Wednesday, December 12, 2012

Jinsi ya kuepuka kupata hasara


BIASHARA yako inapokwenda mrama, ni vema kuweka tamko la kusitisha hasara uliyoipata, kwamba hauko tayari kukubali iendelee.

Jitahidi kuweka mikakati zaidi ya kuiboresha na kuomba ushauri wa kimaendeleo kwa waliofanikiwa.

Tumwangalie mfanyabiashara John Robert, aliyekuwa amepewa fedha na rafiki zake kiasi cha dola 200,000 za Kimarekani, ili kuwekeza katika soko la hisa.

Baada ya kupewa fedha hizo na kuzifanyia biashara, Robert alifikiri kuwa angepata faida ambayo ingemfanya awe na maendeleo zaidi katika maisha yake, lakini kwa bahati mbaya ilikuwa kinyume na matarajio yake.

Awali, alipoanza biashara hiyo alipata faida iliyomfanya asiwe mbunifu katika biashara yake, lakini matokeo yake ni kwamba baada ya muda mfupi alifilisika.

Baada ya kufilisika, alipata hofu kutokana na fedha alizopewa kwa ajili ya kufanya biashara.

“Sikujali kupoteza pesa zangu mwenyewe,” anasema mfanyabiashara huyo na kwamba kipindi hicho kilikuwa kigumu kwake, kutokana na kupoteza pesa za rafiki zake.

Lakini, mara baada ya kufanikiwa kuishinda hofu iliyokuwa ikimkabili, alijikuta amepata ujasiri mpya na kwenda kuwakabili tena rafiki zake na kuwaeleza kilichomsibu.

Pamoja na maelezo hayo, marafiki wale hawakuonesha mshangao katika jambo hilo, bali walilichukulia kuwa la kawaida.

Lakini kwa upande wake ilionekana kuwa halitatibika.

“Nilijua nilikuwa nafanya biashara katika mtindo wa 'pata potea' nikitarajia zaidi bahati na mawazo ya watu. Nilikuwa nikishiriki katika soko la hisa kwa kusikia,” anasema.

Kwa maelezo ya Robert, alianza kufikiria makosa yake na kufanya uamuzi kabla ya kuamua kurudi kwenye soko kwa mara nyingine, alijaribu kutafuta chanzo cha jambo hilo, pia alifikiri na kuamua kuja na mwongozo mpya wa mafanikio.

Baada ya hali hiyo kumtokea, alitafuta ushauri kutoka kwa rafiki zake, kwa kuwauliza ni jinsi gani wameweza kufanikiwa na kuendesha biashara zao, ambazo zinakwenda vizuri.

Mmoja wa marafiki zake, aliyeendesha biashara yake vizuri, alimweleza akiweka tamko la kusitisha hasara katika hofu yake kwenye majukumu aliyojipangia.

Hivyo, mtu yeyote anaweza kuondoa tabia ya hofu aliyonayo. Hivyo popote unaposhawishika kuweka pesa zako baada ya kupoteza, ni vizuri kutulia na kujiuliza maswali yafuatayo: Ni kwa kiasi gani umekuwa na hofu kuhusu jambo fulani juu yako? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika hofu inayokukabili na kusahau? Ni kwa jinsi gani utaepuka kupata hasara katika wasiwasi na kusahau?

Kumbuka unapoanza kuwa na hofu ya vitu vilivyopita na kufanyika ni kama unakuwa ukijaribu kupanda mazao yako kwenye vumbi.

Maana yake ni kwamba yale yaliyopita usiyasumbukie, bali ugange yajayo. Ukiendelea kuyasumbukia utajisababishia mikunjo katika paji la uso wako na vidonda vya tumbo.

Hivyo, endapo una tatizo la kukumbuka mambo yaliyopita, iambie nafsi yako kwamba huishi kwa ajili ya mambo hayo. Badala yake unaweza kuwa na mipango mizuri zaidi kwa ajili ya maisha yako.

Unaweza kujishughulisha kwa kuandaa mashindano mbalimbali kama vile muziki, ngumi au uchoraji.

Lengo ni kuwa unajishughulisha kila mara ili usiwe na nafasi ya kufikiria mambo yaliyopita, ambayo yamekusababishia hasara na hofu maishani mwako.

Kwa nini wajasiriamali hukopa, hawafanikiwi? - 3


WIKI mbili zilizopita nilizungumzia kwanini wajasiriamali wengi na wafanyabiashara wa kati licha ya kukopa kwenye taasisi za fedha wanashindwa kufikia malengo waliyojiwekea.

