Friday, August 28, 2009

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI (4)

NAWAKARIBISHA tena katika safu hii ya Maisha Yetu yenye lengo la kukufahamisha jinsi maisha yalivyo na yanavyopaswa kuwa.

Leo tunaendelea na mada yetu ya msongo katika maeneo ya kazi ili uweze kujua jinsi ya kukabiliana na hali hiyo mara unapokutana nayo.

Watafiti mbalimbali wamegundua kuwa, endapo bosi katika kampuni, atakuwa na hali ya msongo wa mawazo, ofisi, kampuni au shirika hilo litakuwa na mawasiliano mabaya.

Naye mwanasaikolojia mmoja anayeshughulika na masuala ya viwandani amewahi kuelezea jinsi meneja mzuri anavyopaswa kuwa.

Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, meneja mzuri anapaswa kuwa mshauri mzuri kwa wafanyakazi wake, ari ya kupenda kujituma, kupenda kufanya kazi na kushirikishana mambo mbalimbali na wafanyakazi wake.

Kwa maelezo ya mwanasaikolojia huyo, endapo bosi atakuwa karibu na wafanyakazi wake, ushauri mwingi utakaotoka kwa wafanyakazi hao, utampa mwanga wa kujua nini cha kufanya kwa kipindi hicho katika kuboresha ofisi.

Ndiyo maana katika ofisi nyingi ni rahisi kutambua sababu za meneja fulani kuwa mzuri, au wa kawaida ama mbaya katika utendaji wake, kutokana na jinsi anavyojishughulisha na watu wake.

Meneja mzuri ni yule anayependa kuwa karibu na wafanyakazi wake, kuwasikiliza na kufuatilia uzalishaji unavyokwenda katika kampuni.

Pia anakuwa mwadilifu katika utendaji wake, hatetereki katika malengo yake ya uzalishaji, pia huwasikiliza wafanyakazi wake wanapokuwa na mahitaji.

Bosi wa wastani katika utendaji wake, ni yule anayeangalia ufanisi wake pekee, bila kuona umuhimu wa wengine. Kama vile wanavyowajibika katika kazi zao.

Kwa upande wa bosi mbaya ni yule anayefanya kazi kwa kutumia vitabu, pamoja na kujenga hali ya kujilinda kila wakati.

Utafiti mwingine uliofanywa, ulionyesha kuwa, msongo katika kazi unawafanya watu wengi kutumia vileo na kujikuta wanashindwa kufikia malengo katika kazi zao, hali inayowafanya kufukuzwa kazi.

Wengine wanaokabiliwa na msongo, hutumia dawa za kulevya, hali inayowafanya kupatwa na magonjwa ya akili, kuathiri utendaji wao katika uzalishaji na kuhatarisha ajira walizonazo.

Utafiti mwingine unaonyesha kuwa, msongo mwingine kwa wafanyakazi huchangiwa na uamuzi unaofanywa na kampuni kwa kuwapunguza kazini wafanyakazi kutokana na sababu mbalimbali.

Hivyo basi, ni vyema kwa mameneja katika ofisi zao kuzungumza na kuwasikiliza wafanyakazi wao.

Pia wawe wanawauliza wafanyakazi hao kuchanganua mambo matatu yanayoweza kuboresha kampuni au ofisi hiyo na mambo matatu yatakayoweza kuzorotesha uzalishaji katika kampuni hiyo.

Bosi huyo apende kujua kama mazingira wanayofanyia kazi wafanyakazi wake, yanaridhisha.

Ni vema bosi kuwaheshimu watu aliowaajiri ama anaowasimamia katika kampuni hiyo na kuwajulisha kuwa yuko tayari kushughulikia taarifa yoyote itakayomfikia.

Ni vema wafanyakazi wakawa wanashirikishwa katika maamuzi yanayofanyika ili wajione nao ni sehemu ya ofisi hiyo.

Si mbaya wakaorodhesha matatizo mbalimbali yaliyowapata wafanyakazi na kuangalia jinsi ya kuyashughulikia.

