufanya maamuzi ya busara.
Wanakuwa watu wanaokusudia kuwa na mafanikio, hivyo wanafanya jitihada mbalimbali ili kufikia walipokusudia.
Mara nyingi katika maisha yetu ya kawaida, unakuta mtu anakuwa anapenda kufika mbali katika maisha lakini anakatishwa tamaa na wengine.
Cha msingi, unapaswa kufanya kile ulichokusudia. Usiwe mwepesi wa kukata tamaa katika maisha yako. Na matokeo yake utayaona.
Unapokuwa na imani ya kufanya jambo fulani, kamwe usikate tamaa, kinachokupasa ni kufikiri mbinu ya kukutoa hapo ulipo na kusonga mbele.
Unapokuwa jasiri kufanya jambo fulani, kunawafanya na wengine wakuamini kuwa unaweza.
Hivyo unapoamini kuwa unaweza kufanya jambo fulani, utafanikiwa. Kwa wale wasiokuwa na imani ya kufanikiwa hata wanapofanya jambo hukwama njiani, kwa kuwa tokea awali walishaona hawataweza.
Unapokuwa na imani kuwa huwezi kufanya jambo fulani, ama kuwa na wasiwasi wa kufanya jambo, akili yako inapata sababu ya kukubaliana na kile unachokiamini.
Hofu, wasiwasi, kutokuamini kuwa unaweza, vinakufanya ushindwe kufikia malengo uliyojiwekea.
Hivyo ni vema kuwa na mawazo ya ushindi ili uweze kufanikiwa.
Imani ni kipimo chako katika maisha ambacho kitakuongoza. Kama unaamini kuwa kamwe hautakuwa tajiri, hali huwa hivyo hivyo.
Kama unaamini hutaweza kufanya mambo makubwa katika maisha, ndivyo itakavyokuwa. Kama unajiona kuwa wewe si wa muhimu, utaendelea kuonekana hivyo hivyo.
Kwa mtu anayewaza mambo makubwa, anakuwa anaamini kuwa atakuwa na utajiri, ndivyo inavyokuwa kwake.
Anaamini kuwa ataweza kufanya shughuli ngumu ambazo zitaMfikisha mahali pazuri na ndivyo inavyokuwa.
Kila kitu anachokifanya, jinsi anavyochukuliana na watu, tabia yake, mawazo yake, vyote vinamweka katika nafasi nzuri ya kuwa na mafanikio zaidi. Na kuonekana ni mtu wa maana.
Mtu ni bidhaa ya mawazo yake mwenyewe kwa kuamini na kufikiri mambo makubwa.
Tukutane Alhamisi ijayo.

KUWA NA MAWASILIANO MAZURI KAZINI KWAKO

MSOMAJI, katika mfululizo wa makala hizi za maisha yetu, nimedhamiria kukuletea kitu kipya kila Alhamisi. Leo tutaangalia jinsi gani unaweza kuwa na mawasiliano mazuri katika ofisi unayofanyia kazi.
Ni ukweli usiopingika kuwa, wale wote wanaofanya kazi maofisini, hutumia muda mwingi zaidi wakiwa ofisini kuliko nyumbani.
Hivyo ni muhimu kufurahia kazi ile unayoifanya na kuwa karibu na wale wote unaofanya nao kazi kwa muda huo, kwa sababu, wakati mwingine kazi tuzifanyazo husababisha msongo, hivyo kama unapata msaada kutoka kwa wenzako, inakusaidia kuondoa hali hiyo.
Lakini kwa upande mwingine, unaweza ukajikuta kuwa bila sababu ya msingi unapata upinzani katika shughuli zako unazozifanya kutoka kwa wafanyakazi wenzako.
Na kwamba, pasipo sababu ya msingi unakuta watu wanakutendea matendo yanayokuudhi, unachotakiwa kukifanya ni kuwasamehe.
Unaweza ukawa mwema kwao, lakini wakakudharau, endelea kuwa mwema kwao.
Unaweza ukawa mpole, wakatumia nafasi hiyo kukuhadaa, endelea kuwa mpole kwao.
Ukiwa katika shughuli zako, unaweza ukaamua kutafuta furaha lakini wengine wakakuonea wivu, usivunjike moyo, endelea kuwa na furaha hiyo unayoitafuta.
Au unaweza kujikuta kuwa, mambo mazuri unayoyafanya leo, kesho yanaweza yakawa yamesahauliwa, Endelea kufanya vile vile bila kupunguza.
Pamoja na upinzani unaoweza kukutana nao katika ofisi yako, elewa kuwa na mawasiliano ni muhimu katika eneo lolote la kazi.
Kuzungumza na kusikiliza wasimamizi wako na wafanyakazi wenzako ni muhimu, si tu kwa ajili ya mafanikio yako, bali kwa ajili ya mafanikio ya kampuni yako pia.
Jifunze njia sahihi za kuwasiliana na wafanyakazi wenzako kwa njia mbalimbali, pia weka mazingira bora ya kazi kwa kila mmoja.
Penda kujifunza kusikiliza kwa makini, kusikiliza mtu ni jambo la muhimu sana, ni zaidi ya kuzungumza.
Kwa kuwa, kusikiliza kunakufanya kuwaelewa wafanyakazi wenzako, mawazo na thamani yao.
Kuwa na tabia ya kumsikiliza mwenzako na uliza maswali ili uwe na uhakika wa kile anachokizungumza na matarajio yake.
Pili, watendee wenzako vile unavyotaka wakutendee wewe. Kila mmoja mheshimu jinsi alivyo. Usimwingilie anapofanya shughuli zake, usimbughudhi na wala usigombane naye kuhusiana na vifaa vya ofisini.
Unapohitaji kufanya jambo mwombe na ukimaliza mshukuru, usisite kumpa sifa zake pale anapostahili.
Kuwa mwangalifu na ishara za mwili unazotaka kuzitumia. Kamwe hata kama hupendi kusikiliza jambo unaloambiwa na mfanyakazi mwenzako, epuka kushika shika mikono yako, kugonga gonga miguu yako au kuzungusha macho yako.
Kwa kufanya hivyo itaonyesha dhahiri kwamba hauna utayari wa kumsikiliza mtu huyo, na kufanya mawasiliano yenu kuwa magumu kwa siku zinazofuata.
Kuwa na muonekano wa tofauti katika shughuli zako. Pokea simu unazopigiwa, jibu barua pepe unazotumiwa na fanya kazi zako kwa wakati. Utaheshimika na jaribu kujenga mahusiano mazuri na baada ya muda nao watakuwa wema kwako.
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa mashirika ya habari.
Tukutane Alhamisi ijayo.

Twitter Facebook