Baadhi ya wajasiriamali hao walitoa sababu katika safu hii ya Maisha Yetu inayowafanya wasisonge mbele katika shughuli wanazozifanya.

Pamoja na sababu hizo zilizotolewa, bado elimu kwa wajasiriamali hao inahitajika kwa kiasi kikubwa. Inatakiwa wapate elimu kuhusu biashara wanazozifanya na kwamba endapo watapeta fedha wanatakiwa kuzitumia vipi.

Ukweli ni kwamba kumpa mjasiriamali fedha tu, hapo unakuwa hujamsaidia. Cha msingi ni kumpa fedha hiyo pamoja na elimu ya jinsi ya kuboresha biashara anayoifanya.

Wapo wajasiriamali waliofanikiwa kutokana na nidhamu ya fedha wanayoipata ikiwemo pia elimu kuhusu shughuli anayoifanya.

Ni vema basi, taasisi za fedha zinazokopesha wajasiriamali wakaliangalia suala hilo ili mjasiriamali huyu aweze kupiga hatua.

Mfano unapompa mjasiriamali elimu ya jinsi ya kutengeneza batiki, anapomaliza anajua kuwa anahitajika kununua vitambaa, rangi na dawa kwa ajili ya kutengenezea batiki hizo, anapotengeneza akichanganya na ubunifu wake anakuwa na mafanikio makubwa.

Pia ukiangalia soko la batiki lipo ndani na nje ya nchi. Mbali na elimu pia mjasiriamali huyu anapaswa kuunganishwa kwenye mtandao wa wajasiriamali wa ndani na nje ya nchi. ili apate soko ndani na nje pia asiwe muuzaji wa hapa hapa.

Kumuunganisha mjasiriamali na mitandao mingine ya ujasiriamali kunatoa fursa ya mjasiriamali huyo kujifunza kutoka kwa wengine na kujua katika biashara yake hiyo aongeze ama apunguze nini.

Hivyo basi mbali na kutoa mikopo yenye riba kubwa, yenye usumbufu, inayomfanya mjasiriamali huyu kuzunguka anapoupata soli ya viatu inakuwa imekwisha, ni vema akapewa elimu hiyo.

Naamini penye nia pana njia, shime wajasiriamali msikate tamaa katika kufikia mafanikio mnayoyatarajia, ama maono yale mliyonayo juu ya mafanikio katika maisha yetu.

Miongoni wa wajasiriamali walitoa maoni yao ni Alexander kutoka Dar es Salaam ambaye anasema tatizo kubwa kabisa ni wajasiriamali wengi wanakuwa hawana ndoto ya kufanya wanachotaka, hivyo wanapokopeshwa fedha hizo hushindwa kuendelea.

Mjasiriamali huyo aliyejitambulisha kwa jina moja anasema matokeo yake wajasiriamali hujikuta wakitanga tanga katika biashara nyingi kwa kuwa hawakujua wanataka kufanya nini.

Msomaji mwingine kutoka Mwanza ambaye hakujitambulisha jina lake alisema kuwa, taasisi nyingi za fedha ama benki zimekuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.

Anasema amekutana na adha ya kusotea mkopo japokuwa amekwisha kamilisha taratibu zote zinazohitajika katika benki aliyoiombea mkopo ikiwemo hati ya nyumba, huu ni mwezi wa pili anazungushwazungushwa na kila akiulizia anaambiwa ripoti imetumwa Dar es Salaam, hivyo kumfanya kushindwa kutimiza malengo aliyojiwekea.

Andondile Anjawe kutoka Ludewa, anasema katika mambo yanayoumiza wajasiriamali kwenye mikopo na kutolea mfano wa benki aliyoomba mkopo, ni zile gharama mbalimbali zinazotozwa kabla ya kupata mkopo husika.

Anasema unalipia gharama ya mkopo, pili unalipia mhuri, tatu unalipia mahakamani, hivyo unajikuta mkopo wote unamalizika kabla hujaushika mkononi.

Hapo hapo bado unatakiwa kurudisha mkopo huo mwezi unaofuata baada ya kuupata.

Maoni mengine yaliyotolewa na mjasiriamali ambaye hakutaja jina lake anasema wengi wana sifa za kukopa kiasi kidogo ambacho hakiwezi kutoa faida ya kubadilisha maisha.