Ni vizuri kiongozi huyo akawa anaongoza kwa vitendo. Asiwe mwepesi wa kuzungumza.

Hayo yote yatakapoweza kutekelezwa na mameneja ama waajiri wa kampuni, msongo katika eneo hilo la kazi hautawapata wafanyakazi wake.

Ugonjwa mbaya katika kampuni ni ile hali ya wafanyakazi kukosa ari ya kufanya kazi kutokana na msongo wanaokabiliana nao.

Hiyo ni pamoja na kupunguza ari ya kupenda kazi kwa wafanyakazi, utendaji mbovu na unaopunguza uzalishaji, kuongezeka kwa magonjwa miongoni mwa wafanyakazi, wafanyakazi kuchelewa kazini hali inayosababisha kampuni hiyo kutokufikia malengo iliyokusudia.

Vile vile baada ya kampuni kupunguza wafanyakazi, wale wanaobakia nao wanaendelea kupatwa na hali hiyo ya msongo kwa kuwa, kunakuwa na ongezeko kubwa la kazi hali itakayowafanya washindwe kupata muda wa kupumzika.

Tukutane alhamisi ijayo

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI (3)

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika siku nyingine ambayo Mwenyezi Mungu ametujalia kuiona.

Leo tutaendelea kuangalia mada kuhusu msongo katika sehemu za kazi.

Wengi wetu tumekuwa tukikabiliana na hali ya msongo katika vipindi mbalimbali vya maisha, kuanzia kipindi cha utoto hadi uzee.

Hali hiyo humpata mtu anayefanya kazi, mzazi katika kipindi cha kulea watoto wake na katika vipindi mbalimbali vya maisha.

Ila humjia kila mmoja kwa jinsi yake.

Mafanikio yetu katika maisha na thamani ya maisha, inategemea ni jinsi gani tunavyokabiliana na hali hiyo.

Tunahitaji kuelewa msongo ni kitu gani na kujifunza jinsi ya kukabiliana na hali hiyo.

Mtaalamu mmoja aliwahi kuelezea fani saba ambazo haziepukiki katika suala la msongo, ambazo ni fani ya ualimu, uuguzi, umeneja, ustawi wa jamii, udereva, upolisi na ofisa magereza.

Je, umejiona katika kundi lolote hapo juu? Usijali kuhusu hilo, cha msingi ni kujua unafanya nini na jinsi gani ya kujiepusha na msongo katika kazi yako.

Pia inawezekana wewe ni miongoni mwa watu zaidi ya 200,000 ambao hupatwa na maradhi yanayotokana na hali ya msongo katika kazi zao, kila mwezi na kulazimika kupumzika nyumbani ili kuondoa hali hiyo.

Pia yawezekana kwamba, wewe ni miongoni mwa asilimia 27 ya watu wanaolalamikia mazingira ya kazi zao, ama kati ya asilimia 19 ambao hawana mazingira bora ya kufanyia kazi, au asilimia 17 ya wale ambao ofisi zao haziko katika muundo wa kisasa hivyo kufanya kazi zao kuwa ngumu, kwa kuwa hakuna mwanga au hewa ya kutosha.

Pia yawezekana umo miongoni mwa asilimia 14 ya wale wafanyakazi ambao hawana nafasi ya kutosha ya kukutana na wenzao, kutokana na kazi kuwa nyingi, asilimia 13 ya wale ambao hawajaridhika na eneo ambalo ofisi yao ipo, asilimia 12 ya wale wasio na vifaa vya kisasa ofisini kwao, asilimia 5 ya wale wanaolalamika kuhusu kukosa uhuru wa kuvuta sigara ama mazingira wanayofanyia kazi hayana uhuru wa kumfanya avute sigara na asilimia nne wanakosa ushirikiano na wafanyakazi wengine.

Je, hofu kuhusu kazi yako inaongezeka bila kupata suluhu? Uamuzi wako wa mwisho ni kubadili kazi na kuchukua tahadhari kwa hatari unazoweza kukabiliana nazo katika kazi hiyo mpya.

Lakini lazima uchukue tahadhari, kwa sababu ni gharama.

Pia utaona kuwa, mpangilio mbaya wa kazi zako unaweza kukusababishia maradhi.

Utawala mzuri huwafanya wafanyakazi kuwa na afya bora, hivyo uzalishaji unakuwa mzuri pia.

Utafiti mwingine uliofanywa kwa wafanyakazi 600, asilimia 60 kati ya hao wamewalalamikia watengenezaji wa barabara kuwa wanachangia msongo katika maisha yao, kutokana na kusababisha foleni wawapo barabarani, asilimia 40 wamesema kuwa, malengo waliyojiwekea hawajaweza kuyafikia hivyo yanawasababishia hali hiyo.

Wengine walisema kuwa, hali ya hofu na wasiwasi wanayoipata wanasababishiwa na rafiki zao, ama kutoelewana kwa wafanyakazi ndani ya ofisi.

Pia katika ofisi nyingi, suala la mapumziko limekuwa ni kitendawili, wafanyakazi hawapati mapumziko wawapo kazini, hali inayosababisha hofu, wasiwasi na hasira za mara kwa mara.

Ni wafanyakazi wachache wanaoweza kupata muda wa mapumziko na kwenda kupata chakula cha mchana, wengine kutokana na muda kuwa mdogo kwa ajili ya kazi nyingi hujikuta wakipitisha mchana bila kula chakula.

Vile vile haijalishi wewe ni nani, unaweza kukabiliwa na msongo katika mazingira ya ofisi.

Tuangalie mfano wa sekretari, ambao wamekuwa wakisumbuliwa na hali ya hofu na wasiwasi katika kazi zao.

Hivyo msongo mkubwa huwakabili kutokana na kazi zao za kila siku wanazozifanya.

Sekretari hupatwa na msongo pale anapokuwa ana kazi nyingi mara simu inaita au wageni wanafika na kuuliza habari mbalimbali zinazomhusu bosi wake, ilhali kipindi hicho anahangaika akamilishe kazi ya bosi wake anayoisubiri ili aanze kikao.

Vile vile hupatwa na msongo pale mashine yake ya kutolea ‘photocopy’ inapokwamisha karatasi au kukwama ama inaposhindwa kufanya kazi kwa kipindi hicho anachohitaji kuitumia huku akiwa anakabiliwa na kazi nyingine.

Wakati huo huo, kunakuwapo na watu wanaosubiri kuweka ahadi ya kuongea na bosi wake, ambao hawako kwenye ratiba ya siku hiyo.

Vile vile hukabiliwa na msongo pale anapopata kazi nyingine ya dharura ilhali alishajiandaa kwenda nyumbani.

Mbali na hali ya msongo wa kawaida, wanayokabiliana nayo katika shughuli zao za kiofisi, kwa upande mwingine hulalamika kupewa kazi za dharura na mabosi wao, wakati hakuna posho.

Wanapewa kazi zinazopoteza nguvu zao na kuwafanya washindwe kuwasiliana na watu wengine, pia wapo wanaolalamikia masuala ya ngono.

Hayo yote yanajumuisha mazingira mabovu ya ofisi, muundo mbaya wa viti vya ofisi ambavyo havimpi starehe mtumiaji na badala yake vinamfanya achoke na kuchukia mazingira ya ofisi anayofanyia kazi.

Hivyo unapoona una dalili ya kuchoka, ama kuumwa mara kwa mara, ni vema kuangalia afya yako ilhali isiwe mbaya zaidi.

Utafiti uliofanywa katika nchi za wenzetu mwaka 2003, ulibaini kuwa, asilimia 35 ya mabosi wamekuwa wakikubali majukumu mbalimbali ya ofisi zao ili kuwafanya wafanyakazi wao, wasipate msongo ama kupunguza hali hiyo kabisa.