Naye Msofe kutoka Morogoro anasema, tatizo la wakopaji Watanzania si waaminifu hivyo inawafanya wakopeshaji kuweka mazingira magumu.

Pia ikumbukwe kuwa wakopeshaji nao wapo kibiashara zaidi, si kwa nia ya kuinua wajasiriamali.

Mwandishi wa safu hii anashukuru kwa maoni yote yaliyotolewa, anakaribisha maoni mengine kutoka kwa wataalamu wa benki mbalimbali kwa lengo la kujenga nchi yetu na si kubomoa.



Kwa nini wajasiriamali hukopa, hawafanikiwi? - 2


WIKI iliyopita katika safu hii tuliangalia kwa kifupi ni kwanini wajasiriamali wengi na wafanyabiashara wa kati, pamoja na kukopa kwenye taasisi za fedha au benki wanashindwa kufikia malengo yao.

Leo tutachapisha maoni mbalimbali ya wasomaji wa safu hii ambao wameyatoa katika kuelezea changamoto hiyo inayowakabili wajasiriamali.

Mmojawapo wa wasomaji hao aliyejitambulisha kuwa ni Alexander kutoka Dar es Salaam, anasema tatizo kubwa kabisa ni wajasiriamali wengi wanakuwa hawana ndoto ya kufanya wanachotaka, hivyo wanapokopeshwa fedha hizo hushindwa kuendelea.

Matokeo yake hujikuta wakitangatanga katika biashara nyingi kwa kuwa hawakujua wanataka kufanya nini.

Msomaji mwingine kutoka Mwanza ambaye hakujitambulisha jina lake alisema kuwa, taasisi nyingi za fedha ama benki zimekuwa ni kikwazo kwa wajasiriamali wadogo na wakati.

Anasema amekutana na adha ya kusotea mkopo japokuwa amekwisha kamilisha taratibu zote zinazohitajika katika benki aliyoiombea mkopo ikiwepo hati ya nyumba, huu ni mwezi wa pili anazungushwazungushwa na kila akiulizia anaambiwa ripoti imetumwa Dar es Salaam, hivyo kumfanya kushindwa kutimiza malengo aliyojiwekea.

Andondile Anjawe kutoka Ludewa, anasema katika mambo yanayoumiza wajasiriamali kwenye mikopo na kutolea mfano wa benki aliyoomba mkopo, ni zile gharama mbalimbali zinazotozwa kabla ya kupata mkopo husika.

Anasema unalipia gharama ya mkopo, pili unalipia mhuri, tatu unalipia mahakamani hivyo unajikuta mkopo wote unamalizika kabla hujaushika mkononi.

Hapo hapo bado unatakiwa kurudisha mkopo huo mwezi unaofuata baada ya kuupata.

Maoni mengine yaliyotolewa na mjasiriamali ambaye hakutaja jina lake anasema wengi wana sifa za kukopa kiasi kidogo ambacho hakiwezi toa faida ya kubadilisha maisha.

Pia familia inachangia kukwama akizungumzia familia za Kitanzania mtu akiwa na maisha mazuri kidogo ndugu wanajikusanya kwake.

Jambo lingine anasema ni kwamba, mikopo mingi hukopwa kwa ajili ya ubarikio, harusi ama shughuli nyingine na si kufanyia kazi ya kuzalisha.

Vile vile kodi kubwa na ushuru, pia benki nyingi zinadai fidia kubwa, pamoja na ugumu wa maisha kiasi kwamba mkopo unaotoka mwingine anaweza kulipia ada ya mtoto au kununulia chakula.

Msomaji mwingine anasema katika sekta ya biashara ukitaka kukopa inabidi uwe na mtaji wako kwanza.

Tatizo la ukopaji wa vikundi ni kulaza deni likiwa kubwa wote mnakatwa akiba zenu.

Mkopo binafsi ni mgumu kwa kuwa unawashinda wengi lazima uwe na hati ya nyumba, mdhamini naye anataka kupewa kitu kidogo, au itafika siku atakuomba umkopeshe hivyo hela uliyoipata unaanza kuigawa kwa mambo mengine.

Msomaji mwingine wa safu hii, Elimringi Mero anatolea mfano benki moja iliyoko Dar es Salaam, ambayo wafanyakazi walifika dukani kwake eneo la Bunju B wakihamasisha wafanyabiashara wadogo wafungue akaunti na kupewa mikopo, kigezo ni biashara na leseni yenye umri wa mwaka mmoja, na dhamana ni duka lake.