Tukutane wiki ijayo

MSONGO KATIKA SEHEMU ZA KAZI

KWA mara nyingine nawakaribisha tena katika safu hii ya Maisha Yetu, inayokujia kila Alhamisi, lengo likiwa ni kuelimisha.

Wiki iliyopita tulizungumzia kuhusu msongo katika maeneo ya kazi, tuliona sababu zinazosababisha mtu kupatwa na msongo katika eneo la kazi ni hofu, ongezeko la muda wa kazi, ilhali masilahi ni madogo na msisitizo wa kuongeza uzalishaji kazini wakati hakuna ongezeko la marupurupu yoyote.

Leo ni mwendelezo wa makala ile na tutaangalia jinsi ya kuondoa hali hiyo, ambayo kwanza inakubidi ujijali wewe mwenyewe.

Wakati msongo katika kazi yako unaingilia uwezo wako wa kufanya kazi, ni vema kujijali wewe mwenyewe, au kusimamia maisha yako mwenyewe, ni wakati wa kuchukua hatua.

Wakati unapodhamiria kujali mahitaji yako, unakuwa na nguvu ya kushinda hali hiyo ya msongo.

Vile vile unavyojihisi, unavyoweza kujizatiti, ndipo utakapoweza kusimamia kazi yako bila kuendelea kujisababishia msongo mwingine.

Kujijali mwenyewe hakujalishi maisha uliyonayo kama ni ya kifahari au la. Hata katika kufanya vitu vidogo vidogo vinaweza kuinua tena hali yako ya kuvunjika moyo na kukata tamaa, vitu hivyo vinaweza kukuongezea nguvu.

Fanya kitu kimoja kwa wakati na kufanya vile ulivyoamua maisha yako yawe, hapo utagundua kuwa kuna tofauti katika hali ile ya msongo uliyokuwa nayo, nyumbani hata kazini kwako.

Vile vile unaweza kuondoa hali hiyo kwa kuangalia picha mbalimbali. Kwa kufanya hivyo kunaweza kuinua tena hisia zako, kukuongezea nguvu, kukufanya uwe na matarajio ya baadaye na kutuliza akili na mwili wako.

Kwa kiasi kikubwa utaondoa hali iliyokuwa inakutesa. Pia kutengeneza chakula unachokipenda kutakufanya ujisikie vizuri.

Unapopangilia mlo wako, hata kama ni kidogo kutakufanya upate nguvu katika mwili wako na kujisikia vizuri.

Ili kuondokana na hali hiyo ni vema, kulala usingizi wa kutosha. Kwani hali hiyo inakufanya ukose usingizi.

Lakini hali ya kukosa usingizi, inaweza kukusababishia ukapatwa na maradhi mengine.

Unapolala na kukosa usingizi, hali hiyo inakuweka katika hatari ya kuwa na msongo zaidi. Lakini wakati unapokuwa umepata mapumziko mazuri, inakuwa ni rahisi kukabiliana na hali hiyo ya msongo.

Pia unaweza kuondoa hali hiyo kwa kutoa vipaumbele na kuwa na mpangilio katika kazi zako.

Wakati unazungukwa na hali ya msongo katika kazi na eneo lako la kazi, unaweza kukabiliana na hali hiyo kwa kuamua kuikubali hali hiyo ngumu inayokutesa na kujitahidi kukamilisha kazi zako kwa wakati.

Jitahidi kujitawala katika kazi zako wewe mwenyewe bila kusaidiwa na mtu, pamoja na kujenga mahusiano bora katika kazi.

Haya ni baadhi ya mapendekezo katika kupunguza hali hiyo kwa kutoa vipaumbele na kuwa na mpangilio katika majukumu yako.

Baadhi ya mambo yanayoweza kukuondolea hali hiyo

Ni vema kutengeneza ratiba. Changanua utaratibu wako wa kufanya kazi, majukumu, na shughuli za kila siku.

Kamwe usivuruge utaratibu uliojiwekea kwa kazi isiyokuwepo. Jaribu kutafuta uangalifu kati ya kazi, maisha ya familia, shughuli za kijamii na mambo binafsi na majukumu ya kila siku.

Kamwe usijiwekee ratiba zilizo nje ya uwezo wako. Epuka kuwa na ratiba ya mrundikano wa kazi katika siku moja.

Unapokuwa na ratiba ya kazi nyingi kwa siku moja, mara nyingi kazi hizo hufanywa chini ya viwango.

Ondoa kazi zile ambazo hazina umuhimu kwa siku hiyo katika ratiba yako.

Jaribu kuondoka mapema muda wa asubuhi. Dakika moja mpaka 15; zinaweza kufanya tofauti kwa kuweza kukamilisha kazi zako vizuri kwa siku hiyo na kukurahisishia utendaji wako wa siku hiyo.

Kamwe usijiongezee kiwango cha msongo unaokukabili kwa kuendelea kuchelewa ofisini.

Ni vema kuwa na ratiba ya kupumzika. Hakikisha unakuwa na muda mfupi wa kupumzika kwa ajili ya kuisafisha akili yako.

Pia ni vema kwenda mbali na meza yako unayofanyia kazi kwa ajili ya kupata chakula.

Na kwa kufanya hivyo kunaongeza ari yako ya kufanya kazi, kinyume cha hapo kutakufanya uwe na uzalishaji mdogo.

Mambo yanayoweza kukuondolea msongo katika kazi yako endapo wewe ndiyo mmiliki mkuu, ama mkurugenzi ni pale, unapotoa kipaumbele kwa kazi zilizopo.

Andika ratiba ya kazi unazoweza kuzifanya na uzifanye kulingana na umuhimu wake. Anza na kazi ile yenye umuhimu. Na kama una jambo la muhimu, ni vema kuamka mapema.

Kwa kuamka mapema, shughuli nyingine za siku hiyo zitakuwa na matokeo mazuri.

Ni vema kukabidhi majukumu yako kwa wengine. Huwezi kufanya kazi zote wewe mwenyewe, iwe nyumbani, shuleni au kazini.

Kama wapo watu wengine wanaoweza kufanya kazi hiyo, ni vema ukawashirikisha.

Hali hiyo itakupunguzia kuwa na msongo usio na lazima.

ONYESHA UPENDO KWA RAFIKI, FAMILIA

KARIBUNI wapenzi wasomaji katika safu hii ya Maisha Yetu. Leo tunaangalia jinsi unavyoweza kuonyesha zawadi ya upendo kwa watu, hata kama huna fedha.

Kila mtu anapenda kupendwa, hivyo yakupasa kuwa na rafiki wa karibu atakayekushirikisha katika mambo mbalimbali anayokabiliana nayo. Kutokana na ukweli huo ni vema kuwa na rafiki mzuri na kuonyesha upendo wako kwake, kwa sababu wakati mwingine unajikuta hata familia yako inakuwa mbali nawe, ilhali katika kipindi hicho unahitaji mtu wa kuongea naye.

Ni muhimu kuwa rafiki mzuri kwa sababu unajifunza ni jinsi gani ya kukutana na watu wapya na unajifunza kutokana na makosa yako. Tafuta watu unaopenda wawe rafiki zako, kwa kujitambulisha na kumwacha mwingine kukueleza juu ya mambo anayoyapendelea.

Mwonyeshe mtu huyo kuwa unamwamini, mwache ajue kuwa ni sawa kupendana, mwache ajue kuwa uko pale kwa ajili yake na atakuwa rafiki yako wa kudumu. Mara zote mfanye atabasamu hata kama ana huzuni. Pia mwache ajue kuwa upo tayari kusikiliza chochote atakachosema.

Je? unawezaje kuonyesha upendo bila kutumia fedha? Wakati mwingine tunajitahidi kwa bidii kutafuta zawadi ambayo ni sahihi tunayofikiria kuwa ina maana kwa yule unayempelekea.