Hivyo alihamasika kujiunga, lakini chakushangaza alipotaka mkopo aliambiwa apelike wadhamini watatu wenye vitanda na magodoro, pamoja na kusema ana nyumba ambayo haijapauliwa aligonga mwamba.

Anasema akaunti yake ilikuwa na sh 30,000 baada ya miezi sita akataka alipotaka kuchukua aliambiwa haina pesa na kuambiwa kila mwezi wanakata sh 5,000. Hivyo mtaji wake ulizidi kushuka.

Naye Msofe kutoka Morogoro anasema, tatizo la wakopaji Watanzania si waaminifu hivyo inawafanya wakopeshaji kuweka mazingira magumu.

Pia ikumbukwe kuwa, wakopeshaji nao wapo kibiashara zaidi si kwa nia ya kuinua wajasiriamali.

Mwandishi wa safu hii anashukuru kwa maoni yote yaliyotolewa, anakaribisha maoni mengine kutoka kwa wataalamu wa benki mbalimbali kwa lengo la kujenga nchi yetu na si kubomoa.

Kwa nini wajasiriamali hukopo, hawafanikiwi? - 1


HAKUNA mtu asiyependa kufikia malengo yake aliyojiwekea kwa wakati.

Mara zote wajasiriamali wadogo au wafanyabiashara wa kati wamekuwa wakitamani kupata mafanikio, lakini wanakabiliana na changamoto mbalimbali.

Changamoto hizo ndizo zinazowafanya wasifikie ndoto zao za kuongeza biashara nyingine, ama kupanua biashara zao kwa muda maalumu.

Jambo hili limekuwa ni kilio kwa wajasiriamali wengi ambao wamekuwa wakiomba mikopo katika taasisi mbalimbali za fedha au benki, lakini matokeo yake fedha yote huishia kulipa madeni hayo. Hivyo wanajikuta hawasongi mbele.

Ninajua zipo sababu nyingi sana zinazowafanya wasisonge mbele, lakini leo tutaambiana kwa uchache. Zaidi nitapenda kujifunza kwa wajasiriamali wenyewe ambao nitapenda wanitumie maoni yao kupitia simu yangu ya mkononi ama e-mail yangu ambayo ipo katika safu hii ili tuweze kuyaandika na wengine waweze kupata mwanga.

Mojawapo ya changamoto inayosemwa ni ile ya wakopeshaji wengi kuwa kibiashara zaidi badala ya kulenga kumsaidia mjasiriamali wa kweli.

Wengi wa wakopeshaji hao huweka riba kubwa, lakini pia huwa hawana mafunzo kwa wajasiriamali wanaowakopesha.

Vile vile hawawaachii muda wa kuweza kujikusanya ili warudishe fedha hizo kwa utulivu na amani. Hapa namaanisha kuwa, mtu anapokopa mwezi huu, mwezi ujao anatakiwa kurejesha deni lile.

Pia unaweza ukakuta mjasiriamali huyo biashara yake haiendi vizuri, iwe ni nafaka, mifugo ama duka.

Anaamua kwenda kutafuta mtaji wa kuweza kumuinua, anapokwenda huko anakutana na vikwazo vingi vigumu kama vile hati za nyumba, pamoja na kuwa na wadhamini wa kueleweka wanaofanya kazi.

Mbali na hiyo, unakuta mtu anaomba mkopo mwezi huu anakaa miezi minne baadaye ndipo anaupata mkopo huo, hapo anakuwa ameshachoka na malengo yake yote yamevurugika.

Kwa mfano mtu anapokuja kuomba mkopo mwezi huu, lakini baada ya kukamilisha taratibu zote mkopo huo unatoka baada ya miezi mitatu au miwili.

Hali kama hiyo hurudisha nyuma maendeleo ya mtu anayetaka kusonga mbele. Hebu tujiulize ni watu wangapi hivi sasa wanazo hati za kuwawezesha kupata mkopo?

Je, upatikanaji wa hati hizo unachukua muda gani? ni kiasi gani mtu anapaswa kuwa nacho ili aweze kupatiwa hati hiyo.

Mbali na hilo, je, mkopeshaji anawezaje kuisemea vibaya biashara ya mkopaji? mfano, baada ya kukamilisha taratibu zote za kukopa, inabidi maofisa mikopo kutembelea kwenye eneo husika la biashara, je, ni vema kuanza kuzungumza kwa dharau kuhusu eneo ulilopo la biashara ama biashara unayoifanya?