Au tunaishikilia zawadi hiyo tukifikiria kama kuna sababu maalumu ya kutoa zawadi hiyo. Ninakutia moyo kutoa zawadi yako kwa uhuru na iwe ni mara kwa mara, kumbuka kuwa utoaji ni shughuli inayomnufaisha mtu kila mara anapofanya hivyo.

Tuangalie zawadi 10 zinazofaa kwa siku ya kawaida na maalumu. Pia, ni zawadi ambazo mtu yeyote anaweza kutoa kwa sababu halazimishwi ila ni kwa nia ya kuleta ushirikiano.

Zawadi ya kwanza ni muda. Kumbuka kuutoa muda wako na kushirikiana na wenzako ni moja ya zawadi kubwa unayoweza kuitoa. Kama unatoa dakika 10 kwa kupiga hadithi na mtoto wako, kupata chakula cha mchana na rafiki yako au kutumia muda wa mchana kwa shughuli za nyumbani, shambani au nyinginezo, ukiwa na mume au mke wako, unajitolea nafsi yako na kujenga uhusiano mzuri kwa muda huo.

Zawadi nyingine ni kukiri kwa uaminifu. Tumekuwa tukisikia watu wachache wakisema kuwa wamepokea shukrani nyingi au pongezi nyingi.

Wote tunajisikia vizuri wakati tunapata taarifa nzuri na shukrani kwa vile tulivyo au tunayoyafanya.

Anza kuzingatia kuimarika katika hilo na kutoa sifa nzuri kwa wengine na kujenga tabia ya kukiri jambo zuri linalofanywa na wengine kwa kile unachokiona.

Nyingine ni msamaha. Hii ni zawadi nzuri mno yenye nguvu. Wakati tunasamehe wengine, tunaacha kuwaadhibu, tunawaruhusu wajisikie hatia au kuona aibu ili waweze kugundua makosa yao. Msamaha pia ni zawadi ya kutuweka huru kutoka kwenye uzoefu ulioupata wakati ulipoumizwa moyo wako au maumivu katika matukio yaliyopita.

Vile vile upendo. Wakati unapotaka kuuonyesha upendo wako kwa wengine, usiwahukumu wengine, na uwaone kama ni watu wa muhimu kwako. Tunaposhiriki kwa uwazi upendo wetu na wengine inasaidia kuponya majeraha, kujenga uhusiano mzuri na kumsaidia mtu katika kupitia changamoto za maisha pia kuwa na maisha mapya ya uhakika.

Usiugawe usikivu wako. Ingawa tunatoa muda wetu kwa ajili ya wengine, akili zetu zinaweza kuwa popote kutokana na uzoefu. Jiruhusu nafsi yako kuwa kwa mtu mwingine, kupanga naye shughuli nyingine, mawazo au ajenda mpaka utakapofikia malengo yako uliyokusudia.

Kama utafanya hivyo, watu watakuona unastahili kupata asilimia zote, kwa usikivu wako na kwa upande mwingine inawezekana ukawa hujafikia kiwango hicho ila kutokana na hali hiyo uliyojiwekea kwa watu.

Heshima. Mara kwa mara tunakuwa na shughuli nyingi au tunajishughulisha sana katika maisha yetu ambayo yamekuwa na matukio mfululizo ya kuvutia, tunasahau kama kuna watu wengine wanaotuzunguka. Iache nafsi yako ipumue na kutoa heshima kwa watu unaokutana nao kila siku.

Yapo mambo madogo madogo yanayoweza kufungua milango kwa watu wengine kuthamini mambo unayowafanyia kama kumpa lifti kwenye gari yako, kumbebea gazeti lake mpaka mlangoni pake au kusimamisha gari lako mbele ya mtu unayemfahamu na kumpa lifti kipindi cha msongamano wa abiria kituoni.

Mambo yote hayo yataonyesha hali ya kujali kwa mtu ingawa wakati mwingine mtu hawezi kuelewa wema wako na kukushukuru. Shitukiza. Zawadi za aina hii zinamfanya mtu kuwa mbunifu wa hali ya juu. Je, unataka kumpa dada yako kadi inayosema unampenda? Unajisikiaje unapomtumia mumeo maua?

Je, ni kweli utamshitusha? Au labda umechagua kujitolea kumpa mfanyakazi mwenzako kigari cha kusukuma cha watoto ili aweze kufurahia jioni anapokuwa matembezi na rafiki zake?

Zawadi kama hizo zinakuwa tukio kubwa kwa yule unayempelekea katika siku yake ya kawaida kwa sababu hakutarajia kufanyiwa jambo kama hilo kwa siku hiyo.

Shukrani ni zawadi pekee kwa yule unayempa, kwani inasababisha mtu huyo kujua kuwa umekuwa makini kwa lile alilokufanyia. Kama ukiri wa dhati, na neno jingine ni kusema asante, linaonekana ni jambo ambalo si la kawaida.

Endapo utachagua kusema au kuandika shukrani zako, hii ni zawadi inayokwenda ndani ya moyo wa mpewa shukrani. Tabasamu katika dunia ya kisasa, mara nyingi tunaona tabasamu chache na nyuso zenye furaha ya kweli.

Tabasamu linajulisha moyo mkunjufu, mapokezi na urafiki. Pia inafanya kuonekana kwa urahisi kwa wote wenye nyuso za tabasamu. Iache zawadi hii ya tabasamu itoe ujumbe. Mfano “Nina furaha uko hapa.”

Maombi ya kimya kimya. Wote tunakuwa na maombi ya ziada na ya baraka katika maisha yetu. Hata kama hufahamu, mtu mwingine anaweza kukubariki wakati unampa zawadi ya maombi yenye nguvu.

Kama unajua au la, mazingira ya mtu au dini yake, unaweza kuuliza kwa msaada au usikivu. Maombi rahisi unaweza kumwombea kwa kutumia “Mungu, ninakuomba umbariki mtu huyu na ukutane na mahitaji yake yoyote ambayo anayo katika maisha yake, asante.”

Tukutane wiki alhamisi ijayo.

JIFUNZE KUSHUKURU

KARIBUNI wapenzi wasomaji wetu katika safu hii ya Maisha Yetu inayokujia kila alhamisi. Leo tutaangalia jinsi ya kutoa shukrani. Kila siku ni njema ya kukuwezesha wewe kutoa shukrani kwa vitu vyote ulivyonavyo katika maisha yako.

Kuna baadhi ya watu, wamekuwa wakifikiri ni jambo gani la kuweza kulitolea shukrani. Wengi wenu wanaweza wakawa wamepoteza kazi au nyumba zao. Pengine umekabiliana na changamoto katika afya yako au uhusiano wako.

Bila kujali hali uliyo nayo, ni vema ukawa mtu wa kushukuru kwa kuwa Mungu kwani ndiye anayejua mambo mema anayokuwazia kila siku.

Kamwe sijawahi kukutana na yeyote ambaye hana kitu chochote cha kumfanya ashukuru.

Inapokuwa unahisi kuwa huna jambo lolote la kulitolea shukrani, unakuwa unakosea kwa sababu ulimwengu hauwezi kukupa zaidi ya kile ulichonacho.

Kinachotakiwa ni kushukuru na kuonyesha unajali kwa kile ulicho nacho.

Kama wewe ni mmoja wa watu wanaohisi kuwa hawana jambo lolote la kushukuru, ngoja nikupe maelekezo machache.

Je, umeamka asubuhi hii ya leo? Yakupasa utoe shukrani kwa zawadi ya siku inayofuata, nafasi nyingine ya kuanza upya na kutembea.

Unasoma maneno haya muda huu? Hivyo utoe shukrani kwa zawadi ya kuona, uwezo wa kusoma na kuelewa.

Kwa zawadi hii utapata ujuzi wote unaohitaji wa kubadilisha hali uliyonayo kwa mambo mazuri. Unajua idadi ya mchanga unaokuzunguka? Hivyo, toa shukrani kwa zawadi hiyo. Kama unaweza kusikia vicheko vya watoto, kusikia sauti za ndege juu ya miti na kusikia wimbo uupendao katika redio, hiyo ni zawadi tosha.