Ni nani asiyependa kufanya biashara yake katika mazingira bora na mazuri ya kupendeza?

Binafsi nilitegemea maofisa hao badala ya ‘kuponda’ kama Waswahili wanavyosema, biashara ya mtu, ni vema wangemshauri mjasiriamali huyo kujitahidi katika biashara aliyonayo ili aweze kupata eneo zuri zaidi ama kuwa na mazingira mazuri ya kufanyia biashara yake.

Katika safu yetu hii ya ‘Maisha Yetu” leo ninapenda kumkaribisha kila mmoja aweze kutoa maoni yake kuhusiana na changamoto zinazowakabili wajasiriamali katika taasisi za fedha au benki, na wafanye nini ili wajikwamue kutokana na hali hiyo.

Ugumu wa maisha wawatatiza vijana 2


NAKUKARIBISHA katika safu hii ili kupata elimu juu ya maisha yetu ya kila siku.

Wiki iliyopita nilizungumzia vijana wenye umri wa kujitegemea kuendelea kuishi na wazazi wao kutokana na ugumu wa maisha uliopo.

Leo nitaendelea na mada hiyo huku nikizungumzia jinsi gani kijana anayekaa na wazazi wake anapaswa kufanya nini ili kuonesha kama amekomaa.

Ili kuonesha kama umekomaa unapoishi na wazazi wako, onesha kuwa upo nao kwa muda tu, kwa kuwa una mpango wa kwenda kuishi katika eneo lako.

Kabla ya kuondoka nyumbani kwa wazazi ni vizuri ukawaeleza ni lini unatarajia kuanza maisha ya kujitegemea.

Kijana anapokuwa nyumbani kwa wazazi wake anazungukwa na maadili yaliyopo katika nyumba yao.

Kwa mfano atapenda kuangaliwa kwa ukaribu na wazazi wake katika mahitaji yake. Lakini kama kijana huyo anataka aonekane amekuwa akiwa nyumbani kwa wazazi wake ni vema akafanya mambo yote yanayomhusu mwenyewe bila kumtegemea yeyote.

Mfano kufua nguo zake mwenyewe, kusafisha chumba chake, kununua chakula pamoja na kutatua matatizo yake mwenyewe.

Na pale unapogundua kuwa, mama yako anakukumbusha ratiba ya kumuona daktari wako labda wa meno, lakini unaona ya kwamba mambo hayo unayamudu mwenyewe ni vema ukawaeleza kuwa unafurahi vile wazazi wanavyokufanyia lakini hapo ulipofikia una uwezo wa kujiongoza mwenyewe.

Pia ni vema kuchanganua uhusiano uliopo baina yako na wazazi wako. Elewa unapokaa na wazazi wako sebuleni muda wa jioni watakukumbusha kuhusu kufuata maadili mema, mila na desturi pamoja na jinsi ya kuishi na watu.

Lakini ukumbuke kuwa hivi sasa umekua, uhusiano na wazazi wako inabidi ubadilike, badala ya kuzungumza nao kama mtoto mdogo inakubidi uzungumze nao kama mkubwa mwenzao kwa kuzingatia heshima na maadili bora.

Zungumza nao kuhusu matarajio yao kwako na wanatarajia nini kuhusu mipango yako ya kujitegemea.

Kama kijana katika familia yako, je, unachangia kitu chochote? Kama unataka kujihisi kuwa sasa ni mtu mzima hata kama unaishi na wazazi wako, inabidi uchangie katika nyumba ya wazazi wako chakula na mambo mengine.

Ni vema kuheshimu mawazo ya wazazi wako kwa marafiki wanao kutembelea. Kama una uhusiano na kimapenzi si vizuri kulala na rafiki yako huyo chumba kimoja kwenye nyumba ya wazazi wako. Heshimu nyumba ya wazazi wako kwa kutokuruhusu jambo hilo kufanyika kwenye nyumba ya wazazi wako.

Hii ni kutokana na mila na desturi zilizopo katika familia nyingi.

Ni vema wazazi wako wakajua ratiba zako vizuri ili endapo ikatokea umechelewa kurudi nyumbani wasipate wasiwasi au utakapowagongea usiku wakiwa wamelala wajue vema ulipokuwa, hii itakufanya uheshimike katika familia yako.

Jione wewe kuwa ni mgeni katika nyumba ya wazazi wako. Pale unapotaka kula kitu chochote ni vema ukaomba ruhusa badala ya kujichukulia tu kama ni mali yako.



Ugumu wa Maisha wawatatiza vijana


NAMSHUKURU Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kukutana nawe tena katika safu hii inayokujia kila Alhamisi.

Katika miaka ya hivi karibuni vijana wengi wenye umri wa kujitegemea wamekuwa wakiishi na wazazi wao kwa kuogopa kupanga kutokana na changamoto mbalimbali zilizopo.

Kuendelea kuishi na wazazi baada ya kuhitimu chuo, ni jambo linalorudisha nyuma fikra za kijana au anakuwa na mawazo ya kudumaa.

Ukweli ni kwamba, vijana wa kiume wenye umri miaka 25 na 34 siku hizi wamekuwa wakirudi nyumbani kwa wazazi wao kwa ajili ya kuangalia video na michezo mbalimbali katika nyumba za wazazi wao.

Vijana hao wamekuwa wakiukataa ukweli halisi kuwa wamekwishakuwa wakubwa na wanapaswa kujitegemea.

Vijana wa aina hiyo wamekuwa wavivu, hawapendi kujishughulisha katika shughuli mbalimbali, wengi wao wakiwa wanaringia utajiri au mali za wazazi wao. Bila kufikiri ni jinsi gani wazazi hao wamezipata hizo mali.

Mazingira ya utamaduni wa kisasa nayo yamechangia kuwaathiri vijana hao, ongezeko la idadi ya vijana hao kurudi nyumbani kwa wazazi kumesababishwa na sababu mbalimbali.

Sababu mojawapo ni gharama kubwa za elimu ya juu. Unakuta kipindi cha likizo kijana anaamua kurudi nyumbani kwa wazazi wake ili kukwepa gharama za kuishi hosteli kipindi kile cha likizo.

Ikizingatiwa kuwa bodi ya mikopo imekuwa ikitoa kiasi kidogo cha mikopo hata pale mwanafunzi anapomaliza anajikuta bado ana deni liko mbele yake.

Ukosefu wa ajira kwa vijana hao kuanzia miaka ya 1970, kipato kwa vijana hao kimekuwa kikishuka, na soko la ajira limekuwa ni la ushindani mkubwa. Jambo hili limefanya mambo yawe mabaya.

Vile vile ongezeko la mahitaji katika elimu. Katika miaka ya nyuma mtu aliweza kupata kazi akiwa na cheti kidato cha sita tu.

Lakini hivi sasa soko la ajira linahitaji angalau awe na digrii, ila kikwazo kipo pale shule inapokuwa ya gharama ili kufikia malengo ambayo mtu amejipangia, hivyo inachukua muda mrefu kwa kijana kuweza kujitegemea kiuchumi.

Hivi sasa mtu anatumia zaidi ya nusu ya kipato chake kwa ajili ya gharama za nyumba.

Kutokana na gharama hizo,vijana kuwa na maeneo yao ya kuishi inakuwa ni vigumu.

Miaka ya zamani wazazi walikuwa na muda mzuri wa kukaa na watoto wao, lakini katika miaka ya hivi karibuni wazazi wamekuwa wakitumia muda mwingi wawapo maofisini hivyo kijana anapokuwa na umri wa kujitegemea, wazazi wake huona fahari kuendelea kuishi naye nyumbani.

Hivyo kwa mazingira hayo utaona ni kwa jinsi gani vijana wa siku hizi wamekuwa ni wavivu na wasiopenda kujituma.

Hivyo basi kutokana na mazingira haya, si busara kwa vijana waliofikisha umri wa kutengana na wazazi wao kuwaambia waondoke.

Kwa changamoto hizo utakuwa na sababu maalumu ya kwanini unarudi nyumbani na kuishi na wazazi wako.

Kwa miaka ya zamani vijana wengi walikuwa wakipenda kuficha mambo yao, lakini siku hizi mambo yamebadilika, vijana wanakuwa wazi katika kila jambo kwa wazazi wao ndio maana wanaendelea kuishi nyumbani.

Vijana wa zamani walikuwa wakiondoka nyumbani kwa kuwa walikuwa hawataki mambo yao yajulikane na kila mtu.

Imeandikwa kwa msaada wa mashirika ya habari.

Twitter Facebook