Bila kujali kwamba jambo hilo ni dogo kiasi gani au kuliona kuwa halina umuhimu, toa shukrani kwa hilo. Wakati unafanya hivyo, utaanza kuwa na mabadiliko mazuri katika mwili na hisia zako. Pale unapotoa shukrani na kuonyesha unajali kwa kile ulichonacho katika maisha yako, ndivyo watu wengi zaidi watakavyokushukuru.

Utakaposhukuriwa na watu wengi zaidi, ndivyo utakavyojisikia vizuri na ndivyo utakavyoongeza jitihada kwa kila kinachokuzunguka. Hivyo ni jambo gani unalopaswa kushukuru? Vile vile katika suala hili la kushukuru ni vema likifanywa na waajiri pamoja na waajiriwa, kwa kuwa huleta hamasa kwa kila mmoja.

Unaweza kuwaambia washirika wako, wafanyakazi na waajiri ni jinsi gani unawathamini na mchango wao wa kila siku. Ni ukweli usiopingika kuwa neno la shukrani lina maana kubwa sana kwa mtu yeyote kuliko zawadi.

Pia shukrani huwafanya watu katika kazi zao kipindi chote cha mwaka kujiona kuwa ni wathamani kubwa, kuliko kubaki kuwasema na kuwanenaa mabaya.

Zifuatazo ni njia ambazo zinaonyesha shukrani kwa wafanyakazi na waajiri.

Ni vema kupongeza kitu chochote ambacho wafanyakazi wako wamekifanya vizuri. Elezea kwa ufasaha kile hasa kilichokufurahisha.

Sema asante. Onyesha shukrani kwa kazi wanayoifanya na michango yao. Mahusiano mazuri katika kazi yanajenga heshima, nidhamu na utukufu kwa kila mmoja.

Penda kuulizia habari zinazohusu familia za wafanyakazi wako, vitu wanavyopendelea na matukio maalumu wanayopenda kuhudhuria.

Pia waeleze kile unachokipenda, mambo hayo huwafanya watu wajisikie wanathamani na wanajaliwa.

Toa mapumziko kwa wafanyakazi wako katika siku za sikukuu, kama upo uwezekano. Kama kwa siku hiyo haitawezekana tafuta siku nyingine utayowapa wafanyakazi wako mapumziko.

Jitahidi kufahamu mambo ambayo wafanyakazi wako wanayapenda, ili uweze kutoa zawadi siku za sikukuu. Kutoa zawadi kama kuonyesha shukrani na kutambua uthamani yao, kunainua ari ya wafanyakazi wako siku hadi siku tofauti na kuonyesha kutowajali.

Pia kama unaweza kutoa pesa kwa wafanyakazi wako, kama vile mwisho wa mwaka kutoa bonasi pamoja na cheti cha kuonyesha kuwa unajali kuwapo kwao.

Kila mmoja anafurahia chakula. Hivyo wakaribishe chakula cha mchana wafanyakazi wako katika sikukuu za kuzaliwa au matukio muhimu katika mwaka au bila kuwepo kwa sababu yoyote ile.

Pia unaweza kuwa mbunifu wa vitu mbalimbali katika ofisi yako ili mradi kuwe na mawasiliano mazuri kati ya bosi na wafanyakazi wake. Pia unaweza kuwapa wafanyakazi wako zawadi za bagia, donate au vitu vingine kama hivyo. Kutoa zawadi kama hizo ambazo umezipika nyumbani kwako ni zawadi kubwa.

Pia unaweza kutoa nafasi, watu wanataka nafasi kwa ajili ya mafunzo zaidi. Wanapenda kushiriki vitu mbalimbali wanavyovipendelea vinavyoweza kuwasaidia katika kazi zao.

Vitu kama hivi huongeza umoja, ushirikiano pamoja na uzalishaji katika kampuni au shirika lako.

Twitter Facebook